Mshumaa wasababisha vifo vya watoto wanne wa familia moja Lindi

Nachingwea. Watoto wanne wa familia moja, wakazi wa Kijiji cha Mazoezi, wilayani Nachingwea, Mkoa wa Lindi, wamefariki dunia kwa kuungua na moto uliosababishwa na mshumaa wakiwa chumbani kwao.

Watoto hao, waliokuwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Nambano, ni Hassan Juma (11), mwanafunzi wa darasa la tano, Shufaa Juma (9), mwanafunzi wa darasa la tatu, Basrat Juma (6), mwanafunzi wa darasa la kwanza, na Izdat Boniface (4).

Leo Jumapili, Februari 16, 2025, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, Andrew Ngasa, amezungumza na waandishi wa habari akisema tukio hilo limetokea jana Jumamosi saa 3 usiku.

Amesema watoto hao walikuwa wanaishi na mama yao, Maua Mshamu (43), ambaye aliwaacha ndani, na watoto hao wakawasha mshumaa kwa lengo la kupata mwanga ambapo waliuweka karibu na pazia la chumba walichokuwa wamelala.

Ngasa amesema wakati watoto wakiwa ndani, mama huyo alitoka kwenda kumtafuta mwanawe mwingine aliyekuwa amechelewa kurudi nyumbani.

“Maua Mshamu amepoteza watoto wake wawili, ambao ni Hassan Juma na Shufaa Juma, hawa wengine, Basrat na Izdat, ni wajukuu wake,” amesema Kamanda Ngasa.

“Watoto hao walikuwa wamelala chumba kimoja huku mshumaa ukiwa unawaka, na mama yao alikuwa ametoka zaidi ya umbali wa mita 400 kwenda kumtafuta mtoto wake mwingine aliyekuwa amechelewa kurudi,” amesema kamanda huyo.

Amesema chanzo cha tukio hilo ni kuwaacha watoto ndani ya nyumba bila uangalizi, ambapo watoto hao waliwasha mshumaa kwa lengo la kupata mwanga, ndipo moto huo uliunguza neti, godoro, na vitu vingine vilivyokuwamo ndani.

Kamanda huyo amesema miili ya watoto hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea, na uchunguzi wa kitabibu ukikamilika, wataruhusu taratibu za mazishi kuendelea.

Ngasa ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kuwa waangalifu na kuhakikisha wanawaacha watoto na watu wazima wanapotoka majumbani mwao, hususan nyakati za usiku.

Aidha, wametakiwa kuwa waangalifu na vitu vinavyoweza kusababisha ajali ya moto kama vile mishumaa, viberiti, na wakati mwingine mafuta ya petroli na dizeli, kwani ni vitu hatari vinapoachwa kwenye makazi ya watu.

Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Fatuma Sadick, amesema alikuwa amekaa nyumbani kwake na akastukia moshi mzito ukitokea kwenye nyumba hiyo, ndipo alipokwenda na kukuta nyumba imeshateketea na watoto wameshafariki dunia.

“Ni huzuni sana kwa kweli, watoto wamekutwa tayari wameshafariki, na mama yao alipokuwa anarudi, akakuta watu wamejaa na watoto wameshatolewa nje wakiwa wameshafariki,” amesema Sadick.

Related Posts