Ndoa inaweza kuwa nzuri au mbaya. Pia, ndoa inaweza kujengwa au kubomolewa. Wajenzi na wabomozi wa ndoa ni wanandoa.
Ndoa, kama taasisi yoyote ina changamoto zake. Kuna kufanya makosa kwa sababu, kama binadamu yeyote, hufanya makosa.
Pia, yanapofanyika makosa lazima kuwepo na suluhu na namna ya kufikia suluhu. Leo tutaongelea ulazima na umuhimu wa wanandoa kuwa kama daraja au uwili usiotenganishwa wala kuyumbishwa.
Daraja huwa ama na nguzo mbili, ingawa kutokana na kukua kwa teknolojia, kuna madaraja yana nguzo moja. Pamoja na kuwa na nguzo moja, madaraja yote huwa na sehemu kuu mbili, yaani sehemu ya kuingilia na kutokea.
Ili daraja lifae, kuwa na nguvu, lihimili mikiki, na kutumika, lazima nguzo mbili zisimame pamoja na kutegemeana ili kufanikisha umuhimu wa kuwapo daraja.
Mfano, upande mmoja wa daraja lazima ujue na kukubaliana au kujenga mazingira wezeshi kwa upande wa pili na wa pili kadhalika kwa upande wa kwanza.
Mfano, kama upande wa kuingilia utaruhusu magari au wavukaji wengi, upande wa pili utashindwa na daraja litayumba au kushindwa kufanya kazi yake ya kuvusha watu na vitu.
Udaraja katika ndoa unajengwa kwa njia mbalimbali, zikiwemo:
Mosi, kukubaliana. Kila kinachoingia au kutoka lazima kipitie sehemu mbili na kubebwa na nguzo mbili au nguzo moja ambayo katika ndoa ni ushirika na wawili.
Hapa lazima tukazie. Tunaongelea ndoa ya mke na mume mmoja. Kwa ndoa za mitala, udaraja unawezekana japo kwa tabu. Huko hatutaenda.
Katika dhana ya kulindana, lazima wawili wawe kama nyuki au siafu wanapojilinda au kulinda mzinga au shimo lao.
Ukiangalia uhohehahe na utepetevu wa wadudu tajwa, utagundua kuwa bila kushirikiana na kuhamiana, si chochote si lolote. Na wanandoa kadhalika. Mkishikamana, kulindana na kuhamiana, wengine watawaogopa. Mkibomoana inakuwa rahisi maadui ambao ni wengi kumalizia. Katika kulindana, lazima kuwa kulihali. Mpendane, mheshimiane, mshirikiane, mhifadhiane, na kuaminiana. Mfano, mkianza kuitana viatu na majina mengine mabaya, wengine watawaita hata makanyagio.
Kila kitu mnacho na mna uwezo kubomoa au kujenga, kusuka au kunyoa. Tutatoa visa viwili vinavyotuhusu. Cha kwanza, Nkwazi alitembelea rafiki yake mmoja aishie Canada. Siku ya kwanza kufika tu, baba alimkaribisha Nkwazi kwa shangwe. Kitu kimoja kilitibua kila kitu.
Jamaa alikuwa akimfokea mkewe mbele ya mgeni kama mtoto mtoto mdogo. Hata mtoto mdogo huwezi kumfokea na kumdhalilisha hivyo. Jambo hili lilimuudhi Nkwazi kiasi cha kumwambia mwenyeji wake kuwa asingerudi katika nyumba yake.
Mwenyeji alishangaa na kustuka na kuuliza “kwanini.” Nkwazi alimjibu kuwa hakupenda anavyomdhalilisha mkewe hata mbele ya mgeni kitu ambacho kwa Waswahili ni dharau hata kwa mgeni. Jamaa aliahidi kujirekebisha na mambo yakaisha
Cha pili, kabla ya Nesaa kuja Canada, marafiki zake Nkwazi walizoea kuuliza ana mke wa aina gani. Aliwajibu kuwa madam huwa ni mtu wa kupenda amani. Ajabu ya maajabu, marafiki zake karibu wote, walianza kumuita Nesaa Madam jina ambalo lilimkaa hadi tunahama mkoa ule tulikofikia.
Hata kwenye mapokezi yake uwanja wa ndege, marafiki walionyesha wazi heshima na aina fulani ya woga kulingana na Nkwazi alivyokuwa amemjenga Nesaa ambaye kiumri alikuwa mdogo kuliko marafiki wa Nkwazi.
Kwanini rafiki wa Nkwazi aliyemkaripia mkewe mbele ya mgeni aliamua kuachana na tabia hiyo? Jibu ni rahisi kuwa mwenzake alimfundisha tabia ya kumjali na kumheshimu mkewe.
Kwanini marafiki wa Nkwazi, kwa pamoja, walimuita Nesaa Madam kama ishara ya heshima? Ni kwa sababu Nkwazi alimjenga badala ya kumbomoa.
Somo kubwa hapa ni kwamba mwanandoa anao uwezo wa kumjenga, kumbomoa, kumheshimisha au kumdharaulisha mwenzake.
Mwisho, kila mwanandoa anao uwezo huu. Hivyo, ili mheshimike, lazima mjiheshimu na kuheshimiana. Kufanya hivyo, lazima kuwa na tabia za haki, usawa, upendom kulindana, kuhamiana, na kutegemeana.
Akitukanwa au kudharauliwa mwenzio, nawe kadhalika unatukanwa au kudharauliwa. Kadhalika, akiheshimiwa mwenzio nawe kadhalika unaheshimika.
Hapa kuna faida bila hasara. Hivyo, wanandoa, wajue ni daraja lililojengwa na nguzo mbili yaani mke na mume.