USISHANGAE bwana! Ndivyo ukweli ulivyo, timu za Mashujaa, JKT Tanzania, Fountain Gate na Dodoma Jiji zilizopo ligi Kuu Bara, hazijaonja ushindi tangu mwaka 2025 ulipoingia.
Kipigo cha jana kwa Mashujaa cha mabao 2-0 kutoka kwa Azam, kimeifanya timu hiyo kufikisha jumla ya dakika 720 sawa na michezo minane ya Ligi Kuu bila ya ushindi, kwani mara ya mwisho ilishinda dhidi ya Namungo nyumbani bao 1-0 mechi iliyopigwa Novemba 23, mwaka jana.
Katika michezo hiyo minane, Mashujaa imechapwa minne na kutoka sare pia minne ikifunga jumla ya mabao matano na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 11, hali inayochochea presha kwa kocha wa kikosi hicho, Mohamed Abdallah ‘Baresi’.
JKT Tanzania iliyovunjiwa rekodi ya kutopoteza mchezo ikiwa nyumbani dhidi ya Singida Black Stars ilipochapwa bao 1-0, imecheza pia michezo minane bila ya ushindi tangu ilipoifunga Fountain Gate bao 1-0, Novemba 29, mwaka jana.
Katika michezo hiyo, JKT imechapwa minne na kutoka sare minne, ikifunga mabao mawili tu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba.
Kwa upande wa Fountain Gate imecheza michezo sita ya Ligi Kuu bila kuonja ladha ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga Coastal Union kwa mabao 3-2, katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Kwaraa Babati Manyara Desemba 13, mwaka jana.
Katika michezo hiyo sita, Fountain Gate imepoteza mitano na kutoka sare mmoja tu na safu ya ushambuliaji imefunga mabao mawili tu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 15, ikiwa ni wastani wa kuruhusu mabao mawili kila mechi.
Kwa upande wa Dodoma Jiji angalau haina muda mrefu sana tangu mara ya mwisho ilipoifunga Mashujaa mabao 3-1, Desemba 28, 2024 kwa sababu kuanzia hapo imecheza michezo miwili tu ya Ligi Kuu Bara, ikipoteza mmoja na kutoka sare mmoja.
Kikosi hicho kilichapwa nyumbani bao 1-0 na Pamba Jiji na kutoka sare ugenini ya mabao 2-2, mbele ya Namungo, ikiwa imefunga mabao mawili na kuruhusu matatu, ikiwa ni tofauti na wapinzani wake ambao hawajashinda kwa muda mrefu.
Akizungumza hali ya kikosi cha Mashujaa, kocha wa timu hiyo, Mohamed Abdallah ‘Baresi’ alisema wachezaji wamekosa morali ya upambanaji kutokana na kitendo cha kutopata matokeo chanya kwa muda mrefu, ingawa anaendelea kuwajenga kisaikolojia.
“Kadri unavyopoteza ndivyo ambavyo hata hali ya kujiamini kwa wachezaji inapungua, angalia mfano mechi yetu na Azam, hatujacheza vibaya sana ila kuna wakati unaona tunafanya makosa ya kizembe yanayowapa faida wapinzani wetu,” alisema.
Kocha wa Fountain Gate, Roberto Matano alisema changamoto kubwa ndani ya timu hiyo ni kukosa muunganiko mzuri wa safu ya ulinzi na kiungo, huku akieleza bado anaendelea kupambana na hali iliyopo ili kukitengeneza kikosi bora cha ushindani.
Kwa upande wa Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally alisema upana wa kikosi ni changamoto kubwa inayomkabili kwani baadhi ya nyota wa timu hiyo wamekuwa wakicheza mara kwa mara, hali inayowasababishia uchomvu kutokana na kutumika sana kikosini.
“Kwa mfano ukiangalia mchezo wetu wa mwisho na Singida Black Stars, beki wa kati, Wilson Nangu na kiungo Hassan Kapalata walishindwa kuendelea na mechi mapema tu, hii ilisababisha kufanya mabadiliko ya lazima na kutuharibia malengo yetu.”