MSHAMBULIAJI wa FC Juarez ya Mexico, Opah Clement anatarajia kucheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Chama la Mtanzania mwenzake, Enekia Lunyamila, Mazaltan.
Hii ni mara ya kwanza kwa nyota huyo wa zamani wa Simba Queens kuitumikia timu kutoka Mexico ambayo pia anachezea mbongo mwenzie beki Julietha Singano ambaye yuko nchini humo kwa msimu wa tatu sasa.
Opah tayari ameanza mazoezi na timu hiyo ambayo wiki iliyopita ilimtambulisha kwa ukubwa wake Februari 09 mwaka huu akitokea Henan Jianye ya nchini China na juzi ilimtakia heri kwenye siku yake ya kuzaliwa.
Mchezo huo utapigwa leo Oktoba 17 na Chama la kina Opah likiwa nyumbani dhidi ya Mazaltan ambayo iko mkiani ikiwa haijaonja ladha ya ushindi wowote kwenye mechi nane za ligi, huku Juarez ikiwa nafasi ya sita kwenye msimamo na pointi 17, ushindi mechi tano, sare mbili na kupoteza mchezo mmoja.
Msimu uliopita zilipokutana timu hizo, Chama la kina Opah liliondoka na ushindi wa mechi zote mbili ikishinda nyumbani mabao 3-2 na kuivuruga chama la Lunyamila ugenini mabao 6-0.