Simchimba ajichomoa mbio ufungaji | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI wa Geita Gold, Andrew Simchimba amesema licha ya kasi yake katika kufunga mabao akiwa na kikosi hicho msimu huu, ila hana malengo ya kutwaa kiatu cha ufungaji bora, zaidi ya kutaka kuipambania timu hiyo kwanza kurejea Ligi Kuu.

Simchimba anashika nafasi ya pili kwa mastaa waliofunga mabao mengi hadi sasa baada ya kutupia kambani 13, sawa na nyota wa TMA FC, Abdulaziz Shahame ‘Haaland’, wakipitwa bao moja na kinara, Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar anayeongoza na 14.

Akizungumza na Mwanaspoti, Simchimba alisema moja ya malengo yao makubwa ni kushika nafasi ya kwanza na kupanda Ligi Kuu Bara moja kwa moja, japo kama itatokea pia akaibuka mfungaji bora msimu huu itakuwa ni jambo nzuri kwake maishani mwake.

“Ukiangalia pointi ilizonazo timu sita za juu utaona bado tuna kazi ya kufanya ili kutimiza malengo hayo kwa sababu gepu sio kubwa, malengo yetu kwanza kama wachezaji ni kuirejesha Geita Ligi Kuu Bara, kisha mambo mengine yatafuata.”

Nyota huyo aliyewahi kuzichezea timu mbalimbali zikiwemo za Azam FC, Singida Black Stars (zamani Ihefu) na Coastal Union, alisema licha ya kushika nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi, ila hawatabweteka bali wataendelea kupambana zaidi.

Related Posts