Dar es Salaam. Wakati watumishi wa afya waliokuwa chini ya miradi ya USAID wakisimamishwa kazi bila malipo, baadhi wameelezea hali ngumu ya maisha wanayopitia, huku wadau wakiitaka Serikali kuchukua hatua kunusuru ujuzi, kufanya tathmini ya athari na kuzikabili kisayansi.
Sintofahamu hiyo imekuja baada ya Januari 20, 2025 Rais wa Marekani Donald Trump kusitisha kwa siku 90 misaada ya maendeleo ya nje, kupisha tathmini ya ufanisi na uwiano na sera yake ya kigeni, hali iliyowalazimu wasimamizi wa ufadhili nchini kusitisha miradi.
Baadhi ya watumishi waliofanya kazi chini ya miradi ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), wamesema hawakupata mishahara ya Januari hali iliyowaingiza kwenye ugumu wa maisha pasipo kutarajia.
Pia wanaeleza hawana uhakika wa kurejeshwa kazini baada ya likizo ya hiari kumalizika Aprili 24, 2025.
Mmoja wa watumishi hao aliyeomba kutokutajwa jina amelieleza Mwananchi kuwa, hakuwahi kudhani angeingia katika janga la kukosa ajira kwa kuwa alikuwa na mkataba wa muda mrefu.
Mtumishi huyo mwenye mke na watoto watatu, amesema anapitia changamoto ya ukata baada ya kukosa mshahara wa Januari kutokana na agizo la Rais Trump.
Mtumishi huyo aliyekuwa amejiondoa kwenye ajira serikalini miaka kadhaa iliyopita amesema: “Januari hatukupata mshahara, hivyo ikabidi tuendelee kwenda kazini kama kawaida. Lakini baadaye tuliambiwa tusimame kupisha siku 90.”
“Nimelipa kodi ya nyumba mwanzoni mwa Januari kwa mwaka mzima, karo za watoto na mambo mengine muhimu nikabaki sina fedha. Matarajio yangu mshahara wa Januari ungenisaidia kuendesha familia.”
Mtumishi huyo anayeishi Makongo Juu jijini Dar es Salaam, amesema: “Kwa sasa nimemuomba mwenye nyumba msaada atafute mpangaji mwingine ili anirudishie ile kodi nikatafute nyumba ya bei nafuu nipate na fedha za mtaji wa biashara yoyote nifanye. Sina uhakika wa kurudi kwenye ajira, natafuta mbadala mapema.”
“Tulianza kufanyia kazi nyumbani, ilipofika mwisho wa mwezi hatukuingiziwa mshahara wa Januari. Tayari tumeanza kuonja makali kwani Januari ina mambo mengi kama unavyojua, bado ukose mshahara tunapitia wakati mgumu sana,” amesema mfanyakazi mwingine wa shirika lingine.
Kutokana na wanayoyapitia, mtaalamu wa saikolojia, John Ambrose amesema watumishi hao wataathirika kisaikolojia kwa kuwa hawakubaliani na kilichotokea, akieleza mhusika anaweza kupata hasira, lawama na shutuma hivyo anaweza kufanya mambo yasiyo sawa. Ameshauri wakubaliane na hali iliyotokea na kuacha maisha yaendelee.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko ameitaka Serikali kuhakikisha inatafuta ufumbuzi wa haraka ili kulinda ujuzi na kuondoa usumbufu kwa wananchi.
“Tunapendekeza hatua za haraka kunusuru hali hii, hatuwezi kukwepa wajibu huo, Serikali iendelee kufanya tathimini ya athari na kuzikabili kisayansi,” amesema.
Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA), Alexander Baluhya amesema kuondoka kwa watumishi wengi kwa wakati mmoja katika vituo vya afya ni changamoto kubwa iliyokuja wakati ambao Taifa halijajiandaa, watumishi hawakuwa wamejiandaa. Amesema huenda Serikali itakuja na mpango kunusuru upungufu.
“Serikali inapaswa kuwajibika, tayari kulikuwa na upungufu hivyo utaongezeka. Wanaoathirika si wauguzi waliobaki kwa mzigo mkubwa wa kazi, bali wananchi hawatapata huduma zao kwa wakati, naamini lazima Serikali itakuwa na njia mbadala kuona namna ya kupunguza changamoto hii,” amesema.
Amesema watumishi hawana kosa lolote, hivyo stahiki zao lazima ziangaliwe kwa makini na zisimamiwe kulingana na mikataba yao.
Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), Fadhili Hezekiah amesema takwimu ni muhimu kwa nchi kujua ni wangapi wameathirika na kwamba, wafamasia wengi walikuwepo kwenye miradi ya Ukimwi.
“Serikali ijue kuna upungufu kiasi gani. Tathmini ya kina nini kifanyike kwa wakati huu. Huenda wapo waliolipwa asilimia 50 na Serikali na asilimia 50 na mashirika hili pia tulijue.
“Pengine athari inaweza isionekane moja kwa moja kwenye tafiti na uwezeshaji lakini naamini zitaonekana katika huduma,” amesema.
Tayari Halmashauri ya Mji Mafinga imetenga fedha kupitia mapato ya ndani ili kuendelea na baadhi ya watumishi hao.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Regnant Kivinge amesema Baraza la Madiwani limetenga Sh15.6 milioni kwa ajili ya malipo ya watumishi waliokuwa wakilipwa na taasisi za Benjamin William Mkapa Foundation na Mpango wa USAID Afya Yangu.
“Tumeweka makubaliano ya kila mwezi, baada ya kuona haya mashirika yametoa barua ya kusitisha ili wananchi wetu wasiathirike imebidi tufanye maamuzi ya kulipia fedha zetu za ndani kati ya watumishi 73 tumewabakiza 26 waliokuwa wakifanya kazi kwenye maeneo muhimu,” amesema.
Kivinge amesema walichagua maeneo muhimu manane hasa katika masuala ya Ukimwi, saratani ya shingo ya kizazi, uzazi wa mpango na mengine muhimu.
Hata hivyo, Februari 12, Mkurugenzi Idara ya Tiba, Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea aliliambia Mwananchi kuwa tayari uchambuzi umeshafanyika kuhusiana na upungufu utakaotokea na vituo vimeshafanya marekebisho kwa kuangalia mbadala.
“Kama ni hospitali, kituo cha afya, wameshaangalia maeneo ambayo yatakuwa na upungufu na kuweza kufanya mtawazo wa watumishi wale ambao wameajiriwa na Serikali ili waweze kujaza hizo nafasi huduma zisitetereke,” alisema Dk Nyembea.
Katika hatua nyingine, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Siha, Paschal Mbotta akijibu swali la mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Dancan Urasa alisema watumishi sita ndio walioathiriwa na uamuzi huo.
Akizungumza kwenye kikao cha kawaida cha baraza la madiwani la halmshauri hiyo Februari 14, amesema watumishi hao ajira zao zimekwama.
“Athari iliyopo ni kwamba watumishi sita katika Hospitali ya Wilaya ya Siha mikataba yao imesitishwa baada ya tangazo lile, lakini wapo wengine ambao idadi yao bado sijaipata, tutafuatilia sehemu mbalimbali ikiwamo Ashengai na Ngarenairobi ili kupata idadi kamili ya watumishi watakaoathirika,” amesema.
Hata hivyo, amesema watumishi hao wamebakizwa ili waendelee kusaidia wagonjwa ambao wamekuwa wakiwafuatilia majumbani na kuwatibu ambao wanaishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Kaimu Mkurungenzi Mtendaji wa halmshauri hiyo, Mark Masue amesema ofisi ya mkurungenzi haijapokea maelekezo yoyote kutoka serikalini.
“Tunaendelea na utaratibu huu wakati tukisubiri maelekezo ya Serikali kuhusu suala lao,” amesema.