Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) amesema sio sawa kwa bara la Afrika kutokuwa na kiti cha mwakilishi wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na ameahidi kufanya kazi na Umoja wa Afrika na nchi wanachama ili kuhakikisha kuwa nchi za Afrika zinapata mwakilishi wa kudumu katika Baraza la Usalama.
Akihutubia jana Jumapili kwenye Mkutano wa Umoja wa Viongozi wa Afrika huko Addis Ababa mji mkuu wa Ethiopia, Antonio Guterres aliashiria kauli mbiu ya mkutano huo inayosema “Haki kwa Ajili ya Waafrika na Kulipwa Fidia Watu Wenye Asili ya Afrika” alikiri kuwa harakati za kupambana na ukoloni na kupigania uhuru hazijatatua changamoto za msingi za Waafrika ambazo ni urithi wa ukoloni na biashara ya utumwa kupitia bahari ya Atlantiki.
Maelfu ya Waafrika waliuzwa na wazungu kama watumwa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amesisitiza nia ya kufanyiwa marekebisho taasisi hiyo anayoiongoza na kutaja kukosekana mwakilishi wa nchi za Kiafrika katika Baraza la Usalama kuwa ni jambo lisilofaa.
Baraza la Usalama la UN lina nchi wanachama 15 ambapo nchi tano yaani Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na Russia ni wanachama wa kudumu na nchi 10 nyingine ni wanachama wasio wa kudumu.