Mwanza. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imesema kila mwaka inapokea zaidi ya notisi 500 za wananchi kuishtaki Serikali kutokana na kukerwa au kutoridhishwa na huduma wanazopata kutoka kwa watendaji na viongozi wake.
Hayo yamesemwa leo, Jumatatu, Februari 17, 2025, na Kaimu Mkurugenzi wa Uratibu na Ushauri wa ofisi hiyo, Neema Ringo, wakati wa uzinduzi wa kamati za kisheria na kliniki ya kisheria bila malipo jijini Mwanza. Neema amemwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari.
Amesema hali hiyo inaonyesha namna ambavyo viongozi na watumishi wa Serikali hawafuati utawala wa kisheria ama hawawaelezi sawa sawa wananchi ili waelewe utaratibu ukoje, hivyo kuona haki zao zimekiukwa.
“Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendelea kupokea ongezeko la notisi au nia ya kutaka kuishitaki Serikali mahakamani kutokana na wananchi mbalimbali wanaoona wanakwazwa na namna tunavyowahudumia au namna tunavyotekeleza majukumu yetu kama viongozi.
“Kwa hiyo, wingi wa zile notisi ndio umeamsha hali hii ya kufikiri kwamba umefika wakati tuanzishe hizi kamati ili tuweze kuwasikiliza wananchi kwa utaratibu kabla hawajafikia huko wanapofika kutaka kuishitaki Serikali, lakini pia na wao kuwa na uelewa wa kujua hatua za kufuata ili wasichelewe kupata haki zao,” amesema Neema.
Amesema kutokana na wingi wa notisi hizo, ofisi hiyo imeandaa muongozo wa kusikiliza kwanza wananchi kupitia kamati za ushauri wa kisheria za mikoa ambazo zimeanzishwa kwa mujibu wa sheria, akikitaja kifungu cha 21 cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura ya 268.
Aidha, amesema katika tafiti zao walibaini hakuna mfumo rasmi wa kushughulikia haki za madai nje ya utaratibu wa mahakama ambao umerasimishwa, akieleza kuwa kwa kuanzisha kamati hizo, sheria inarasimisha taratibu za kushughulikia malalamiko ya madai na jinai kabla wananchi hawajaenda mahakamani.
Amesema kamati hizo zitasikiliza malalamiko kwenye ofisi za wakuu wa wilaya na mikoa, lakini pia zitaandaa mikutano ya kliniki za kusikiliza malalamiko ya wananchi, hasa ya kisheria.
Akizindua kamati hizo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewataka wananchi kujitokeza katika kamati hizo kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili, kuliko kusubiri viongozi wa kisiasa, wakiwemo mawaziri, kwenda kulalamika na kulia ili waonewe huruma, kwani maamuzi yao wakati mwingine yanakuwa nje ya utaratibu wa kisheria.
Katika hatua nyingine, Mtanda amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo kujenga utaratibu wa kwenda kupata ushauri wa kitaalamu wa sheria kabla ya kuingia kwenye mikataba na wazabuni mbalimbali ili kuondoa changamoto mbalimbali, ikiwemo kukiukwa kwa mikataba hiyo.
Naye, Mwenyekiti wa kamati hiyo Mkoa wa Mwanza, Subira Mwandambo, amesema kamati hizo zenye wajumbe 12 zitapunguza mashauri dhidi ya Serikali, kupunguza muda mwingi wa mawakili wa Serikali wanaosimamia mashauri hayo na kuokoa fedha za Serikali ambazo inaweza kutumia baada ya kushindwa kesi mahakamani.
Amesema pia, kamati hizo zitaimarisha utawala wa sheria nchini, kulinda shughuli za uwekezaji na maendeleo, kuongeza ushirikiano katika jamii na kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi.