Athari ya vitengo vya ushauri na nasaha kusahauliwa shuleni

Ukosefu wa vitengo madhubuti vya mwongozo na ushauri katika shule nyingi nchini, umewaacha wanafunzi wakikabiliwa na changamoto ikiwa ni pamoja na matatizo ya afya ya akili pamoja na msongo wa mawazo ya kitaaluma.

 Licha ya maagizo ya Serikali yanayosisitiza umuhimu wa huduma hizi, utekelezaji wake umekuwa ukikwamishwa kutokana na uhaba wa wafanyakazi, uelewa mdogo wa umuhimu wake pamoja na ufadhili.

Wadau wa elimu wameitaka Serikali kufanya marekebisho ya haraka ili kuanzisha na kuimarisha huduma za ushauri shuleni, na kuzifanya kuwa sehemu muhimu ya mfumo wa elimu.

 Kwa sasa, shule zinategemea walimu kutumika kama washauri, ambao hawana mafunzo muhimu katika saikolojia ya mtoto au mbinu za ushauri. Hii inaathiri ufanisi wa kushughulikia masuala magumu ya wanafunzi.

 Aidha, shule nyingi hazina miundombinu ya kutoa ushauri wa faragha na siri, hali inayowazuia wanafunzi kutopata msaada.

 Daktari wa saikolojia Eliza Mwakalonge, akizungumza Januari 2, 2025 na gazeti dada la The Citizen alisisitiza uzito wa hali hiyo: “Wanafunzi wengi wanapambana kimya kimya na unyogovu, wasiwasi, na matatizo. Bila msaada wa kitaalamu, changamoto hizi zinaendelea na kudhoofisha utendaji wao wa kitaaluma na ustawi wa jumla.”

 Changamoto za kifamilia, kama talaka na ugumu wa maisha kiuchumi, mara nyingi huacha watoto wakiwa na msongo wa mawazo, hali inayoweza kuathiri tabia na umakini wao darasani.

 Mshauri wa familia, Gerald Mboma alisema: “Mawazo ya umaskini na kutengana kwa familia hakuishii nyumbani, hufuata watoto darasani, na kuathiri umakini na utendaji wao. Shule zinapaswa kuunda mazingira salama kwa wanafunzi hawa.”

 Pia katika upande wa kidigitali umeongeza ugumu wa hali hiyo, ukichangia matatizo kama vile uonevu mtandaoni, maudhui yasiyofaa, na uraibu wa mitandao ya kijamii.

 Mtaalamu wa teknolojia ya elimu, Sarah Masanja, alisema: “Teknoloijia ya dijitali inabadili jinsi watoto wanavyofikiria na kutenda. Bila mwongozo sahihi, wanafunzi wengi wanashindwa kusawazisha maisha yao ya kidigitali na masomo na ukuaji wao binafsi.”

 Ni kwa sababu hiyo anasema kuna umuhimu wa kuwa na washauri wenye ujuzi kusaidia wanafunzi kusimamia changamoto za ulimwengu wa kidijitali.

  Ukosefu wa huduma za ushauri pia unamaanisha kuwa wanafunzi wanakosa mwongozo muhimu wa kazi.

Kadri soko la ajira linavyobadilika, ushauri sahihi juu ya kazi mpya unahitajika ili kuwasaidia wanafunzi kufanya maamuzi sahihi ya baadaye yao.

 Mshauri wa kazi, Grace Munuo alieleza: “Bila ushauri sahihi wa kazi, wanafunzi wengi hufanya maamuzi yasiyo sahihi yanayopunguza fursa zao.”

 Ukosefu wa ushauri pia unachangia matatizo ya tabia yanayozua wasiwasi, kama vile wanafunzi kuandika maudhui yasiyofaa wakati wa mitihani ya kitaifa.

 Katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka 2024 yaliyotangazwa hivi karibuni, watahiniwa watano waliandika matusi kwenye karatasi zao za majibu. Hii inaonyesha hitaji la haraka la kuingilia kati kuhusu afya ya akili na tabia.

 Mtaalamu wa afya ya akili katika Chuo Kikuu cha Aga Khan, Dk Stewart Mbelwa, alisisitiza: “Wanafunzi wanakabiliwa na msongo mkubwa wakati wa hatua muhimu za elimu yao. Hataua za mapema zikichukuliwa, zinaweza kuzuia athari za muda mrefu za kitaaluma na zile binafsi.”

 Ingawa serikali ya Tanzania imetambua umuhimu wa ushauri, changamoto katika utekelezaji zinaendelea kubaki.

 Waraka Na. 6 wa 2022 unahimiza kuimarisha vitengo vya ushauri, lakini shule mara nyingi zinashindwa kuteua washauri wenye sifa na kutegemea walimu wasio na mafunzo maalum. Afisa elimu Jacob Mushi anasema: “Tunahitaji washauri waliofunzwa ambao wanaweza kutoa msaada wa kitaalamu, sio tu walimu wenye nia njema.”

 Wataalamu wanakubaliana kwamba huduma za ushauri na unasihi shuleni ni muhimu kwa maendeleo ya jumla ya wanafunzi.

 Dk Mwakalonge alisema: “Mafunzo ya walimu katika mbinu za ushauri ni muhimu. Shule pia zinapaswa kuajiri washauri walioidhinishwa ambao wana uwezo wa kushughulikia mahitaji ya afya ya akili ya wanafunzi.”

 Miundombinu ni wasiwasi mwingine mkubwa. Masanja alisisitiza umuhimu wa kuwapo kwa siri katika ushauri.

“Ushauri lazima uwe wa faragha na salama. Shule zinahitaji nafasi za faragha ambapo wanafunzi wanaweza kujisikia salama kujadili masuala ya binafsi bila kuogopa kuhukumiwa,”anasema.

 Aidha, wataalamu wanapendekeza utekelezaji mkali wa sera zilizopo. Mshauri wa kazi, Munuo anasisitiza umuhimu wa miongozo iliyo wazi na thabiti kwa shule.

 “Sera zipo, lakini zinahitaji kutekelezwa kwa usahihi ili kuhakikisha vitengo vya ushauri vinapata wafanyakazi wa kutosha na rasilimali,”anasema.

 Kampeni za uhamasishaji ni muhimu kubadilisha mtazamo wa umma kuhusu ushauri na unasihi.

Mwanasaikolojia Anna Kweka anasema wazazi, walimu, na wanafunzi wanahitaji kuelewa kuwa kutafuta msaada ni ishara ya nguvu, sio udhaifu.

‘’ Mabadiliko haya ya mtazamo ni muhimu kwa kuboresha matumizi ya huduma za ushauri,’’ anaeleza.

Pendekezo jingine la wadau ni kujumuishwa kwa elimu ya afya ya akili kwenye mtalaa, ili kukuza mazingira ya usaidizi shuleni.

 Mshauri katika Shule za Sega mkoani Morogoro, Grace Msele, anasema: “Afya ya akili inapaswa kufundishwa pamoja na masomo ya msingi kama hisabati na sayansi. Wanafunzi wanahitaji kuelewa hisia zao na jinsi ya kudhibiti msongo wa mawazo.”

Makala haya yaliyoboreshwa, awali yalichapishwa na gazeti la The Citizen.

Related Posts