Bondia mchinja kuku na kisa cha kupigwa Uganda

Katika maisha kila binadamu anapitia mkasa wake apitia haso zake katika kitabu cha maisha yake kama ilivyokuwa kwa bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Ramadhan Ramadhani lakini jina lake la utani akijulikana kama Chicho na wengi humuita Rama Chicho.

Rama Chicho ambaye anatokea katika mitaa ya Manzese siyo mgeni katika majukwaa ya mchezo wa ngumi za kulipwa kutokana na ukubwa wa rekodi yake licha ya mwenyewe kuwa mgeni katika macho ya wadau wa mchezo huo.

Bondia huyo mwenye rekodi ya kucheza mapambano 21 mpaka sasa kwenye mchezo huo akiwa ameshinda 11, kati ya hayo sita kwa Knockout lakini amepigwa mara tano kati ya hizo moja ni kwa Knockout huku akitoka sare tano.

Rama Chicho anayepigana kwenye uzani wa feather akiwa na hadhi ya nusu nyota ambapo anakamata nafasi ya 20 katika mabondia 57 wa uzani huo wakati duniani akiwa anakamata nafasi ya 651 katika mabondia 1783 wa uzani huo.

Bondia huyo aliyeanza kupanda ulingoni mwaka 2016 katika pambano la kulipwa baada ya kupita sana kwenye ngumi za ridhaa, amefichua mambo mengi aliyokutana nayo kwenye mchezo huo na sababu kubwa iliyosababisha kuwa bondia.

Rama Chicho, anasema sababu kubwa iliopelekea ajifunze mchezo wa ngumi ni kutokana na kuonekana mnyonge mbele ya watoto wenzake waliokuwa wakifanya kazi ya kumuonea kabla ya kuanza mazoezi ya mchezo huo.

“Kilichonifanya nijifunze mchezo huu wakati nilipokuwa mdogo mtaani kwetu nilikuwa naonewa sana na watu waliokuwa wamenizidi umri, kupigwa makonzi kutumwa sana ilikuwa kawaida.

“Nakumbuka ilifika kipindi mtu anataka kupiga kisa zile gololi ambazo tumekuwa tukichezea zamani, nishapigwa sana na walionizi umri yaani wakikuta unacheza wanakupiga halafu wanachukua wao kuchezea.

“Lakini kutokana na hali hiyo ndiyo nilianza mwenyewe kujifunza kwa kupiga ndala na vitu vingine ila kutokana muda kadiri unavyokwenda ndiyo nilianza kutafuta Gym za mazoezi ili kupata usimamizi wa kutosha badala ya kufanya mazoezi peke yangu.

“Nashukuru Mungu baada ya hapo nilipata gym za kuweza kufanya mazoezi, nikaanza kupata mapambano ya ngumi za ridhaa kabla ya kugeukia ngumi za kulipwa japo kuwa kwenye ngumi za ridhaa sikukaa sana, nilicheza mapambano matano pekee.

“Mwaka 2016, ndiyo nilipata nafasi ya kucheza pambano langu la kwanza ambalo nilipoteza kwa pointi dhidi ya Hassan Mgosi ambapo mpaka sasa nashukuru Mungu naendelea kupigana maana ni kazi yangu ambayo nimeichagua na inanipa ugali kila kukicha.

Jambo gani la tofauti ambalo umewahi kukutana nalo kwenye ngumi

“Nadhani ilikuwa kwenye pambano la Safari ya Beach ambapo nilikuwa nacheza na Tampela Mahurusi lakini wakati nilipokuwa kwenye kipindi cha maandalizi nilikutana na balaa ambapo sitoweza kulisahau.

“Nakumbuka siku hiyo nilikuwa nimeenda kukimbia ‘road work’ sasa njiani wakati nakimbia mitaa ya fire, nilishikwa na hali ya kizungunguzu, nikawa sielewi chochote na ilikuwa peke yangu.

“Lakini niliweza kumpigia mwalimu wangu nikamuelezea kwamba nimepatwa na hali ya ajabu, napata kizunguzungu, siwezi kutembea wala kukimbia, mwalimu akaja na bodaboda, akanichukua nikarejea nyumbani.

Kitu gani ambacho huwezi kukisahau kwenye ngumi?

“Kiukweli kuna mwaka nilipata pambano la kwenda kupigana Uganda sasa kwa bahati mbaya mazingira ya chakula yalikuwa tofauti kwa upande wangu maana huku tushazoea kula ugali au wali lakini kule ilikuwa tofauti.

“Kuhusu chakula, nilikuta wanakula ndizi, zimechanganywa na ugali, ulezi hadi wali humohumo, kikanishinda ikawa chakula changu ni mihogo ya kuchemsha ambayo nilikuwa nanunua mtaani.

Lakini siku ya pambano upande wangu ikawa mbaya kwa sababu sehemu ambayo nilikuwa napata mihogo haikuwepo kwa sababu ilikuwa Jumapili, ikanibidi ninunue ndizi zilizoiva  niwe nakula kwa ajili ya kwenda kupigana.

“Binafsi sijawahi kupigana kwa kula ndizi kama tunda, nishazoea napata chakula cha kutosha lakini kwa Uganda ni kama nilipigana na njaa pambano la raundi nane bila ya kupata chakula, nilijitahidi lakini nilipoteza kwa pointi kwa sababu nilimaliza raundi zote.

Una mipango gani kwenye ngumi?

“Kubwa ni kuona nafikia malengo yangu licha ya kuwa mchezo wa ngumi umekuwa na changamoto nyingi hasa za kukosa usimamizi wa watu ambao wanautaalam na wataweza kutufikisha kwenye malengo.

“Lakini kwa upande wangu naendelea kujipanga na nitaendelea kutafuta namna ya kuweza kufikia ndoto za kufika mbali hasa kwenye majukwaa makubwa.

Nje ya ngumi unafanya kazi gani?

“Kazi yangu nje ya ngumi, huwa nachinja kuku pale kwenye soko la Shekilango, kuku mmoja huwa tunachinja kwa Sh 300, sasa inategemea kuna wakati unaweza kupata hadi Sh 50,000 ambayo inategemea na oda za wateja au unakuta mtu mwingine anakupa zaidi ya ile ambayo inayotakiwa.”

Unajua kuna mtu anaweza kuja akakupa hata 1000 kwa ajili ya kumchinjia kuku badala ya 300, mwingine anakuwa hana chenchi au anaamua tu kukusaidia.

Ukiwa na mechi mazoezi unafanya wakati gani?

“Mara nyingi huwa nafanya usiku kwa sababu kuna wakati nataka kupumzika halafu usiku nafanya hadi saa 11 alfajiri  ambayo nikitoka hapo najiandaa kwenda sokoni kuchinja kuku kwa sababu ndiyo kazi ya kila siku na inanisaidia kupata chakula na kuendesha maisha,” anasema Rama Chicho.

Related Posts