Mbeya. Jumla ya kilo milioni 31 za tumbaku zinatarajia kuzalishwa mkoani hapa kwa msimu wa kilimo 2025/26 sambamba na uanzishaji wa mfuko wa majanga kwa wakulima.
Uzalishaji huo umetajwa kuongezeka kutoka wastani wa kilo milioni 19 zilizopatikana msimu wa kilimo 2024/25 kati ya kilo milioni 26 zilizotarajiwa kuzalishwa.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Februari 17, 2025, Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku Wilaya ya Chunya (Chutcu), Isaya Hussen amesema msimu wa 2024/25 hawakuweza kufikia malengo kutokana na changamoto za mvua kubwa ya mawe kuathiri uzalishaji na mabadiliko ya tabianchi.
“Msimu wa kilimo 2024/25 ulikuwa na changamoto ya mvua nyingi za mawe na kusababisha tumbaku kuharibika shambani, mbolea kusombwa na maji hali iliyosababisha kutofikia malengo ya uzalishaji,” amesema.
Isaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Wakulima wa Tumbaku Lupa (Mtanila Amcos), amesema hali hiyo ilisababisha wakulima kuingia hasara kubwa za gharama za uzalishaji.
Isaya amesema ili kufikia malengo wametumia mbinu mbalimbali za uzalishaji sambamba na upandaji miche, kuweka mbolea kwa wakati, kujenga mabani ya kukaushia kwa ubora na kuzingatia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA).
“Msimu huu matarajio ni kuzalisha wastani wa kilo milioni 31 ambazo zinahusisha wakulima 8,000 waliojiunga kwenye vyama vya ushirika,” amesema.
Wakati huohuo, Isaya amesema katika kukabiliana na changamoto za majanga kwenye uzalishaji wameanzisha mfuko wa majanga kwa kuzingatia mpango maalumu kwa kila mkulima kukatwa Sh2,000 kupitia mfuko wa pembejeo.
“Kwa sasa mapokeo ni makubwa tunatarajia mfuko huo kuwa mkombozi kwa wakulima wakipata majanga kwenye uzalishaji kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo hayazuiliki,” amesema.
Kuhusu hali ya uzalishaji shambani, amesema mpaka sasa wastani wa asilimia 30 mpaka 40 wakulima wameanza kuchuma majani ya tumbaku yaliyokauka.
Januari 25 mwaka huu, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbarak Batenga aliagiza vyama vya ushirika wa wakulima wa tumbaku kuanzisha mfuko maalumu wa majanga ili kuwasaidia yanapojitokeza maafa
Agizo la Batenga lilikuja kufuatia ekari 128 za tumbaku kuharibiwa na mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na kunyesha kwa mvua Januari 20, 2025 na kusababisha hasara kwa wakulima.