Kahama. Ujenzi wa daraja linalounganisha mikoa ya Shinyanga na Tabora katika Mto Kasenga linatajwa kuwa suluhisho la usafiri na kuondoa kero kwa wananchi wa mikoa hiyo.
Hayo yameelezwa na Mhandisi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Shinyanga, Evans Maridai leo Februari 17, 2025 akisema kwa sasa upasuaji wa miamba umekamilika.
“Daraja hili lina urefu wa mita 80 na upana wa mita 20 na kwa sasa tumemaliza kupasua miamba na ujenzi huu utasimamiwa kikamilifu hadi ukamilikaji wake,” ameesema Maridai.
Mbunge wa Ushetu Emmanuel Cherehani amesema gharama zitakazotumika katika ujenzi huo ambao ni tiba kwa wananchi katika utatuzi wa changamoto zinazotokana na kujaa kwa daraja hilo,
“Ujenzi huu utagharimu zaidi ya Sh5 bilioni ambazo zimetolewa na Serikali ambayo ni suluhisho kwa wananchi wa Kata ya Ulowa na kata jirani na wananchi wanaotumia barabara hii,” amesema Cherehani.
Mkazi wa Kijiji cha Ulowa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, January Andrew amesema daraja hilo linapoojaa linawakwamisha kuendelea na shughuli za kiuchumi.

Naye Gabriela Kimaro ambaye ni mkazi wa kijiji hicho amesema wakati wa mvua ng’ombe wanaenda na maji hata watu pia walishawai kwenda na maji,
Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Ernest Mkumbo amesema kutokana na changamoto ya kujaa maji kwa daraja hilo, kuna kipindi aliwahi kulala kando ya daraja hilo akisubiri wavushaji kuelekea Tabora.
“Wavushaji walikuwa wametengeneza ngalawa kwa kutumia magome tulikuwa tunaenda Tabora tulifika saa tisa usiku hapa kivukoni hatukukuta wavushaji tulala hapa,” amesema Mkumbo.
Mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa daraja hilo ambaye ni mwakilishi wa kampuni ya ujenzi Jonta Edger Malya ametaja hatua za ujenzi wa daraja hilo,
“Wakati ambao mvua sio nyingi kama sasa tunanyanyua nguzo kuanzia chini ambazo zitatusaidia kuendelea kazi hata wakati wa mvua” amesema Malya.