Tanga. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kuhakikisha upatikanaji endelevu wa mafuta kwa gharama halisi, kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya sheria, na kushughulikia malalamiko ya wateja kwa haraka ili kuboresha huduma kwa Watanzania.
Dk Biteko ametoa maagizo hayo leo Jumatatu, Februari 17, 2025, jijini Tanga, wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Nne cha Baraza la Pili la Ewura.
Amesema ameridhishwa na utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa katika kikao cha Baraza kilichofanyika Novemba 2024.
Katika kikao hicho cha awali, aliagiza Ewura kuongeza kasi ya kushughulikia malalamiko ya wateja, kuondoa urasimu katika utoaji wa vibali vya ujenzi wa vituo vya kujazia gesi kwenye magari (CNG), kupunguza gharama za ujenzi wa vituo hivyo, kulegeza masharti ya ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini na kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Tangu Novemba 2024 hadi Januari 2025, Ewura imetoa vibali vya ujenzi wa vituo vinane vya CNG, huku wawekezaji 50 wakionesha nia ya kujenga vituo vingine.
Aidha, mamlaka hiyo imeshusha gharama za leseni na vibali vya ujenzi wa vituo vya CNG, gharama za maombi ya vibali zimeshuka kutoka Sh500,000 hadi Sh50,000, na gharama za maombi ya leseni kutoka Sh1,000,000 hadi Sh100,000.

Katika hatua nyingine, Dk Biteko ametoa maagizo mengine kwa uongozi wa Ewura, yakiwamo kuhakikisha malipo na stahiki za kifedha za watumishi zinasimamiwa ipasavyo, kuboresha mazingira ya kazi kwa kuwapatia vifaa na vitendea kazi vya kisasa vinavyoendana na mahitaji ya taasisi na watumishi wake.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuwaendeleza watumishi kitaaluma kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu, mfupi na wa kati katika fani mbalimbali ili kuwawezesha kuendana na mabadiliko ya teknolojia na maendeleo ya sekta ya nishati duniani.
Katika jitihada za kuimarisha mahusiano kati ya uongozi na watumishi, imependekezwa kuanzisha mijadala ya wazi kuhusu maendeleo na mipango ya baadaye ya taasisi.
Amesisitiza umuhimu wa kutambua na kuthamini kazi nzuri za watumishi kupitia vyeti, barua za pongezi, tuzo za ufanisi na ubunifu, pamoja na kutambua mafanikio katika kufikia malengo ya taasisi.
“Hatua hizi zinawafanya watumishi wahisi kuthaminiwa na hivyo kuongeza bidii katika utendaji wao,” amesema.
Aidha, amesisitiza suala la motisha kwa wafanyakazi na kuhimiza kuanzishwa kwa utamaduni wa mazoezi na ushiriki wa michezo ndani ya taasisi na kwa kushirikiana na taasisi nyingine.
Katika kikao hicho ambacho kinajadili bajeti ya mwaka 2025/26 pamoja na utekelezaji wa bajeti ya 2024/25, Dk Biteko amewahimiza wajumbe kuangazia utekelezaji wa malengo ya taasisi kwa kuzingatia ajenda ya Taifa, hususan matumizi ya nishati safi ya kupikia na upatikanaji wa maji kwa gharama nafuu kwa wananchi wote.
“Naamini mtafanya tathmini ya bajeti iliyopita ili kuona nini kifanyike kuboresha huduma kwa Watanzania,” amesema Dk Biteko.
Katika hatua nyingine, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameipatia nchi heshima kubwa kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ndani na nje ya nchi, huku akitafuta fedha za kufadhili miradi hiyo.
“Ewura mnapaswa kubeba ajenda hii ya nishati safi kwa kutoa elimu kwa umma kuhusu manufaa yake. Sambamba na hilo, tunataka kuongeza bomba la kusafirisha mafuta na kujenga matenki ya kushusha mafuta katika maeneo mbalimbali kama Morogoro na Makambako ili kupunguza msongamano wa magari yanayokuja kujaza mafuta Dar es Salaam,” ameongeza.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Buriani ameipongeza Ewura kwa usimamizi mzuri wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), akisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wazawa na maslahi ya nchi katika mradi huo.
Ameeleza kuwa usimamizi mzuri wa Ewura umewezesha Mkoa wa Tanga kuwa na upatikanaji wa nishati ya mafuta ya kutosha. Kuhusu umeme vijijini, amesema vijiji vyote 763 vya mkoa huo vina umeme, huku juhudi zikiendelea kupeleka umeme kwenye vitongoji 4,596.
Akizungumzia nishati safi ya kupikia, amesema Tanga inaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo na taasisi zinazohudumia zaidi ya watu 100, zipatazo 1,493, zipo katika mchakato wa kuhama kutoka kuni kwenda gesi.
“Jeshi la Magereza limeonesha mafanikio kwa Magereza yake kuanza kutumia nishati safi. Hadi sasa, Tanga imepokea mitungi ya gesi 21,000, ambayo inatolewa kwa wananchi kwa bei ya ruzuku, ikiwa na punguzo la asilimia 50,” amesema Dk Buriani.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Andilile amesema taasisi hiyo imetekeleza maagizo yaliyotolewa na Dk Biteko katika kikao cha Novemba 2024, yakiwamo kushughulikia malalamiko ya wateja kwa haraka kupitia Mkataba wa Huduma kwa Wateja wa Ewura.
Kuhusu uwekezaji wa vituo vya CNG, amesema kuwa utekelezaji umeendelea na kati ya Novemba 2024 na Januari 2025, vibali vya ujenzi wa vituo nane vimetolewa, huku wawekezaji 50 wakionesha nia ya kuwekeza.