ECLAT NA UPENDO WAPELEKA NEEMA YA ELIMU NGORIKA.

Na John Walter -Simanjiro.

Shirika la ECLAT DEVELOPMENT FOUNDATION kwa kushirikiana na Upendo Association limekabidhi rasmi Shule Mpya ya Msingi Kariati iliyopo Kijiji cha Ngorika, Kata ya Ngorika, Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara kwa serikali baada ya kukamilisha ujenzi wake.

Gharama za ujenzi wa shule hiyo ni shilingi milioni 121.1.

Shule hiyo mpya inajumuisha madarasa mawili, matundu 16 ya vyoo, pamoja na miundombinu ya kuvuna maji ya mvua ili kusaidia upatikanaji wa maji kwa wanafunzi na walimu.

Lengo la ujenzi wa shule hii ni kusaidia watoto wa eneo hilo kupata elimu kwa urahisi na kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta shule.

Akizungumza wakati wa makabidhiano, Mkurugenzi wa ECLAT DEVELOPMENT FOUNDATION, Peter Toima, amesema kuwa shirika lake linajenga shule katika maeneo yenye uhitaji mkubwa kwa lengo la kusapoti jitihada za wananchi na serikali katika kuboresha elimu nchini.

“Elimu ndiyo kila kitu kwa jamii, na ndiyo maana tunajitahidi kujenga shule ili wazazi wawapeleke watoto wao shule na wapate elimu bora,” alisema Toima.

Mkuu wa shule hiyo Stanley Bert ameishukuru ECLAT DEVELOPMENT FOUNDATION na Upendo Association kwa msaada wao mkubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu.

Aidha, kaimu Afisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Simanjiro, Mwalimu Gabriel Mapunda, amepongeza juhudi hizo, akisema kuwa kazi iliyofanywa na mashirika hayo ni kazi ya kinabii na inapaswa kuungwa mkono na kila mmoja anayependa maendeleo.

Mapunda ameahidi kuwa serikali itahakikisha inalinda miundombinu ya shule hiyo kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Meneja Miradi wa ECLAT DEVELOPMENT FOUNDATION, Bakir Angalia, alibainisha kuwa shirika hilo limeshajenga zaidi ya shule 50, ambapo kila shule ina madarasa manane pamoja na madawati 23 kwa kila darasa, jambo linalolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wa Tanzania.

Mwenyekiti wa shirika la Upendo Association la nchini Ujerumani, Dr. Fred Heimbach, ameeleza kuwa ataendelea kushirikiana na ECLAT DEVELOPMENT FOUNDATION katika ujenzi wa shule mpya ili kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bila kikwazo chochote.

Wananchi wa Kijiji cha Ngorika wameonesha furaha yao kwa msaada huo, huku wakimpongeza na kumshukuru Mkurugenzi wa ECLAT DEVELOPMENT FOUNDATION kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya jamii.

Shirika la ECLAT DEVELOPMENT FOUNDATION na Upendo Foundation limeendelea kuwa mshirika wa maendeleo katika sekta ya elimu, likiboresha mazingira ya kusomea na kuongeza fursa kwa watoto kupata elimu bora.





 

Related Posts