Fanya haya kukabili ongezeko la joto

Dar es Salaam. Wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ikisema vipindi vya ongezeko la joto vinatarajiwa kuendelea kujitokeza Februari mwaka huu, wataalamu wa afya wameshauri mambo ya kuzingatia katika unywaji, uvaaji, mtindo wa maisha, na ulaji, wakisisitiza kuepuka ulaji wa vyakula vyenye mafuta.

Madaktari wameshauri wananchi wanaoishi katika ukanda wa Pwani na maeneo yanayokumbwa na joto kwa hivi sasa kuzingatia mtindo wa maisha unaofaa, ili kupunguza kero ya joto inayowakabili na kuepuka athari zake.

Februari 12, 2025, TMA ilitoa taarifa kuhusu hali ya joto katika maeneo mbalimbali nchini, ikieleza kutarajiwa ongezeko hususan katika maeneo ambayo msimu wa mvua za vuli umeisha na yale yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Miongoni mwa mambo waliyoyagusia ni pamoja na unywaji wa maji ya kutosha, ulaji wa matunda yenye majimaji, mboga kwa wingi, wanga, na mafuta kwa kiasi kidogo.

Wakizungumza na Mwananchi leo, Jumatatu, Februari 17, 2025, madaktari hao wamesisitiza watu kuepuka vyakula vinavyotengenezwa kwa kutumia mafuta kwa wingi, ili kudhibiti joto la mwili.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Pedro Pallangyo, amesema ni vyema mtu akala vyakula vyepesi na kuepuka vile vinavyoupa mwili joto na vizito, hasa nyakati za usiku.

“Tunashauri vyakula vyepesi ili kuepuka kuchoka ghafla. Ni vyema chakula kikawa laini, chenye majimaji au mchuzi wa kutosha. Matunda yanayoshauriwa zaidi ni tikiti, tango, machungwa na mengine yenye majimaji ya kutosha,” amesema.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ngozi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Andrew Foi, amesema ili kutunza ngozi katika msimu huu, mtu anashauriwa kuvaa nguo nyepesi na kupendelea nguo nyeupe, akisisitiza kuepuka nguo nyeusi.

“Vaa nguo nyepesi na nyeupe na epuka nguo za kufunika sana mwili. Wale wanene wahakikishe miili yao inakuwa safi ili kuepuka mazalia ya bakteria, kwao ni rahisi kupata maambukizi. Muhimu kuvaa kofia mviringo ili kulinda ngozi ya uso, na kwa wenye uwezo, wapake mafuta ya kulinda ngozi dhidi ya miale ya jua (sunscreen),” amesema.

Ametoa onyo kwa wazazi kutoruhusu watoto kucheza juani na kuepuka kutumia mafuta mazito.

“Tusiwaache watoto wacheze juani, tusiwapake mafuta mazito hasa mgando yanayoleta joto, bali tutafute mafuta ya nazi au lotion. Pia, tuangalie nguo wanazovaa watoto wachanga, tusiwafunike sana; tuwaache wapate hewa ya kutosha,” amesema.

“Makazi yetu, nyumba zetu, tumezijenga kwa msongamano usio rasmi, hivyo mzunguko wa hewa huwa mdogo. Waweza kufungua madirisha ili kuruhusu hewa kupita,” ameongeza.

Dk Foi amesema ongezeko hili la joto linakwenda sambamba na madhara ya moja kwa moja kwa mwili wa binadamu.

Ametaja mambo ambayo ikiwa hayatazingatiwa, ni rahisi mtu kupata athari, ikiwa ni pamoja na wale wanaokwenda katika fukwe za bahari.

“Jana ilikuwa ni joto kubwa. Wengi hawajui wale nini, wavae nini, wakae wapi. Nashauri wale wanaokwenda sehemu za fukwe za bahari, hiki si kipindi kizuri sana. Ule mwanga wa jua ukiingia kwenye maji, ukitoka unakuwa mkubwa zaidi, hivyo ni rahisi kupata magonjwa ya ngozi,” amesema.

Daktari huyo maarufu wa tiba ya ngozi nchini amesema kwa kawaida binadamu jotoridi lake huwa 36.9°C, lakini linapozidi hutambulika kuwa na homa.

“Joto linapokuwepo mpaka TMA inatoa taarifa, ni kitu kinachoweza kuleta madhara, ambayo hata hivyo hayapo kwenye ngozi peke yake.

“Kawaida, mwili wa binadamu una jotoridi la 36.9°C, endapo joto la nje likizidi hili lililopo ndani ya mwili, kuna uwezekano mkubwa wa watu kupata madhara,” amesema.

Dk Foi amesema madhara hayo hutegemea umri na maumbile, ambapo mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano anatarajiwa kuathirika zaidi na joto, kwa kuwa tezi zake zinazohusika na jasho hazijakomaa vya kutosha, hivyo atapata vipele vingi kwenye ngozi.

Dk Foi amesema madhara hayo hutegemea umri na maumbile, ambapo mtoto chini ya umri wa miaka mitano anatarajiwa kuathirika zaidi na joto, kwa kuwa tezi zake zinazohusika na jasho hazijakomaa vya kutosha, hivyo atapata vipele vingi kwenye ngozi.

Related Posts