Bukavu. Gavana wa jiji la pili kwa ukubwa katika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) la Bukavu, Jimbo la Kivu Kusini, Jean-Jacques Purusi, amethibitisha uwepo wa waasi wa M23 ndani ya jiji hilo baada ya kusonga mbele kwa kasi.
Waasi wa M23, wanaodaiwa kuungwa mkono na serikali ya Rwanda, walithibitisha kuitwaa Bukavu, jiji la pili kwa ukubwa mashariki mwa DRC, Jumamosi, Februari 15, 2025.
“Wao (M23) wako Bukavu,” Purusi aliiambia shirika la habari la Reuters Jumapili, akiongeza kuwa askari wa Jeshi la Ulinzi la DRC (FARDC) walijiondoa katikati mwa jiji hilo ili kuepuka mapigano na kuleta madhara kwa raia eneo la mjini.
Kundi hilo lenye silaha lilikuwa likisonga kuelekea mjini tangu liliponyakua Jiji la Goma, jiji kubwa zaidi katika eneo hilo lililoko Jimbo la Kivu Kaskazini mwishoni mwa Januari, kisha kujitanua na kuutwaa Mji wa Nyabibwe uliopo Kivu Kusini kabla ya kuingia Bukavu.

Kuanguka kwa Bukavu kunawakilisha upanuzi mkubwa zaidi wa eneo lililo chini ya udhibiti wa M23 tangu uasi wa hivi karibuni ulipoanza mwaka 2022.
Serikali ya DRC imethibitisha kuwa waasi wameingia Bukavu, ikiongeza kuwa wanajeshi wa Rwanda walikuwepo pamoja nao. Hata hivyo, Serikali haikusema kuwa jiji lote liko chini ya udhibiti wa M23.
“Rwanda inaendelea kwa ukaidi kutekeleza mpango wake wa kukalia, kupora na kutenda uhalifu na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika ardhi yetu,” ilisema Serikali katika taarifa yake.
Mapema Jumapili, ofisa mmoja wa eneo hilo, chanzo cha usalama na mashuhuda watano waliripoti kuwaona waasi ndani ya jiji, huku msemaji wa kundi hilo la waasi akiiambia Reuters: “Tuko hapo.”
Msemaji wa M23, Willy Ngoma, alisema kupitia kipande cha video kilichorekodiwa kwa simu kuwa kundi hilo tayari liko mjini.
Kwa upande wake, kamanda mwandamizi wa waasi hao wa M23, alionekana akizungumza na wakazi kote Bukavu, kulingana na ripoti ya Alain Uaykani wa Al Jazeera.
“Kamanda mwandamizi wa (waasi)… alikuwa na shughuli nyingi mjini, akijaribu kuzungumza na watu, akiwaahidi kuwa sasa wao ndio wanaosimamia hali, kwamba jeshi la DRC limekimbia,” alisema Uaykani, akiripoti kutoka Goma.
Mbali na Uaykani, kiongozi mwingine wa kikosi cha M23 kilichoingia katika Mji wa Bukavu, Bernard Byamungu, alionekana akizungumza na wananchi hao, huku akiwahakikishia kuwa amani itarejea eneo hilo na kuwataka waendelee na shughuli zao za uzalishaji.
Mkazi wa Bukavu, Arsene Cishungi, alisema mbali na kujawa hofu wakati wa uvamizi wa waasi hao, anaamini kwa maneno ya viongozi wa kundi hilo huenda hali ikarejea kuwa shwari.
Jiji lilikuwa katika hali ya machafuko siku moja kabla, kukiwa na uporaji mwingi na wakazi wengi waliokuwa wakihaha na kukimbia, lakini hali ya utulivu inaonekana kurejea sasa, aliongeza.
Taarifa nyingine inadai kuwa umati wa wakazi wa Bukavu walivamia na kupora ghala la Shirika la Chakula Duniani (WFP), kisha kutokomea na magunia ya vyakula na bidhaa.
Mkazi wa Bukavu, Claude Bisimwa, aliiambia Associated Press kuwa alibeba miili ya wanaume wawili waliouawa kwa risasi “ndani ya nyumba yao”.
“Walikuwa katika chumba chao. Tunapeleka miili yao mochwari. Hizi si risasi zilizopotea, askari alifanya hivi kwa makusudi,” alisema Bisimwa.
Licha ya hofu ya awali miongoni mwa baadhi ya watu, mashirika ya habari ya Associated Press na Agence France-Presse yaliripoti kuwa wakazi wengi waliwashangilia waasi wa M23 walipokuwa wakitembea na kuendesha magari katikati ya jiji.
Baadhi yao waliimba: “Ninyi ndio tuliowasubiri. Tunahitaji mabadiliko katika nchi hii. Tunataka kazi.”
Siku moja kabla, waasi walidhibiti Uwanja wa Ndege wa Kavumu, ambao unahudumia Bukavu. Inaripotiwa kuwa walikabiliana na upinzani mdogo waliposonga mbele.
Kwa mujibu wa waasi hao, Uwanja wa Ndege wa Bukavu ndiyo ulikuwa kizuizi kikubwa cha mwisho cha kijeshi kwa waasi kabla ya kufika Bukavu, jiji lenye zaidi ya watu takriban milioni moja.
Kusonga mbele kwa waasi hao kumetokea wakati mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) ukiendelea nchini Ethiopia.

Mzozo wa DRC umekuwa mada kuu ya mjadala katika mkutano huo wa siku mbili, ambapo viongozi waliazimia kutafuta mwarobaini wa suala hilo, huku baadhi wakipendekeza Serikali ya Rais Félix Tshisekedi kukaa meza moja na waasi hao, ili kufikia mwafaka na kuepuka kuibuka kwa janga la kibinadamu nchini humo.
Akihutubia mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), António Guterres, alisema mzozo huo wa kikanda lazima uzuiliwe kwa gharama yoyote huku akitaka uadilifu wa eneo la DRC uhifadhiwe.
“Kuingia kwa M23 na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) mjini Bukavu ni ukiukaji wa uhuru wa DRC na uadilifu wa eneo lake, pamoja na uvunjaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa,” alisema Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza katika taarifa yake aliyoichapisha kwenye mtandao wa X (zamani Twitter).
“Uingereza inatoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano, kuondolewa kwa wanajeshi wote wa RDF kutoka ardhi ya Kongo, na kurejea katika mazungumzo kupitia michakato ya amani inayoongozwa na Afrika. Hakuna suluhisho la kijeshi,” aliongeza msemaji huyo.
Umoja wa Afrika umekosolewa kwa mtazamo wake wa tahadhari, na wachambuzi wanataka hatua madhubuti zaidi juu ya mzozo huu.
Rwanda inakanusha kutoa msaada wa kijeshi kwa M23, lakini inadai kuwa makundi ya Wahutu wenye msimamo mkali nchini DRC yanatishia usalama wake.
Ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa ilisema mwaka jana kuwa Kigali ilikuwa na takriban wanajeshi 4,000 ndani ya DRC na ilikuwa na udhibiti wa moja kwa moja wa kundi hilo la waasi.
Waasi wa M23 ndio kundi lenye nguvu zaidi kati ya zaidi ya makundi 100 yenye silaha yanayopigania udhibiti wa mashariki mwa DRC yenye utajiri wa madini.
Mapigano hayo yamesababisha zaidi ya watu 3,000 kuuawa, huku zaidi ya watu milioni sita wakiyahama makazi yao, na kusababisha janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani.
Takriban watu 350,000 wameachwa bila makazi tangu waasi walipoingia Goma.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika.