Hatimaye Hersi afunguka ndoa ya Aziz Ki, Mobetto

Rais wa Yanga, Hersi Said amevunja ukimya kuhusu ndoa ya nyota wa timu hiyo, Stephane Aziz Ki na Hamisa Mobetto.

Ndoa hiyo ilifungwa jana Februari 16, 2025 katika Msikiti wa Masjid Nnuur uliopo Mbweni jijini Dar es Salaam ikifuatiwa na hafla ya kibao kata iliyofanyika nyumbani kwa bibi harusi, Bahari beach.

Siku moja kabla ya ndoa, Mobetto alilipiwa mahari ya ng’ombe na pesa taslimu Sh30 milioni, mahari iliyokabidhiwa na Hersi Said kwa niaba ya baba mzazi na wajomba wa Aziz Ki.

Ndoa ya Aziz Ki raia wa Burkina Faso na Mobetto imekuwa na viulizo, maswali na kuwa gumzo katika maeneo mbalimbali.

Miongoni mwa viulizo ni kuhusu ndugu wa Aziz Ki na sababu ya Hersi kusimama kwa niaba ya baba na wajomba wa bwana harusi wakati wa utoaji mahari.

Pia hivi karibuni aliibuka mtu ambaye aliandika kwenye mtandao wa Instagram akihoji ni vipi Hersi amemuoza Aziz Ki bila yeye kupewa nafasi ya kutayarisha harusi hiyo aliyodai ni ya mwanae.

Akizungumza na Mwananchi leo Februari 17, 2025, Hersi amesema mambo yanayozungumzwa kuhusu harusi hiyo na yeye kulaumiwa na mtu aliyejitambulisha kama mama wa Aziz Ki si ya  kuyazingatia.

“Hii ni harusi ya watu na imekwishapita, ni vema wakaizungumza wenyewe wahusika,” amesema Hersi akisisitiza kutotaka kuzungumzia zaidi kuhusu familia ya Aziz Ki na yeye kumwakilisha katika utoaji wa mahari.

Mbali na ishu ya familia, baadhi ya watu wamekuwa wakionyesha wasiwasi na sintofahamu juu ya kiwango cha kiungo huyo mshambuliaji uwanjani baada ya ndoa na wengine kushindwa kutofautisha maisha binafsi na kazi ya mchezaji huyo.

Akizungumzia hilo, Hersi amesema kiweledi hakuna uhusiano kati ya ndoa na kiwango cha mchezaji kushuka akisisitiza si kwa Aziz Ki tu, bali wachezaji wote akitolea mifano ya mastaa wa soka duniani waliofanya vizuri uwanjani wakiwa wameoa mastaa.

“Ronaldo (Cristiano) hadi leo anacheza tena yupo kwenye kiwango kikubwa akiwa na umri mkubwa, ni mwanasoka mwenye mke na watoto, vivyo hivyo Messi (Lionel).

“Kina David Beckham wameanza kuoa mastaa miaka hiyo (alimuoa mwanamitindo na mwanamuziki Victoria Beckham) na bado alikuwa akiitumikia vema timu yake na kazi yake ya soka,” amesema.

Hersi amesema baadhi ya watu wanashindwa kutofautisha maisha ya mchezaji wa kulipwa na majukumu mengine ya kifamilia.

“Weledi ni kitu kingine na majukumu yako ya kifamilia ni kitu kingine, ndivyo ilivyo kwa kila mtu,” amesema Hersi na kuongeza.

“Hakuna uhusiano kati ya kuoa staa na kiwango cha mtu au kuoa tu na kiwango isipokuwa watu wanachanganya na kufikiri mtu akioa shabaha yake inabadilika kutoka kwenye mpira na kuingia kwenye familia, lakini kila mmoja anastahili kuwa mume au kuwa mke.

Aziz Ki kutimkia Uarabuni

Hivi karibuni kulikuwa na tetesi za kiungo huyo mshambuliaji huyo kutakiwa na moja ya timu za soka Uarabuni.

Akizungumzia hilo, Hersi amesema ofa hizo zipo si kwa Aziz Ki bali kila mchezaji anaweza kuwa anahitajika sehemu nyingine.

“Hizi tetesi zipo na ndio maana kuna dirisha kubwa la usajili na dirisha dogo, Aziz Ki kuondoka Yanga ni suala la majadiliano kwa kuwa mpira ni biashara,” amesema.

Amesema Aziz Ki aliongeza mkataba wa miaka miwili Yanga, hivyo kama kuna timu inamhitaji watakaa mezani, lakini kwa sasa bado yupo Yanga.

Related Posts