KESI ZA ACT WAZALENDO: Mahakama yatupa pingamizi la Serikali kumkataa shahidi

Kigoma. Mahakama ya Wilaya ya Kigoma imeitupilia mbali pingamizi la Serikali dhidi ya shahidi wa tano katika shauri la uchaguzi lililofunguliwa na mwanachama wa ACT- Wazalendo, Lovi Lovi.

Lovi ambaye katika chaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2024 alikuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Mtaa wa Gezaulole, Kata ya Gungu, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, amefungua shauri hilo kupinga matokeo nua mwenendo wa uchaguzi huo.

Wajibu maombi (wadaiwa) katika shauri hilo ni  mgombea wa nafasi hiyo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyetangazwa kuwa mshindi, Hassan Mashoto.

Majibu maombi wengine katika shauri hilo ni msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa Mtaa wa Gezaulole (ambaye ni mtendaji wa Kata ya Gungu na Msimamizi wa Uchaguzi, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji (ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa hiyo.

Katika shauri hilo linalosikilizwa na Hakimu Katoki Mwakitalu, Lovi anaiomba Mahakama itamke uchaguzi huo ni batili kwa madai haukuwa huru na wa haki kutokana na ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi.

Katika mwendelezo wa usikilizwaji wa shauri hilo, mawakili wa Serikali wameibua pingamizi dhidi ya shahidi wa tano wa upande wa mwombaji, wakiiomba Mahakama asiruhusiwe kutoa ushahidi.

Pingamizi hilo limeibuliwa na Wakili wa Serikali, Mkama Musalama akidai wakati shahidi wa nne akiendelea kutoa ushahidi, shahidi huyo alikuwa amekaa karibu akiisikiliza na kwamba pia mwombaji katika shauri hilo, Lovi alikuwa alitoka nje mara kwa mara na kwenda kuongea na shahidi huyo wa tano, kilichokuwa kinaendelea.

Pingamizi na hoja za wakili Musalama limepingwa na wakili wa mwombaji, Emmanuel Msasa, akisema wakili huyo wa Serikali amesema uongo mahakamani.

Wakili Msasa amedai mahali alipokuwa amekaa wakili Musalama hawezi kuona alilokuwa shahidi alilokuwa amekaa shahidi.

Kuhusu hoja kwamba mwombaji alikuwa akienda kuongea naye amedai si kweli maana wakili huyo hakusema hicho mwombaji alichomweleza shahidi hiyo ili Mahakama ipime kama kinahusiana na ushahidi huu na ione kuwa hastahili.

Pia, wakili Msasa amedai wakili huyo wa Serikali hajataja hata kifungu cha sheria ya ushahidi kinachokataza hilo na akaiomba mahakama Ione kuwa pingamizi hilo halina mashiko.

Wakili Musalama katika kujibu hoja za wakili Msasa, alidai  wako mawakili wanne wanaowawakilisha wajibu maombi wa pili na wa tatu na kwamba mahali alilokuwa amekaa shahidi huyo alionwa na wakili mwenzako, Steven Kimaro.

Amedai wakati shauri linaendelea wakili Kimaro alinyanyuka mara tatu na kwamba ndiye aliyemuoma, hoja ambayo imepingwa na wakili Msasa kuwa ilikuwa hoja mpya kwani hakuwa amesema awali.

Hakimu Mwakitalu baada ya kusikiza pande zote katika uamuzi wake, amekubaliana na hoja za wakili Msasa (wa mwombaji) akisema kuwa pingamizi hilo halina mashiko.

Hakimu Mwakitalu amesema hakuna ubishi kuwa mahali alilokuwa amekaa wakili Musalama hawezi kuona mtu aliyekuwa amekaa kwenye benchi nje ya chumba lililokuwa litasikilizwa shauri hilo.

“Hoja kwamba si yeye aliyemuona mwombaji akizungumza na shahidi bali ni mmoja wa mawakili wenzake hakuziweka kwenye hoja za msingi. Na kama ni wakili mwingine ndio aliyewaona ni kwa nini hakuweka pingamizi yeye mwenyewe? Hivyo pingamizi hili linatupiliwa mbali,” amesema Hakimu Mwakitalu.

Baada ya uamuzi huo shahisi huyo ameendelea na ushahidi wake akiongozwa na wakili Msasa amesema katika uchaguzi huo, Hamis Ally (36) ameendelea na ushahidi wake mpaka mwisho.

Katika hatua nyingine Mahakama hiyo imepanga kesho Jumanne Februari 18, 2025 kutoa uamuzi wa mapingamizi ya Serikali katika mashauri ya uchaguzi yaliyofunguliwa na chama hicho, uliotarajiwa kutolewa leo kuhusiana na mawakili wa Serikali kumkataa hakimu anayesikiliza mashauri hayo mawili, Ana Kahungu.

Mashauri haya ni kati ya mashauri 51 yaliyofunguliwa na ACT- Wazalendo kote nchini katika Mahakama za wilaya mbalimbali kupinga matokeo na mwenendo wa uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Novemba 27, 2024.

Katika mashauri hayo chama hicho kinalalamikia kugubikwa na kasoro nyingi za ukiukwaji wa sheria na taratibu za uchaguzi zilizoufanya kutokuwa huru na wa haki.

Mashauri hayo yamefunguliwa katika wilaya za mikoa mbalimbali zikiwamo Temeke, Lindi, Ilala, Momba, Mkuranga, Mafia, Kigoma na Kibiti.

Katika Mkoa wa Kigoma chama hicho kilifungua jumla ya mashauri 13, huku Manispaa ya Kigoma Ujiji kikiwa kimefungua mashauri tisa.

Awali, Serikali iliibua mapingamizi ya awali dhidi ya kesi karibu zote zinazoendelea kusikilizwa Kigoma, wakiiomba Mahakama iyatupilie mbali bila kuwasikiliza walalamikaji msingi wa hoja za malalamiko yao, kutokana na sababu tofautitofauti za kiufundi.

Hata hivyo, ni mashauri matatu tu yaliyoondolewa kwa mapingamizi hayo lakini mengine waliyapangua na sasa yako katika hatua kati ya usikilizwaji wa hoja za msingi wa malalamiko ya waombaji.

Kwa mujibu wa wakili Msasa hayo mashauri matatu yaliyotupiliwa mbali, wameridhika na uamuzi wa Mahakama katika mashauri mawili, wanayafanyia marekebisho ya kasoro zilizokubaliwa na Mahakama na wanayafungua tena.

Katika shauri la tatu wakili Msasa amesema uamuzi wa shauri moja hawajakubaliana nao, wako katika hatua za kuukatia rufaa baada ya kupata mwenendo wa shauri na nakala ya uamuzi huo.

Related Posts