Kifungu hiki hakitawaacha salama makada wa CCM

Kuna methali isemayo asiyesikia la Mkuu huvunjika guu na hiki ndicho kinaenda kuwakuta makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), walioanza mapema kampeni na harakati za kuwania ubunge na udiwani, licha ya chama kuonya juu ya hilo.

Ama kwa kutokujua, kupuuza au kujiaminisha liwalo na liwe, hawakuwa wanasoma vifungu vya kanuni za uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya Dola, toleo la 2021 ambazo ndio sasa zinakwenda kuwa kichinjio kwao.

Kulingana na tovuti ya Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), Tanzania ina jumla ya Kata 3,956 na majimbo 264, ambayo maelfu wa makada wa CCM wataomba kuteuliwa, pamoja na wale watakaoomba kuteuliwa viti maalum.

Pamoja na kuonywa na viongozi wa juu wa CCM, baadhi ya wanachama waliamua kuweka pamba masikioni, wakaendelea kutoa misaada ya kijamii kwenye misiba, maafa, harambee na shughuli za kijamii na kujitaja wao ndio viongozi wajao.

Kwa takribani miaka miwili mfululizo sasa, huko majimboni na kwenye kata kumekuwa hakukaliki kutokana na pilikapilika za makada wa CCM wanaofanya vikao vya siri na baadhi ya viongozi wenye dhamana ya kufanya uteuzi.

Si hivyo tu, makada hao, baadhi yao wakiwa na ukwasi mkubwa wa kifedha, wametengeneza mitandao ya ushindi kuanzia uchaguzi wa ndani wa CCM mwaka 2022, ambapo walishiriki kupanga safu za uongozi kwa maslahi yao ya 2025.

Ni kutokana na kupanga safu huko, ndio maana leo wapo makada wanajipitisha majimboni na kwenye kata lakini hawakemewi wala kuchukuliwa hatua, na baadhi ya viongozi nao wana wagombea wao mifukoni ambao wanawaunga mkono.

Ushahidi wa makada kujipitisha pitisha majimboni na kuwafanya wabunge wakose usingizi na kuwafanya wawe mguu mmoja bungeni na mwingine jimboni, kulifichuliwa pia na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika mkutano mkuu maalum wa CCM uliofanyika mjini Dodoma Januari 19, 2025, Rais Samia alisema tayari wamepata malalamiko na ushahidi wa picha za watu wanaoitisha mikutano ya jimbo, lakini nyuma ya pazia ni ili kujitambulisha.

Nikimnukuu mwenyekiti huyo wa CCM alisema “Tuna ushahidi wa picha nyingi tu sana. Tunaomba kutoa onyo mapema,” lakini onyo kama hilo liliwahi kutolewa Septemba 5, 2023 na aliyekuwa makamu mwenyekiti, Abdulrahman Kinana.

Akiwa wilayani Hai, Kinana alionya kuwa chama hicho hakitasita kuwaengua wagombea walioanza kampeni mapema majimbo mbalimbali nchini, onyo ambalo limesikika likitolewa pia na viongozi wengini wakiwamo wenyeviti wa mikoa.

Nimetangulia kusema kanuni za uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya Dola toleo la 2021, zinasema wazi kuwa ni marufuku kwa mwanachama anayetarajia kugombea au wakala wake, kufanya kampeni za mapema.

Kifungu cha 25(5) kinasema “Ni marufuku kwa mwanachama yeyote anayetarajia kugombea au wakala wake, kufanya vitendo ambavyo ni dhahiri kuwa sehemu ya kampeni za kuiwania nafasi anayoitafuta kabla ya uongozi uliopo haujamalizika”

Ibara ndogo ya (6) inasema ni marufuku kwa mwanachama anayetarajia kugombea au wakala wake, kutoa misaada mbalimbali wakati wa uchaguzi unapokaribia (kama huu wa 2025) ambayo ni dhahiri ina lengo la kuvutia kura.

Lakini kanuni hiyo hamgusi Rais, mbunge, mwakilishi au Diwani ambaye yupo madarakani wakati huo kwa kuwa yeye atakuwa bado anao wajibu wa kuhudumia eneo lake la uongozi, iwe ni nchi nzima, jimbo au kata anayohudumu.

Sasa ukisoma ibara ndogo ya 7(a) na (b) inasema kiongozi wa atakayechaguliwa katika kura za maoni lakini ikathibitika alivunja miiko hiyo, atavuliwa uongozi na pia kama ni mwanachama, hatateuliwa kugombea nafasi yoyote aliyoiomba.

Pamoja na Kanuni hizo nzuri hivyo, bado wapo makada ni kama nyumbu vile, anataka kuvuka mto na anaona umejaa mamba bado anavuka na mwisho anakuwa chakula cha mamba, na ndicho tutakachoenda kukishuhudia.

Wala makada hao wasije kutafuta mchawi, kwa sababu ni wao wenyewe wameamua kujichimbia kaburi, kwa sababu ni wazi kampeni ndani ya chama huanza baada ya kuvunjwa kwa Bunge na chama kupuliza kipenga.

Ninaamini kamati za usalama na maadili ndani ya CCM zimefanya kazi yake sawa sawa na ndio maana Rais na mwenyekiti wa CCM akasema tayari wana ushahidi wa picha nyingi tu, za makada walioanza kampeni mapema majimboni.

Inaweza ikaonekana tatizo kubwa liko kwenye majimbo, lakini nataka kuiambia CCM, hata kwenye kata nako kuna shughuli hivyo ni imani yangu ule usemi kuwa “sheria ni msumeno, hukata mbele na nyuma”, basi uondoke na hivyo vichwa.

Ni lazima hao walioanza kampeni mapema watambue kuwa wao hawako juu ya taasisi (CCM), na wala sio kila mmoja ana sharubu kama Kambale, wanaonywa lakini wapo, wanavunja Kanuni za 2021 wazi wazi kwenye majimbo na kata.

CCM ionyeshe mfano, pale kwenye ushahidi wa kada kutoa rushwa ya fedha, khanga, vitenge, sukari na hongo nyingine zinazofanana na hizo kwa viongozi na wajumbe kuanzia ngazi ya chini, basi njia pekee ni kumla ‘kichwa’ kuleta nidhamu.

Related Posts