Musoma. Watu wawili wamefariki dunia, huku wengine 140 wakiugua ugonjwa wa kipindupindu katika Wilaya za Musoma na Rorya, mkoani Mara.
Ugonjwa huo umeibuka katika wilaya hizo tangu Januari 23, 2025, huku chanzo kikuu kikitajwa kuwa ni matumizi hafifu ya vyoo safi na salama katika maeneo yaliyoathiriwa na ugonjwa huo.
Hayo yamesemwa leo, Jumatatu, Februari 17, 2025, na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini, Dk Joseph Fwoma, wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi, aliyefika katika Kijiji cha Bwai kwa ajili ya kujionea hali halisi.
Dk Fwoma amesema hadi sasa wagonjwa tisa wamelazwa wakiendelea na matibabu.

Amesema tangu kuibuka kwa ugonjwa huo katika halmashauri yake, jumla ya watu 63 wameugua ambapo mtu mmoja alifariki dunia.
“Tangu kuibuka kwa ugonjwa huu, mtu mmoja ndiye aliyeripotiwa kufariki dunia baada ya kuchelewa kufikishwa kituo cha kutolea huduma za afya,” amesema.
Amesema mgonjwa huyo alipata ugonjwa akiwa visiwani: “Sasa mchakato wa kumfikisha hapa, ukizingatia na umri wake, akawa amefariki dunia.”
Amesema kufuatia kuibuka kwa ugonjwa huo, halmashauri hiyo imetenga zahanati ya Kijiji cha Bwai kama kambi ya wagonjwa hao, ambapo amesema wagonjwa wengi wanatoka katika visiwa vilivyopo ndani ya halmashauri hiyo ambavyo vinatumiwa na wavuvi kwa ajili ya shughuli za uvuvi.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, amesema hali ya matumizi ya vyoo safi na salama katika halmashauri hiyo, hususan ukanda wa Ziwa Victoria, ni hafifu na kwamba kutokana na udharura uliopo, tayari wamepiga kambi kwa ajili ya kuhamasisha matumizi ya vyoo katika maeneo yao.
“Kwa hapa sina takwimu, lakini kwa ujumla ukanda huu wa ziwa zipo baadhi ya kaya hazina vyoo. Tayari tumeanza oparesheni ya kuhakikisha kila kaya inakuwa na vyoo na vinatumika kama inavyotakiwa,” amesema Chikoka.
Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi, amewaagiza wakuu wa wilaya hizo kupiga kambi katika maeneo yaliyoathiriwa na ugonjwa huo ili kuhakikisha hauendelei kuenea na kusababisha madhara zaidi.
“Ni aibu karne hii wilaya kukumbwa na ugonjwa kama huu ambao tunajua unasababishwa na nini. Wakuu wa wilaya, nawaagiza tokeni ofisini, nendeni kwa wananchi, fanyeni operesheni, elimisheni wananchi wanatakiwa kufanya nini ili kuepuka maambukizi zaidi,” amesema.
Mtambi amesema amebaini uwepo wa ufuatiliaji hafifu kwa wakuu hao wa wilaya baada ya kutolewa kwa maagizo, jambo ambalo kwa namna moja ama nyingine linasababisha wananchi kutokufuata maagizo wanayopewa.
Amesema wananchi wanapaswa kuongozwa kufuata maelekezo wanayopewa na wataalamu wa afya kwa maelezo kuwa ugonjwa huo unaweza kuepukika endapo wananchi watafuata maelekezo hayo.
“Hili jambo halipendezi. Ni bahati mbaya kwamba, pamoja na kujua njia za kukabiliana na ugonjwa huu, lakini watu bado ni wazito kubadilisha mfumo wa maisha, na hii inasababishwa na kutokufanyika kwa ufuatiliaji wa maagizo yanayotolewa,” amesema.
Amesema uwepo wa ugonjwa huo katika wilaya hizo, pamoja na mambo mengine, kunasababisha kusimama kwa shughuli za maendeleo katika maeneo husika.
Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dk Halfan Haule, amesema jumla ya watu 77 wameugua ugonjwa huo wilayani humo katika kipindi hicho, huku mmoja akifariki.
“Hadi sasa tuna wagonjwa wawili kwenye kituo. Tunaendelea kupambana kuhakikisha tunatokomeza ugonjwa huu,” amesema.