Kocha wa maafande acharuka | Mwanaspoti

KOCHA wa maafande wa Polisi Tanzania, Mussa Rashid amewaonya mastaa wa timu hiyo kuacha tabia ya kudharau wapinzani wao, kwa sababu kwa kufanya hivyo inawaweka katika mazingira magumu ya kukipambania kikosi hicho kumaliza nafasi nne za juu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mussa alisema hata mchezo waliochapwa mabao 3-1, dhidi ya Kiluvya United ulitokana na nyota wa kikosi hicho kuwadharau wapinzani wao, huku akiwataka kuacha kucheza kwa mazoea kwa sababu hawapo sehemu salama sana.

“Kiwango tulichokionyesha tulistahili kupoteza kutokana na kushindwa kuongeza umakini, hii sio sifa ya timu zinazotaka kuwania nafasi nne za juu, ushindani ni mkubwa sana na tunatakiwa kubadilika kwa haraka ili kuendana na kasi iliyopo.”

Kocha huyo wa zamani wa African Sports na Green Warriors, amejiunga na kikosi hicho akitokea Biashara United ya Musoma na ameungana kikosini na Bernard Fabian aliyeanza nacho msimu huu, ingawa kwa sasa ameteuliwa msaidizi wake.

Timu hiyo imecheza michezo 18, kabla ya ule wa jana dhidi ya Transit Camp na imeshinda mitano tu, sare mitano na kupoteza minane, ikiwa nafasi ya 10 na pointi 20, huku ikipambana kurejea Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2022-2023.

Related Posts