NYOTA wa kimataifa wa Tanzania, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ amesema mapigano yanayoendelea Goma, DRC Congo yamesitisha mazungumzo na kati yake na klabu ya Tanganyika FC.
Kwa takriban mwezi sasa katika Mji wa Goma kumekuwapo na mapigano baada ya wanajeshi wa kundi la waasi la M23 kuvamia na kuuteka mji huo na hivyo kuathiri shughuli mbalimbali za kijamii na michezo.
Beki huyo wa zamani wa Yanga aliyekipiga pia FC Lupopo nusu msimu uliopita kabla ya kuvunja nao mkataba alitokea Lubumbashi Sports alikocheza msimu mmoja kati ya miwili akiondoka kutokana na changamoto ya mshahara, kwa sasa yuko nchini.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ninja alisema kwa sasa hakuna mazungumzo yaliyoendelea na Tanganyika kutokana na changamoto ya mapigano iliyokuwa inaendelea nchini humo.
“Tangu tulivyozungumza awali sijawarudia tena, nasikilizia kwanza mapigano kama mchezaji huwezi kusaini tu, amani pia ni jambo muhimu sana ili uweze kupata utulivu wa akili na mwili,” alisema Ninja.