Matumizi ya drone kuongeza uzalishaji wa pamba Maswa

Maswa. Matumizi ya teknolojia ya kisasa ya ndege zisizo na rubani (drone) katika kunyunyizia dawa kwenye zao la pamba yanatarajiwa kuongeza uzalishaji kutoka tani 13 katika msimu wa mwaka 2023/2024 hadi tani 50 katika msimu wa mwaka 2024/2025.

Hayo yameelezwa leo, Februari 17, 2025, na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge, katika Kijiji cha Hinduki wakati akikabidhi kwa wakulima pampu za mkono na drone za kunyunyizia dawa ya zao hilo, zilizotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Pamba Tanzania (TCB).

Amesema kuwa teknolojia hiyo ikitumiwa vizuri itasaidia kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa msimu huu katika wilaya hiyo, ambayo ni maarufu kwa kilimo hicho.

“Tunataka uzalishaji wa pamba kwa ekari moja ufikie kilo 1,200 ili kuleta tija kwa mkulima, kwani kwa sasa wakulima wengi wanapata kilo 250 hadi 300 kwa ekari.

“Pia tunataka tutoke huko, na ndiyo maana Serikali imekuja na teknolojia ya kisasa ya kutumia ndege hizi zisizo na rubani katika kunyunyizia dawa kwenye zao la pamba likiwa shambani,” amesema.

Amesema kuwa wakulima wa pamba katika wilaya hiyo wameonyesha kufurahishwa na matumizi ya teknolojia hiyo, kwani imeondoa adha ya kutumia muda mrefu kufanya kazi hiyo.

Jilala Hinda, mkulima wa Kijiji cha Bugarama wilayani humo, amesema kuwa amelima ekari 10 ya zao hilo chini ya usimamizi wa wataalamu wa kilimo na kufuata kanuni bora za ulimaji wa pamba kwa kuepuka kuchanganya na mazao mengine ili kuwa na mafanikio makubwa.

Amesema kuwa kipindi hiki cha kunyunyizia dawa katika shamba lake amekuwa akitumia pampu kwa kuibeba mgongoni, ambapo huchukua siku tatu kukamilisha ekari moja.

“Hii pampu ya kubeba mgongoni kwa kupulizia shamba, ekari moja inatumia siku tatu na wakati mwingine ni mzigo mzito lazima uchoke, lakini kwa kutumia ndege hii isiyo na rubani, inatumia dakika sita tu kwa ekari moja,” amesema.

Naye Emmanuel Makani, mkulima wa Kijiji cha Ishima wilayani humo, amesema kunyunyizia dawa ya kuua wadudu kwenye pamba kwa kutumia pampu ya mkono ni changamoto kubwa kwani wanatumia nguvu nyingi, hivyo uwepo wa drone umerahisisha kazi.

“Matumizi ya drone yametusaidia sana sisi wakulima wenye mashamba makubwa kuanzia ekari 10 na kuendelea. Sasa umefika wakati kwa Serikali kutupia macho bei ya zao hili la pamba kwani kila msimu wa uuzaji ukianza, malalamiko ni makubwa juu ya bei,” amesema.

Msimamizi wa zao la pamba kutoka Bodi ya Pamba Wilaya ya Maswa, Ally Mabrouk, amesema tayari wameshapatiwa drone saba zitakazoanza kufanya kazi kwa wakulima sambamba na kugawa bure zaidi ya pampu 8,000 za mkono kwa wakulima wa zao hilo.

“Hizi drone saba tulizonazo tumezisambaza katika maeneo mbalimbali ya wilaya yetu ili ziweze kuwahudumia hasa wakulima wenye mashamba makubwa kuanzia ekari 10 na kuendelea. Zinatolewa bure, na kinachotakiwa ni mkulima kuleta sumu na maji ya kuchanganyia tu,” amesema.

Related Posts