PAMBA Jiji gari limewaka baada ya kushinda mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu Bara ikiwa ni rekodi kwa timu hiyo iliyorejea katika ligi hiyo baada ya miaka 23 tangu iliposhuka mwaka 2001, lakini licha ya matokeo hayo, kocha wa timu hiyo, Fred Felix ‘Mizniro’ ameshtukia jambo na kuanza kujipanga upya.
Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu ya Muungano 1990, ilianza na ushindi ugenini dhidi ya Dodoma Jiji kwa kuichapa 1-0, kabla ya kuizima Azam pia bao 1-0 CCM Kirumba na juzi ilirejea kwa kuinyoosha Coastal Union kwa mabao 2-0 kwenye uwanja huo huo.
Matokeo hayo yameiondoa timu hiyo eneo la mkiani hadi nafasi ya nane na pointi 21, lakini kocha Minziro aliliambia Mwanaspoti, mfululizo wa mechi zinazopishana kwa muda mfupi unaleta uchovu huku akihofia kukosa maandalizi ya kutosha kwa mechi zijazo, japo hawana cha kufanya.
Minziro alitoa kauli hiyo juzi mara baada ya mchezo walioizima Coastal kwa mabao yaliyowekwa kimiani na nyota wawili wa kigeni, Ben Nakibinge na Abdoulaye Camara ukiwa ni mchezo wa raundi ya 19 na sasa timu hiyo inaifuata Mashujaa mjini Kigoma keshokutwa Jumatano.
Mizniro alisema “Fatiki (uchovu) imekuwa kubwa, lakini hakuna namna lazima tupambane, kwa sasa tunaenda Kigoma kucheza na Mashujaa Februari 19, kumbuka leo (juzi) ni Februari 15, hivyo tunafanya maandalizi ya siku mbili na nyingine kama hizo tutakuwa safarini na kunahitaji kutafuta alama tatu nyingine.”
Beki huyo wa kushoto wa zamani wa Polisi Zanzibar na Yanga, aliongeza; “Tunawapongeza mashabiki na Wanamwanza kwa jumla wanaojitokeza kwa wingi, kwani wanatupa hamasa kubwa na wachezaji wanajitoa uwanjani pengine wanakuwa wamechoka, lakini unamuona anaendelea kupambana kutokana na jinsi gani wanavyotupa hamasa.”
Akizungumzia mchezo wa juzi, Minziro alisema licha ya kushinda bado kikosi kilikuwa na upungufu hasa eneo la ushambuliaji na kujilinda, huku akiwapongeza wachezaji kwa sababu mechi ilikuwa ngumu kwani walikuwa chini na walihitaji ushindi ili kwenda juu kitu walichofanikiwa pamoja na dosarui zote.
“Haikuwa kazi rahisi kupata matokeo haya na sasa tuko ndani ya 10 Bora, kiukweli tumejaribu kutengeneza timu kupitia dirisha dogo, tumepata nafasi zilizotusaidia kiasi kikubwa kila nafasi ina wachezaji wawili hadi watatu,” alisema Minziro.