YANGA imesitisha sherehe za harusi kwa muda ikamsomba hadi bwana harusi, Stephane Aziz KI baada ya kurudi uwanjani na kisha kuizimaisha Singida Black Stars kwa mabao 2-1 jioni hii, shukrani ikienda kwa Clement Mzize na Prince Dube waliotupia kila mmoja bao moja kwenye Uwanja wa KMC Complex.
Yanga ilipata ushindi huo katika mchezo ulioshuhudia Aziz Ki aliyetoka kumuoa Hamisa Mabetto jana, kushuka uwanjani na kusaiidia kutengenezwa kwa bao la pili lililowekwa wavuni na Dube kwa kichwa akimalizia kona safi ya Maxi Nzengeli, kona hiyo ilitokana na krosi ndefu ya ‘Bwana Harusi’ iliyomfikia Maxi na kutolewa na mabeki wa Singida.
Hilo lilikuwa bao la tisa kwa Dube msimu huu na kwa Mzize aliyefunga bao la kwanza dakika ya 14 likiwa ni la 10 na wawili hao kufukuzana katika orodha ya wafungaji mabao wa ligi hiyo.
Katika mchezo huo uliosubiriwa kwa hamu, kutokana na sababu mbili kwanza aina ya kikosi cha Singida ilichonacho ambacho licha ya kuongezewa watu wa maana dirisha dogo kilitoka kuwatoa jasho Yanga kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza na Mabingwa hao watetezi wakishinda kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0.
Sababu ya pili ilikuwa wengi waliona kama Yanga imekuwa na mambo mengi nje ya uwanja juu ya harusi ya staa wao Stephanie Aziz KI aliyehitimisha wiki iliyopita kwa kufunga ndoa na mwanamitindo na msanii Hamisa Mobeto ilionekana kama watetezi hao wamedharau mchezo hivi kumbe wanajitambua.
Na iliposhuka uwanjani ilitumia dakika 45 za kwanza kumaliza kila kitu kwa kufunga mabao hayo kabla ya wageni kuchomoa bao moja likiwekwa kimiani na Jonathan Sowah, likiwa ni la tatu katika mechi nne alizoichezea timu hiyo aliyojiunga nayo katika dirisha dogo la usaljili lililofungwa katikati ya Januari.
Yanga iliandika bao la kwanza kupitia Mzize dakika ya 13 kwa shuti kali akiwazidi hesabu mabeki wa Singida waliokuwa wanapambana kuokoa na kupiga shuti kali lililojaa wavunii kabla ya Dube kuongeza la pili dakika chache kabla ya mapumziko kwa kichwa akimalizia mpira wa kona ya Maxi.
Mjadala mkubwa leo ni kikosi kilichoanzishwa Singida BS, ambapo mastaa waliozoeleka walianzishwa benchi na wengine kutokuwa katika orodha kabisa, lakini kocha David Ouma alisema ni uamuzi wa kubadilisha kutokana na timu kucheza mechi ngumu mfululizo na pia tofauti ya viwanja na kushukuru kupoteza kwa idadi hiyo kwani kama angeamua kuwatumia waliozoeleka huenda wangekutana na maafa kwa aina ya soka ililocheza Yanga jioni hii.
Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko na wageni walinufaika baada ya Jonathan Sowah aliyeingia kipindi cha pili hicho kufunga bao la kufutai machozi lililotokana na makosa ya kipa wa Yanga Djigui Diara aliyetangulia kucheza mpira kabla ya kumkuta mfungaji.
Bao hilo linamfanya Sowah kufikisha bao la tatu akiendelea kuonyesha kiwango Bora tangu asajiliwe dirisha dogo na Singida Black Stars.
Matokeo hayo yamezidi kuifanya Yanga ijikite kileleni ikifikisha pointi 52 kutokana na michezo 20 huku ikifunga mabao 50 na kufungwa tisa hadi sasa ikiwa mbele ya watani zao, Simba wenye mchezo mmoja miwili mkononi na kumiliki pointi 47. Simba itashuka uwanjani Jumatano ya Februari 19 kuvaana na Namungo, mkoani Lindi, siku ambayo ni sherehe ya kupongezwa kwa maharusi, Aziz Ki na Hamisa.