Profesa Mosha apigilia msumari kufutwa daraja sifuri

Katika toleo la tarehe 10 Februari, 2025, gazeti la Mwananchi lilikuwa na makala iliyokuwa na kichwa cha habari: “Daraja la sifuri lifutwe.” Pendekezo hilo lilitolewa na Shirika la Uwezo Tanzania takriban wiki mbili, baada ya kutangazwa kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2024, likisema uwepo wake unawaathiri kisaikolojia vijana.

Mimi nakubaliana asilimia 100 na Shirika la Uwezo Tanzania. Tarehe 7/12/2021 niliandika makala katika gazeti hili iliyokuwa na kichwa cha habari: “Tuachane na Mfumo wa kutoa sifuri katika matokeo ya Mitihani.”

Nilitegemea kwamba huenda wadau wa elimu na hasa wahusika wa kuratibu elimu yetu, wangesikiliza maoni yangu wakati huo, au basi wangejitokeza na kutoa maoni yao au waboreshe maoni yangu. Haijawa hivyo.

Sasa shirika la Uwezo Tanzania limeeleza vizuri kwa nini tuachane na huu mfumo potofu wa kuwapa wanafunzi wetu alama ya sifuri. Mawazo yangu yapo pale pale: huu ni mfumo potofu, ni mfumo onevu, ni mfumo wa udhalilishaji: tuachane nao.

Sababu za kupinga daraja sifuri

Naomba nirudie leo katika makala haya sababu zangu za kupinga mfumo huu kwa kurudia maoni niliyoyatoa gazetini humu tarehe 7/12/2021.

 Tuanze na hadithi ya kweli. Mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi aliyeitwa Tunu alikuwa anapata shida shuleni katika masomo yote. Walimu walijitahidi kumsaidia katika somo la lugha lakini hakulipenda somo hilo.

 Ilikuwa hali kadhalika katika masomo ya hisabati, sayansi, historia, jiografia, na masomo mengine. Hakupenda masomo hayo na hivyo hakuwa tayari kujishughulisha nayo.

 Kwa utaratibu wa shule hiyo, Tunu alikuwa anapata sifuri katika masomo yote.

Mwishowe mwalimu wa darasa aliwaita wazazi wa Tunu na kuwaambia kwamba shule imeshindwa kumsaidia hivyo wazazi wamchukue binti yao na kutafuta njia mbadala ya kumsaidia.

Hawa wazazi wenye uchungu walimchukua binti yao na kumpeleka kwa mtaalamu wa elimu ya akili, yaani mwanasaikolojia, ili amsaidie Tunu.

Huyu mtaalamu aliwasikiliza kwa makini hawa wazazi waliokuwa karibu kukata tamaa kuhusu maendeleo ya binti yao wakijiuliza: hatima ya mtoto wetu itakuwaje?

Baada ya maelezo ya wazazi, mwana saikolojia aliwaomba wazazi watoke hapo ofisini pamoja naye, na wamwache binti yao hapo ofisini peke yake.

Waliingia katika ofisi ya jirani ambayo ilikuwa na kioo kilichotenganisha hizo ofisi mbili. Ni kile kioo ambacho ukiwa upande mmoja utaona kinachoendelea upande mwingine, lakini ukiwa upande mwingine hutaona upande wa pili.

Wazazi na mwanasaikolojia walikuwa pamoja wakimwona huyo binti lakini binti hakuwaona wao.

Huyu mtaalamu alikuwa amefungulia redio ndogo iliyopiga miziki ya aina mbalimbali. Wote watatu walishangaa jinsi huyo binti alivyofurahia huo muziki, alivyochezesha mwili wake na jinsi alivyochangamkia huo muziki. Huyo mtaalamu akawageukia wazazi na kuwaambia: binti yenu ni mwana muziki!

Wazazi hawa wenye furaha walimchukua binti yao na kumpeleka shule ya muziki. Muda si mrefu alianza kutunga nyimbo zake, na ulimwengu ukaanza kumsikia. Amealikwa nchi mbalimbali duniani na kwa sasa yeye ni bilionia mkubwa.

 Hii ni hadithi ya kweli. Jina Tunu si jina lale halisi. Nimelitumia ili kulinda heshima ya huyo binti ambaye sasa ni mama mzima.

 Walimu wake wa zamani walimwalika shuleni wakamwomba radhi kwa kumpa sifuri walizokuwa wakimpa mara kwa mara katika masomo yake. Aliwasemehe, na naamini Mungu aliwasamehe pia.

Zipo hadithi nyingi za namna hii popote duniani. Wapo wanafunzi niliosoma nao ambao walipewa sifuri shuleni, sasa ni wanabiashara wakubwa wanatuajiri sisi tuliodhani tuliwapita kiakili.

Wapo walioshindwa mtihani shule ya msingi au sekondari, lakini baadaye wakafanya vizuri sana katika shule nyingine na mazingira tofauti.

 Yupo mwingine niliyesoma naye darasa moja sekondari, akarudishwa nyumbani kwa kupata sifuri mara kwa mara, kisha akapata sekondari nyingine na leo ni injinia aliye na sifa ya kimataifa. Anajenga na kubomoa injini za ndege!

Hapa tena nina hadithi nyingine ya ukweli. Nilialikwa na chuo fulani nikafundishe kwa miezi kadhaa huko Finland, Ulaya Kaskazini, na somo langu lilikuwa Maadili katika Biashara (Business Ethics).

Kabla sijaingia darasani nilipewa mwongozo juu ya kutahini wanafunzi na mfumo wao wa kutoa matokeo ya mitihani.

Nikaelezwa kwamba mwanafunzi aliyefanya vizuri sana hupewa alama 5, ambayo ni sawa na asilimia 100%. Alama zinazofuata ni 4.5; 4; 3.5; 3; 2.5; 2; 1.5 na ya mwisho ni 1. Hakuna chini ya alama moja.

Hiyo alama moja maana yake ni ufaulu wa chini. Hawatoi sifuri. Maelezo yao ni kwamba hata kama mwanafunzi hakuandika chochote katika karatasi la mtihani, yapo mambo anayoyajua. Ana uwezo fulani wa akili ambao mtihani huu hauwezi kuupima.

 Niliridhika na maelezo hayo hasa nilipoona jinsi nchi hiyo ilivyo na maendeleo makubwa katika uchumi na huduma za kijamii. Kwao hakuna mwanafunzi anayefeli.

Wanafunzi waliopata ufaulu wa chini, yaani alama 1, wanasomeshwa masomo ya ufundi iwe ni katika sekondari au katika chuo.

Hivyo ni vema mfumo wetu wa elimu utambue kwamba hapo zamani kidogo wataalamu wa saikolojia wa elimu walikuwa wanapima mtu ana uwezo wa akili kiasi gani (IQ, Intelligence Quotient).

Sasa wataalamu wengi wa saikolojia wanapima mtu ana akili ya aina gani. Wameachana na dhana potofu ya kupima mtu ana kiasi gani cha akili na kuzingatia ukweli kwamba mtu apimwe ana uwezo wa aina gani, yaani ana vipaji vipi. Mitihani yetu yote ya sasa inapima mwanafunzi ana akili kiasi gani, si ya aina gani. Sababu hii peke yake ingetusukuma tuachane na kuwapa wanafunzi sifuri.

 Kama kweli wizara yetu inayosimamia elimu ina nia thabiti ya kuboresha elimu, basi izingatie mada tunayoizungumzia hapa.

Tutoe elimu inayowajengea wanafunzi tabia ya kujiamini. Tuondoe sifuri katika matokeo ya mitihani ya wanafunzi wetu.

 Tuwape ujumbe usio na shaka kwamba wana uwezo na vipaji vingi, vipaji ambavyo mfumo wa elimu hauwezi kuvipima.

Tuwe na uthubutu wa kufanya mapinduzi katika mfumo wetu wa elimu. George B. Shaw amesema: ‘’ Mtu asiyeweza kubadilisha mtazamo wake, hawezi kubadilisha chochote duniani.’’

Related Posts