Raia wa Malawi adaiwa kukutwa na vipande 18 vya meno ya tembo

Songwe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linamshikilia Chisamba Kameme (60), raia wa Malawi kwa tuhuma za kukutwa na vipande 18 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 84.2.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Februari 17, 2025, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Augustino Senga amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa jana Jumapili saa 4:30 usiku katika Kitongoji cha Msia, Kata ya Chitete wilayani Ileje.

Kamanda Senga amesema kupitia taarifa za kiintelejensia pamoja na misako na doria kwa kushirikiana na idara za wanyamapori Wilaya ya Ileje,  zimesaidia kumkamata mtuhumiwa huyo.

Amesema baada ya kufanya tathimini na wataalamu, imebainika meno hayo yana thamani ya Sh155.3 milioni ikiwa ni sawa na tembo watatu na kila tembo akiwa na thamani ya Sh51.7 milioni.

“Wakati mtuhumiwa anakamatwa alikuwa ameweka meno hayo ya tembo kwenye mfuko wa salfeti kisha kufunga kwenye baiskeli ya rangi nyeusi kwa lengo la kuviuza,” amesema Kamanda Senga.

Amesema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

“Niwasihi wananchi wa Songwe kuacha kufanya uhalifu wa kijangili kwa wanyama pori ambao ni kinyume na sheria,” amesema Kamanda Senga.

Related Posts