BILA shaka umewahi kushuhudia mechi za Ligi Kuu zinazopigwa usiku Uwanja wa Jamhuri, Dodoma zikisimamishwa kwa taa kuzimwa ikielezwa ni kupisha ndege zinazopaa na kushuka Uwanja wa Ndege wa Dodoma, basi Bodi ya Ligi (TPLB) imekata mzizi wa fitina kwa kuzifuta mechi hizo.
Bodi ya ligi imeamua kuzifuta mechi zote za usiku zilizokuwa zikipigwa siku za Jumapili na Ijumaa kwenye Uwanja wa Jamhuri, kutokana na kuingiliana na ratiba za ndege zinazotua na kupaa kwenye Uwanja wa Dodoma ambao haupo mbali na Jamhuri, ili kuepukana na kero za mechi kusimamishwa.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almas Kasongo ndiye aliyeyasema hayo akifafanua kuanzia sasa mechi zote zilizopangwa kupigwa Jamhuri muda wa usiku kwa siku za Ijumaa na Jumapili zinafutwa kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao.
Amefunguka hayo siku chache baada ya changamoto ya kuzimwa kwa taa kwenye mechi zinazochezwa siku hizo hivi karibuni changamoto ikiwa ni kupisha ndege iweze kutua.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kasongo alisema wamefanya vikao na mamlaka ya viwanja vya ndege na Chuo cha Anga na kukubaliana kuondoa mechi za usiku ili kuepusha hatari kwa rubani wanaopata shida kushusha ndege kutokana na mataa ya uwanjani.
“Tumekubaliana na ombi hilo kutokana na suala hilo kuwa ni la ulinzi na usalama, baada ya kupokea barua tumelifanyia kazi kwa kufanya uamuzi wa kusitisha mechi kwa siku hizo baada ya vikao na Serikali, viongozi wa viwanja vya ndege,” alisema Kasongo na kuongeza;
“Ijumaa na Jumapili kunapochezwa mechi usiku taa zinavyowaka zinamsababishia shida rubani wakati wa kushusha ndege, basi taa ziwe zinazimwa ili kumpa unafuu rubani, hivyo kila jambo lina utaalamu wake nasi tumelipokea na kulifanyia kazi kwa kusitisha michezo ya usiku ili ichezwe mchana au jioni.
“FIFA jambo lolote lenye ulinzi na usalama linatakiwa kupewa kipaumbele na sisi hatuna budi kilibeba hilo. Tumelipokea kwa sababu lina kipaumbele. Hata hivyo, kuna shida kidogo, wachezaji wameshapata joto ndege inakuja taa zinazimwa mechi inasimama tutakuwa hatumtendei haki mchezaji.”
Alisema mbali na wachezaji, pia warushaji wa matangazo, mashabiki na hata wao bodi.
Akizungumzia changamoto iliyotokea Kaitaba katika mchezo wa wenyeji Kagera Sugar waliokubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Tabora United alisema ni suala la kukatika kwa umeme na kusababisha hitilafu kwenye jenereta tatizo hilo hadi sasa bado halijatatuliwa.
“Pia kuna changamoto ya mwanga kuwa hafifu na tayari tumeliwasilisha kwa injinia anaendelea kulifanyia kazi na wakati linashughulikiwa mechi zake zitakuwa zinachezwa mchana hadi hapo tatizo hilo litakapo tatuliwa,” alisema Kasongo.
Kutokana na hitilafu hiyo ya umeme, ndio iliyosababisha pambano lililofuata baina ya Kagera Sugar dhidi ya Fountain Gate lilihamishwa kutoka saa 1:00 usiku na kupigwa saa 10:00 jioni na wenyeji kushinda mabao 3-0, mabao yaliyofungwa na Peter Lwasa aliyefunga mawili na Saleh Seif Kambenga.