Bukoba. Ripoti ya kitabibu kutoka Hospitali ya Gereza la Isanga iliyopo mkoani Dodoma imeonesha mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Padri Elipidius Rwegoshora ana akili timamu.
Mbali na Padri Rwegoshoro wa Kanisa Katoliki, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya mauaji ya kukusudia dhidi ya mtoto, Asimwe Novath ni baba mzazi wa mtoto (Asimwe).
Novath Venant, Nurdini Amada Masudi, Ramadhani Selestine,Rweyangira Burukadi Alphonce,Dastan Bruchard,Faswiu Athuman, Gozbert Alikad, Desdery Everist.
Ripoti hiyo, imesomwa leo Jumatatu Februari 17, 2025 na Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, wakati kesi hiyo ya mauaji namba 25513/2024, ilipoitwa kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali (PH).

Jaji wa Mahakama hiyo, Gabriel Malata aliyesoma ripoti hiyo, amesema amepokea ripoti yenye kumbukumbu namba/11927/2024 Desemba 16, 2024 iliyosainiwa na Dk Enock Changarawe kuwa mtuhumiwa huyo hana tatizo la afya ya akili wala dalili zake.
Amesema Oktoba 25, 2024 Padri Rwegoshora alipelekwa hospitalini hapo kupimwa afya ya akili.
“Nianze kwa kuwakumbusha Oktoba 25, 2024 Mahakama ilipokea na kuridhia ombi la Wakili Mathias Rweyemamu anayemtetea mshatakiwa namba moja, Padri Elipidius Rwegoshora kupelekwa Hospitali ya Sanga iliyopo Dodoma kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya ya akili kabla ya kuendelea na kesi inayomkabili na wenzake wanane.
“Hata hivyo, leo hii kabla ya kuendelea na kesi, nipende kuwaeleza kuwa tumepokea ripoti ya majibu ya vipimo kutoka kwa matabibu walioongozwa na Dk Enock Changarawe na mawakili pande zote tumewapatia nakala inayoeleza kuwa, baada ya vipimo imebainika kuwa mshatakiwa huyo namba moja hana tatizo hilo la afya ya akili wala dalili yoyote,” amesema Jaji Malata.
Jaji Malata baada ya kusoma ripoti hiyo, Wakili Mkuu wa Serikali Ajua Awino ameiomba ripoti hiyo ije itumike kama kielelezo katika kesi hiyo na kisha kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo.
Hata hivyo, Mahakama hiyo imekubali ombia upande wa mashtaka juu ya ripoti hiyo.

Mashidi 52 na vielelezo 37 kutolewa
Wakili Awimo amesema upande wa mashtaka unatarajia kuwa na mashahidi 52 na vielelezo 37.
Hata hivyo, upande wa utetezi ulipinga ripoti hiyo kutumika kama kielelezo cha upande wa mashtaka.
Kutokana na mvutano wa mawakili upande wa mashtaka na wa utetezi kuhusu ripoti hiyo itumike au isitumike kama kielelezo cha ushahidi, Jaji Malata amesema nyaraka hizo zimepokewa kwa ajili ya kuthibitisha taarifa ya hali ya mshtakiwa huyo kuwa akili yake ni timamu kama hospitali ilivyoripoti.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi itakapopangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa.