Nairobi. Sera ya Kimataifa ya Kenya na kauli za Rais William Ruto zimetajwa kuwa mzigo mzito uliomharibia mgombea wa nchi hiyo, Raila Odinga, katika jaribio lake la kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Katika uchaguzi huo uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia, Jumamosi Februari 15, Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, Mahmoud Youssouf alimshinda Raila katika mzunguko wa sita, wakati Kenya ikiwa imetumia mamilioni ya shilingi kumfanyia kampeni.
Wachambuzi wa sera za kigeni, sheria na siasa wanaeleza kuwa, kauli na misimamo ya Rais Ruto kuhusu masuala ya Bara la Afrika na kwingineko, hatimaye yalikuwa mzigo uliomharibia Odinga na kuzamisha kabisa matarajio yake ya kushinda.
Hata hivyo, Odinga amesema Rais Ruto alifanya vya kutosha kumuunga mkono katika kampeni zake na kwamba, kushindwa kwake kulitokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao.
Hata hivyo, wataalamu wanahoji Odinga alikosa busara kwa kumtegemea Dk Ruto na kutarajia miujiza, huku sera isiyoeleweka ya kigeni ya Kenya, inayoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi, ikiwa haikumnufaisha hata kidogo.
Mtaalamu wa sera za kigeni, Profesa Peter Kagwanja na wakili wa jijini, David Ochami wanaamini kuwa, Odinga alipoteza nafasi hiyo kwa kiasi kikubwa kutokana na makosa ya kidiplomasia ya Rais Ruto, mtazamo ambao pia unaungwa mkono na Mikhail Nyamweya, ambaye pia ni mtaalamu wa sera za kigeni.
Wameeleza kuwa, matamshi yake kuhusu suala la Sahrawi, mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), simu yake maarufu kwa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron baada ya kuanguka kwa Goma mikononi mwa waasi wa M23, pamoja na mtazamo wake kuhusu Sudan, vita vya Russia-Ukraine na mgogoro wa Israel na Hamas, vilichangia kushindwa kwa Odinga.
“Kwa kiwango kikubwa, Odinga alishindwa kwa sababu alikuwa akifadhiliwa na muuzaji mbaya wa sera za kigeni, yaani Rais Ruto, ambaye matendo yake ya hivi karibuni katika DRC na Sudan yamewachukiza viongozi wengi wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika,” amesema Ochami.
“Hii inamaanisha kuwa, Ruto alikuwa mzigo kwa kampeni ya Odinga na ilikuwa wazi kwamba angeshindwa tangu mwanzo. Alikuwa amenaswa katika hali zisizoweza kuepukika.”
Profesa Kagwanja amesema kushindwa kwa Odinga kunatoa fursa nzuri kwa Kenya kutathmini upya sera yake ya kigeni inayolenga Afrika na Ulaya.
“Kwa mfano, tweet ya Rais Ruto kwamba Israel inapaswa kulindwa dhidi ya magaidi ilionesha wazi alikuwa anaegemea upande mmoja kwenye mgogoro wa Israel na Palestina. Hali hii ilifanya iwe vigumu kwa Kenya kupata kura za mataifa 19 ya Kiislamu barani Afrika,” amesema Profesa Kagwanja.
Amesema, “kauli hiyo isiyo na huruma pia ilipingana na msimamo wa pamoja wa Umoja wa Afrika (AU), unaosaidia suluhisho la mataifa mawili katika mgogoro huo wa muda mrefu na wenye umwagaji mkubwa wa damu.”
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) inayoongozwa na Afrika Kusini ilichukua msimamo tofauti na Kenya kuhusu mgogoro wa Israel na Palestina, huku Afrika Kusini ikiishutumu Israel kwa mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) huko Uholanzi.
“Kwa hali hii, ilitarajiwa kuwa SADC isingeunga mkono mgombea wa Kenya kwa nafasi ya juu ya AUC,” amesema Nyamweya.
Wakati Odinga alihitaji Rais Ruto kumuunga mkono na kufungua hazina ya Serikali kugharamia kampeni yake ya gharama kubwa ya AU, swali la msingi lilikuwa ikiwa mtindo mpya wa diplomasia ya Kenya chini ya utawala wa Ruto ulikuwa mzigo mzito uliomlemea Odinga.
“Matamshi ya Rais Ruto kuhusu Israel na Palestina hayakuwa ya msaada,” amesema Profesa Kagwanja.
Kwa kushangaza, Rais wa Palestina Mahmoud Abbas alikuwa mgeni mashuhuri wa AU katika mkutano huo mjini Addis Ababa wakati wa uchaguzi huo na alipewa fursa ya kuhutubia uongozi wa AU.
Katika siku za hivi karibuni, Serikali ya Rais Ruto imekabiliwa na shinikizo kuhusu nafasi yake katika kuleta utulivu wa mgogoro wa DRC, hasa kufuatia shughuli za waasi na wanasiasa wa upinzani wanaoonekana kufanya harakati zao Nairobi.
Mwaka 2023, kiongozi wa waasi wa M23, Bertrand Bisimiwa na aliyekuwa Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya DRC, Corneille Nangaa, walizindua rasmi Muungano wa Mto Congo (Congo River Alliance) jijini Nairobi , muungano wa kisiasa na kijeshi wenye lengo la kuiangusha Serikali ya Rais Felix Tshisekedi.
Uzinduzi huo, uliotokea siku chache kabla ya uchaguzi katika Taifa hilo lenye machafuko, ulisababisha mgogoro wa kidiplomasia kati ya Kenya na DRC, huku DRC ikimrudisha nyumbani balozi wake aliyeko Nairobi kwa “mashauriano” na kumuita balozi wa Kenya huko Kinshasa.
Kundi la waasi la M23 linaendelea kusababisha machafuko na vifo DRC Mashariki, huku Mji wa Goma ukiangukia mikononi mwao.
Ochami amesema hali ilizidi kuwa mbaya baada ya Rais Ruto kutangaza kuwa alizungumza na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, kuhusu mgogoro wa Congo, akijua kuwa mataifa ya Francophone barani Afrika yanajitenga na Ufaransa kijeshi na kisiasa.
“Unakumbuka kuwa, mwaka 2023, Muungano wa Mto Congo, ambao M23 ni sehemu, ulizinduliwa Nairobi. Huwezi kutarajia DRC na mataifa mengine ya Afrika kuipa Kenya na Ruto zawadi kwa tabia hii,” amesema Ochami, msimamo ambao pia uliungwa mkono na Profesa Kagwanja.
Hivi karibuni, Rais Tshisekedi alikataa juhudi za upatanishi za Dk Ruto kutafuta suluhu kwa mgogoro wa DRC chini ya mwavuli wa EAC, ambayo kwa sasa inaongozwa na Rais Ruto.
Rais Tshisekedi alidai kuwa, Nairobi haikuwa na uaminifu katika juhudi za kutafuta amani mjini Goma, badala yake akageukia SADC kwa msaada wa kijeshi na Angola kwa upatanishi.
“Sera ya kigeni ya Kenya chini ya Ruto imekuwa na upendeleo wa Magharibi, jambo ambalo limeitenganisha na washirika wake wa muda mrefu wa Pan-Afrika kama Afrika Kusini,” amesema Profesa Kagwanja.
Amesema Afrika Kusini, “ilimuona Rais Ruto kama kibaraka wa Magharibi badala ya kiongozi wa kweli wa Pan-Afrika.”
“Hii ndiyo sababu kushindwa kwa Raila ni mwito wa Kenya kutathmini upya sera yake ya kigeni kwa misingi ya maslahi ya kitaifa,” amesema Profesa Kagwanja.