Sababu barafu kupungua Mlima Kilimanjaro – 1

Kilimanjaro. Desemba, 2024, nilipanda Mlima Kilimanjaro, ambao barafu yake inapungua kadri miaka inavyosonga. Sababu kubwa ikitajwa ni mabadiliko ya tabianchi, na baadhi ya watu wanahusisha na matukio ya moto mlimani.

Safari ilianza Marangu ambako nilikatiza msitu wenye miti mingi ya asili (msitu mnene). Kulingana na msimu, kulikuwa na mvua. Kutoka Mandara, niliingia eneo la uwanda wa Savana, ambalo lina nyasi, miti iliyotawanyika na vichaka. Hali ya hewa ikawa tofauti na nilipoanza safari.

Katika eneo la Horombo, hewa ni hafifu zaidi, kukiwa na uoto mdogo wa asili. Horombo iko kwenye urefu wa mita 3,720 juu ya usawa wa bahari, wakati Mandara ni mita 2,720.

Safari ya kutoka Horombo mpaka Kibo hupitia eneo lenye mchanga na mawe likiwa kwenye mwinuko wa mita 4,720 juu ya usawa wa bahari.

Eneo la Kibo, ambalo liko umbali wa kilomita sita tu kutoka kilele cha juu zaidi cha Mlima Kilimanjaro, lina baridi kali, ni kavu na lenye hewa hafifu ya oksijeni pamoja na upepo mkali.

Safari ya kuelekea kileleni hukutana na mwinuko mkali, mawe, miamba na mchanga mwingi. Kwa mujibu wa aliyeniongoza kupanda mlima, kuna wakati udongo au barafu huporomoka.

Kituo cha Gilman’s, kilichopo mita 5,681 kutoka usawa wa bahari, kina baridi kali zaidi, kuna upepo, na theluji hudondoka. Kuna mawe makubwa kuelekea kwenye kilele cha Uhuru.

Kelvin Hande (si jina halisi), mpagazi katika Mlima Kilimanjaro, alipozungumza nami, anasema moto unaowaka mara kwa mara katika Mlima Kilimanjaro unaongeza joto mlimani, hivyo kusababisha athari kwa barafu iliyopo.

“Kumekuwa na matukio ya moto ya mara kwa mara hapa mlimani yanayoongeza joto. Wanaochoma moto wanafanya hivyo kwa masilahi yao, wakijua watalipwa ili kuuzima, lakini wanaharibu mazingira,” anasema Hande.

Akizungumzia kupungua kwa barafu na athari zake kwa utalii, mwongoza wapanda mlima huo, Aron Minja, anasema: “Barafu inapungua sana. Zamani kulikuwa na utalii wa kwenye barafu, lakini sasa umepotea. Tunapata wageni wanaopanda mlima, lakini wakwea barafu hawaji kwa kuwa sehemu imebaki ndogo ambayo nayo haifikiki kwa urahisi.”

Minja, ambaye ameongoza watalii kwa takribani miaka 30, muda mwingi akihudumu katika hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, anasema ni muhimu kuwa na juhudi za pamoja za kulinda asili ya mlima huo ili uendelee kuwa kivutio cha utalii, chanzo cha biashara na uchumi wa maelfu ya Watanzania.

Ofisa uhifadhi wa kitengo cha utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa), Mapinduzi Mdesa, anasema miongoni mwa sababu za kutoweka kwa barafu ni mabadiliko ya tabianchi, ambayo yamesababishwa na kuongezeka kwa joto duniani.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Machi, 2024, ilisema tathmini ya kitaalamu iliyofanywa ilionyesha wastani wa ongezeko la joto kwa mwaka 2023 ulikuwa nyuzi joto moja ya sentigredi, kiwango kilichovunja rekodi na kuandika historia ya kuwa mwaka wenye joto zaidi.

Kwa mujibu wa TMA, ongezeko hilo halikuwa kwa Tanzania pekee, kwani taarifa zinaonyesha wastani wa ongezeko la joto la dunia mwaka 2023 ulifikia nyuzi joto 1.40 za sentigredi na kuufanya kuwa mwaka wenye joto zaidi katika historia.

Hali hiyo inaelezwa ilichangiwa na uwepo wa El Nino (mfumo wa hali ya hewa unaosababishwa na ongezeko la joto la bahari katika eneo la kati la Kitropiki kwenye Bahari ya Pasifiki) na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza na Mwananchi wakati huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a, alisema kiwango hicho cha joto kimepatikana baada ya kukokotoa wastani wa nyuzi joto katika kipindi cha miezi 12 na kuthibitika ongezeko la nyuzi joto 1.0, ambalo halijawahi kurekodiwa nchini.

“Unapozungumzia wastani ni mjumuisho wa muda mrefu. Baada ya kurekodi kiwango cha joto cha mwaka mzima ndipo tulipopata ongezeko la nyuzi joto 1.0, kiwango ambacho hakijawahi kurekodiwa. Ndiyo maana tunasema mwaka 2023 umevunja rekodi,” alisema.

Alisema kwa miaka ya nyuma walikuwa wakirekodi chini ya hapo, akitoa mfano kwamba mwaka 2022 ilikuwa nyuzi joto 0.5. Vingine vilivyorekodiwa kwa miaka mingine ni 0.3, 0.6, na 0.7.

Kwa upande wa viwango vya dunia, alisema wastani wa nyuzi joto 1.2 sentigredi ulirekodiwa mwaka 2022, na mwaka 2021 ulikuwa 1.1.

Kwa mujibu wa Mdesa: “Kuongezeka kwa joto duniani ni moja ya sababu za kupungua kwa barafu. Wakati mwingine kunakuwa na mjadala kwa kuwa hali ya joto juu ya Mlima Kilimanjaro bado ni ya baridi, lakini barafu inazidi kuyeyuka kila mara. Hili ni jambo la kisayansi zaidi.”

Anasema upepo unaovuma Mlima Kilimanjaro unatokea baharini, na barafu inapungua kwa kuwa upepo huo hufika ukiwa mkavu, tofauti na siku za nyuma ulipokuwa ukiambatana na unyevunyevu.

“Ukiangalia, barafu zilizobaki huwa zinakatika pembeni, maana yake ni kuwa upepo mkavu unaziathiri. Kama ungekuja na unyevunyevu, huimarika. Upepo unakuja mkavu kwa kuwa sehemu kubwa ya uoto umepotea, si katika hifadhi ya Mlima Kilimanjaro bali huko unakotokea,” anasema.

Mdesa anasema mamlaka ya hifadhi imefanya jitihada kulinda maeneo ya mlima na uoto wake, lakini sababu kubwa ya kupungua kwa barafu si ikolojia ya Mlima Kilimanjaro, bali hali ilivyo katika maeneo ya pwani kwa kuwa upepo huvuma kutokea baharini.

Mdesa anasema, wakati wa mvua, Mlima Kilimanjaro huwa na theluji nyingi, lakini haikai muda mrefu kwa kuwa upepo huo ukivuma huiyeyusha. Na kwamba, inavyokatika kutokea pembeni, ni ishara kuwa si kwa sababu ya joto la juu pale.

Mdesa anasema miongoni mwa changamoto za uhifadhi wanazokabiliana nazo ni matukio ya moto, hususan katika ukanda wa juu, ambao sehemu kubwa ya uoto wake ni mimea aina ya Erica.

Erica ni mimea ya jamii ya Ericaceae, ambayo huwa vichaka vidogo au wakati mwingine miti midogo. Majani yake ni madogo, membamba, na mara nyingi hujipanga kwa mzunguko kwenye shina.

Huwa na maua madogo yenye umbo la kengele au mirija, yakiwa na rangi ama pinki, nyeupe, zambarau, au nyekundu. Hustawi zaidi katika maeneo ya baridi na milimani, hasa kwenye udongo wenye asidi.

“Baada ya msitu mnene, ukiwa unapanda Mlima Kilimanjaro, uoto unaofuata una kijani kingi, lakini pamoja na uoto huo kuonekana kama wenye maji mengi, ukishika moto unawaka kama petroli,” anasema.

Anasema moto husababishwa na shughuli za kibinadamu, na kutokana na kasi ya upepo mlimani, husambaa kwa kasi kubwa, hivyo ni rahisi kuathiri sehemu kubwa.

“Matukio ya moto ni mengi, pengine uliyowahi kuyasikia ni yale ambayo yalidumu kwa zaidi ya siku tatu, lakini mara kwa mara huwa yanatokea, tunayadhibiti mapema, kisha tunaendelea na shughuli nyingine,” anasema.

Kuhusu madai kuwa wanaochoma moto wana masilahi binafsi, anasema hayana uhalisi kwani matukio hayo huwaathiri.

“Moto kwetu ni janga, na wakati wa janga hakuna mtu anayelipwa ziada zaidi ya kupewa chakula cha kila siku wakati wa kazi. Wakati mwingine moto unakuwa umewaka mbali, tunatembea hadi saa sita porini kuufikia ili kuudhibiti, nani anataka shida hizo?” amehoji.

Anasema moto huathiri bajeti ya mamlaka kwa kiasi kikubwa, kwa kuwa unapotokea huwa kipaumbele, hivyo kuzorotesha miradi ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori Duniani (WWF) nchini Tanzania, mwaka 2020 moto uliteketeza takriban kilomita za mraba 95 za uoto wa Mlima Kilimanjaro.

Mwaka 2022, moto ulizuka karibu na eneo la Karanga na kuathiri takriban kilomita za mraba 33 kwa muda wa wiki mbili.

Mwaka 2023, moto uliibuka katika eneo la Indonet-Rongai, Wilaya ya Rombo, na kuharibu takribani kilomita za mraba 17, sawa na asilimia 0.9 ya Mlima Kilimanjaro.

Umuhimu wa barafu Mlima Kilimanjaro

Balozi wa mazingira wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Dk Aidan Msafiri, anasema suala la barafu katika Mlima Kilimanjaro linahitaji juhudi za pamoja ndani na nje ya nchi kwa kuwa hewa inayosababisha iyeyuke inatoka maeneo tofauti ya dunia.

“Mlima ni mrefu kuliko maeneo yote ya Afrika, ina maana unakutana na hewa kutoka kila pembe ya dunia. Muhimu tuzidi kupanda miti ili kusaidia kufyonza hewa ya ukaa na kupunguza shughuli na matumizi ya bidhaa hatarishi kwa mazingira,” anasema.

Kwa mujibu wa Mdesa, miongoni mwa vivutio vya Mlima Kilimanjaro ni barafu inayodumu muda wote, ikizingatiwa kuwa eneo mlima ulipo ni umbali wa kilomita 300 kutoka ulipo mstari wa Ikweta, ambao kwa kawaida hakuna barafu kwani hupatikana kaskazini na kusini mwa dunia.

“Kwa kuzingatia eneo Mlima Kilimanjaro ulipo na kuwa na barafu muda wote, ni miongoni mwa maajabu katika sayansi ya mazingira, hivyo ni kivutio kikubwa kwa wengi,” anasema, akisisitiza kuwa ni kitu muhimu cha kuendelea kutuzwa na kulindwa.

Anasema vivutio vingine vya Mlima Kilimanjaro ni uwepo wa hali za hewa tano tofauti zinazopatikana kuanzia mstari wa Ikweta hadi kaskazini mwa dunia.

“Ukiwa unapanda Mlima Kilimanjaro, ni kama unatembea kutoka Ikweta hadi eneo juu ya dunia, kwani unakutana na kanda kuu za tabianchi kuanzia Ikweta, tropiki, yabisi, wastani, kibara, na baridi,” anasema.

Sifa ya kanda hizo, anasema, ni kuwa tropiki huwa na unyevunyevu na joto, yabisi kuna mvua kidogo, wastani huwa na joto na unyevunyevu wakati wa kiangazi na kuna wakati wa baridi kali, kibara kunakuwa na joto na baridi kali, na baridi huwa na baridi kali zaidi kuliko kanda zote.

Hali ya asili katika Mlima Kilimanjaro inatajwa kubadilika kadri miaka inavyosonga, sababu kubwa ikitajwa kuwa ni mabadiliko ya tabianchi.

Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro ina eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,688, ambalo ndani yake lina uoto na wanyama ambao ni kivutio cha utalii.

Kwa mujibu wa jarida la Ujirani Mwema la Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) la Januari hadi Machi, 2023, tafiti zinaonyesha kutoweka kwa barafu iliyo katika kilele cha Mlima Kilimanjaro iwapo hatua madhubuti za kudhibiti mabadiliko ya tabianchi hazitachukuliwa.

Kwa mujibu wa tafiti hizo, jarida hilo linaeleza kuwa tangu mwaka 1912, kumbukumbu za mlima huo zilipoanza kuhifadhiwa, barafu imekuwa ikipungua kwa wastani wa nusu mita kila mwaka, na inabashiriwa kuwa huenda ikaisha kabisa ifikapo mwaka 2050.

Miongoni mwa sababu zinazotajwa kusababisha hali hiyo ni kuongezeka kwa joto duniani kunakotokana na shughuli za kibinadamu na uchomaji moto katika Mlima Kilimanjaro.

Habari hii imedhaminiwa na Taasisi ya Gates Foundation.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765 864 917.

Related Posts