Miezi minne kabla ya mkataba wake na PAOK kumalizika, mshambuliaji Mbwana Samatta ameanza kuichonganisha timu hiyo na mashabiki wake.
Moto ambao ameanza kuuwasha katika mechi za hivi karibuni, unaweza kubadilisha mawazo ya timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Ugiriki tofauti na ilivyokuwa mwanzoni mwa msimu.
Kabla ya msimu kuanza, Samatta alikuwa ni miongoni mwa wachezaji wa PAOK ambao walikaribia kuachana na timu hiyo kutokana na kutokuwa katika mipango ya benchi lake la ufundi na akabakia katika dakika za mwisho.
Hata hivyo mchango wa mabao ambao Samatta ameutoa kwa timu hiyo katika siku za hivi karibuni, umemfanya ageuke kipenzi cha mashabiki wa PAOK.
Samatta ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, katika mechi amehusika na mabao matano katika mechi tatu mfululizo za hivi karibuni ambazo PAOK imecheza.

Hiyo ni mara ya kwanza kwa Samatta kufanya hivyo tangu alipojiunga na PAOK, Julai 17, 2023 akitokea Fenerbahce kwa mkataba wa miaka miwili.
Katika mabao hayo matano aliyohusika nayo, amefunga manne na kupiga pasi moja ya mwisho.
Nyota ya Samatta imeanza kurudisha mng’ao wake katika mchezo wa Ligi Kuu ya Ugiriki dhidi ya OFI Crete, Februari 8, 2025 ambapo alifumania nyavu mara mbili huku timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 5-0.
Samatta alifumania nyavu mara moja katika mchezo uliofuata wa timu hiyo ambao ulikuwa ni wa Kombe la Europa League dhidi ya FCSB waliopoteza kwa mabao 2-1, Februari 13, 2025.

Jana Februari 16, 2025, Samatta amefunga bao moja na kupiga pasi moja ya mwisho katika ushindi wa mabao 7-0 ambao PAOK imeupata dhidi ya PAS Lamia katika Ligi Kuu ya Ugiriki.
Katika kuthibitisha kwamba Samatta amekuwa lulu kwa mashabiki wa PAOK, nahodha huyo wa Taifa Stars amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi wa mashabiki katika michezo dhidi ya FCSB na ule dhidi ya OFI Crete.
Katika zoezi la upigaji kura za kuchagua mchezaji bora wa mashabiki wa mechi ya jana dhidi ya Lamia, Samatta anashika nafasi ya pili hadi sasa akiwa amepata asilimia 9.4.
Kinara wa zoezi huyo ambaye ana nafasi kubwa ya kushinda ni Giannis Konstantelis aliye na asilimia 78.08.