Kigoma. Serikali imemkataa hakimu anayesikiliza mashauri mawili ya uchaguzi wa serikali za mitaa yaliyofunguliwa na chama cha ACT-Wazalendo katika Mahakama ya Wilaya ya Kigoma.
Kutokana na maombi hayo ya kumtaka ajiondoe kwenye mashauri hayo, hakimu huyo, Katoki Mwakitalu, atatoa uamuzi wake leo, Jumatatu, Februari 17, 2025.
Katika maombi hayo, mawakili wa Serikali wamemkataa Hakimu Mwakitalu, ajiondoe katika mashauri hayo kwa madai ya kutokuwa na imani naye, wakimtuhumu kutokuandika baadhi ya hoja wanazoziwasilisha.
Miongoni mwa mashauri hayo ni pamoja na lile lililofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Mtaa wa Gezaulole, Kata ya Gungu, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, Lovi Omary Lovi.
Lovi amefungua shauri hilo dhidi ya mgombea wa nafasi hiyo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), aliyetangazwa kuwa mshindi, Hassan Mashoto, aliyekuwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa Mtaa wa Gezaulole na Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Hivyo, Hakimu Mwakitalu atatoa uamuzi wake iwapo hoja hizo za mawakili wa Serikali, ambazo zilipingwa na mawakili wa ACT-Wazalendo, zina mashiko au la.
Hata hivyo, hakimu au jaji ana uhuru wa kuyakataa maombi ya wadaawa ya kumtaka ajiondoe katika kesi kama ataridhika kuwa sababu zilizotolewa hazina mashiko.
Kama ataona kuwa hoja zao zina mashiko, basi Hakimu Mwakitalu anaweza kuamua kujiweka pembeni ili apangiwe hakimu mwingine.
Lakini kama atajiridhisha kuwa hazina mashiko, anaweza kuzitupilia mbali na kuamua kuendelea na usikilizaji wa kesi hizo, ingawa pia anaweza kuzitupilia mbali na bado akaamua kujiweka pembeni kutokana na upande mmoja kuonyesha kutokuwa na imani naye.
Chama cha ACT-Wazalendo kimefungua mashauri 51 ya uchaguzi kote nchini katika Mahakama za Wilaya mbalimbali kupinga matokeo na mwenendo wa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Novemba 27, 2024.
Katika mashauri hayo, chama hicho kinalalamikia kugubikwa na kasoro nyingi za ukiukwaji wa sheria na haki kutotendeka.
Kati ya kesi hizo zilizofunguliwa katika wilaya za mikoa mbalimbali, taarifa hiyo ilizitaja wilaya ambazo mashauri hayo yamefunguliwa kuwa ni Temeke, Lindi, Ilala, Momba, Mkuranga, Mafia, Kigoma na Kibiti.
Katika mkoa wa Kigoma, chama hicho kilifungua mashauri 13, huku Manispaa ya Kigoma Ujiji kikiwa kimefungua mashauri tisa.
Awali, Serikali iliibua mapingamizi ya awali dhidi ya kesi karibu zote zinazoendelea kusikilizwa Kigoma, ikiomba mahakama iyatupilie mbali bila kuwasikiliza walalamikaji katika msingi wa hoja za malalamiko yao, kutokana na sababu tofauti za kiufundi.
Hata hivyo, jopo la mawakili wa ACT-Wazalendo lilipangua hoja hizo isipokuwa mashauri matatu tu ambayo mahakama imeyatupilia mbali.
Kiongozi wa jopo la mawakili wa ACT-Wazalendo, Emmanuel Msasa, amelieleza Mwananchi jana jioni, Jumapili, Februari 16, 2025, kuwa kati ya mashauri matatu yaliyotupiliwa mbali, wameridhika na uamuzi wa mahakama katika mashauri mawili.
Alisema kwa hayo mawili, wako katika mchakato wa kuyafungua upya baada ya kurekebisha kasoro zilizojadiliwa na mahakama, na kwamba uamuzi wa shauri moja hawajakubaliana nao, hivyo wako katika hatua za kukata rufaa.
Kwa mujibu wa Kiongozi mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, mawakili wa Serikali waliweka mapingamizi ya kuipotezea muda mahakama.
“Sasa tunakwenda kwenye kesi za msingi. Tunaanika uozo wote uliofanyika kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 ili kuweka msingi wa mabadiliko makubwa ya sheria za uchaguzi (electoral reforms),” alisema Zitto alipoandika ujumbe huo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X.