KAGERA Sugar inaendelea kupambana kujiepusha kushuka daraja Ligi Kuu Bara, lakini katika vita hiyo, ikashtukia uwezo wa staa wa timu hiyo, Peter Lwasa wakitaka kumuongezea mkataba mpango ambao hata hivyo mabosi wa klabu hiyo wamekutaka na kikwazo kidogo.
Kikosi hicho kilichocheza mechi 19 na kukusanya pointi 15 hdi sasa ikiwa nafasi ya 15 kati ya timu 16 za Ligi Kuu na kujiweka hatarini kurudi Ligi ya Championship (zamani Daraja la Kwanza) ikiwa ni miaka 20 sasa tangu ilipopanda 2005.
Timu hiyo imeanza msimu vibaya ikiruhusu katika mechi zao, huku katika michezo mitano ya mwisho ikipata ushindi mmoja tu dhidi ya Fountain Gate na kiungo mshambuliaji raia wa Uganda, Peter Lwasa alifunga mabao mawili yote ya penalti na kuwazima wageni wao kwa mabao 3-0.
Mabao hayo yamemfanya afikishe saba hadi sasa akiwa ndiye kinara wa timu hiyo yenye maskani yake mjini Bukoba na katika kuhakikisha wanaendelea kusalia na mchezaji huyo, mabosi wa Kagera waliamua kumuita mezani ili kumpa mkataba mpya, hata hivyo, jamaa amechomoa.
Inadaiwa, Lwasa aliyesajiliwa msimu huu kutoka KCCA amewaambia mabosi hao wasubiri kwanza hadi msimu utakapomalizika.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kagera, Thabit Kandoro ameliambia Mwanaspoti ni kweli, Lwasa ametaka kwanza kujikita kuisaidia timu hiyo iliyopo nafasi mbaya ili isishuke na ndipo ataamua hatma yake mwisho wa msimu huu.
“Tunajivunia nguvu ya Lwasa na wengine tuliowasajili msimu huu wamekuwa na tija sana na mtu kama Lwasa tulitaka kumuongezea mkataba, lakini ameomba tusubiri kwa kuwa timu ipo katika pabaya, hivyo anataka kwanza akili yake aielekeze kuisaidia timu,” alisema Kandoro na kuongeza;
“Haya yote tunayafanya kuhakikisha wachezaji walioonyesha kiwango bora basi tunawatunza na kama kuwapoteza basi iwe kwa kuwauza ili klabu iingize kipato kikubwa.”
Lwasa alisainishwa mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Kagera, ndiye kinara wa ufungaji ndani ya akifuatiwa na Saleh Seif Kambenga na Cleopas Mukandala wenye mabao mawili kila mmoja.
Wakati Lwasa akichomoa kusaini mkataba huo, taarifa zzaidi zinasema kiungo huyo yupo mbioni kuikimbia timu hiyo mwisho wa msimu endapo haitabaki Ligi Kuu kutokana na kuwepo kwa ofa nyingi mezani.