Dodoma. Serikali imetangaza mpango mahususi wa kukabiliana na msongamano wa magari katika majiji matano na miji mitatu nchini ikiwamo upanuzi wa barabara zinazoingia katika maeneo hayo.
Misururu ya magari imekuwa kawaida kuonekana asubuhi na jioni wakati watu wakielekea na kutoka kazini. Foleni zimekuwa ni za kawaida katikati ya majiji au miji inayokua.
Kiafya, foleni pia zinatajwa kusababisha maradhi ya akili, pumu, mfumo wa hewa, moyo na mzio utokanao na mafuta.
Msongamano wa magari pia husababisha wasafiri na madereva kuvuta hewa chafu itokanayo na mafuta ya magari na maradhi ya mfumo wa hewa kutokana na kutovuta hewa safi.
Wataalamu wa masuala ya kijamii wanaeleza madereva na abiria wamekuwa wakitumia muda mwingi kwenye foleni na kusababisha kupoteza muda wangeutumia kwenye uzalishaji.
Watumiaji wa barabara wengi hulazimika kusema uongo kwa kuchelewa katika mikutano ya kikazi, elimu, biashara na wakati mwingine kujikuta wakiadhibiwa kwa kuchelewa maofisini na majumbani, jambo linalosababisha kuyumba kwa uhusiano.
Kutokana na hilo, leo Jumatatu, Februari 17, 2025, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) imekutana na waandishi wa habari jijini Dodoma kuelezea miradi mbalimbali ikiwamo ya kukabiliana na msongamano katika majiji na miji.
Majiji hayo ni Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Dodoma na Mbeya pamoja na miji ya Moshi (Kilimanjaro), Manispaa ya Iringa (Iringa) na Mji wa Songea (Ruvuma). Jiji la Tanga si sehemu ya mpango huu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Lutengano Mwinuka amesema watu wamekuwa wakipoteza muda mwingi katika foleni, hivyo kufanya muda wa kufanya shughuli za kiuchumi kuwa chache.
“Ukipoteza muda ina maana shughuli uliyoipanga kuifanya hutaifanya kwa wakati, kama jambo ulitakiwa kufanya kwa saa 10 unajikuta ukifanya kwa saa nane. Muda unapotea wa kufanya kazi unapotea ukiwa njiani,” amesema.
Dk Lutengano amesema jambo jingine ni gharama zinaongezeka kwa maana ya mafuta yanatumika mengi wakati ukisubiri njiani, jambo linalofanya kutumia gharama kubwa kwenye usafiri.

“Mengine yanaweza kuambatana na hayo kama athari, lakini hayo ndio makubwa kutumia muda mwingi na hivyo kupunguza muda wa uzalishaji na pia gharama kubwa kwenye usafiri,” amesema.
Profesa wa uchumi, Haji Semboja katika moja ya mahojiano yake na Mwananchi aliyowahi kuyafanya, alichanganua hasara ya msongamano katika mtazamo wa upotevu wa muda na mafuta.
Profesa Semboja alisema msongamano wa magari unachangia uzembe kazini na imekuwa kawaida mtu kusingizia kuchelewa kwa sababu ya foleni.
“Jambo la muhimu ni kutafuta kiini cha tatizo, mfumo wa barabara ambao hauendani na mfumo wa maji, makazi, biashara, maisha na ofisi,” alisema.
Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu wa Tanroads, Ephatar Mlavi amesema mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, Machi 19, 2021 ni mengi.
Amesema mkakati huo wa kupunguza msongamano unahusisha miradi ya Miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), awamu ya pili, kilomita 20.3 (Mbagala – Mzunguko wa Bandari (Bendera Tatu), Bendera Tatu – Kariakoo, Sokoine – Zanaki, Barabara ya Kawawa – Barabara ya Morogoro (Magomeni).
Pia, barabara ya miundombinu ya BRT ya kilomita 23.3 kutoka katikati ya jiji hadi Gongo la Mboto ambao umefikia asilimia 74 na awamu ya nne unaohusisha kilomita 30.1 kutoka katikati ya jiji hadi Tegeta ambao umefikia asilimia 22.
Aidha, Serikali imekuwa ikijenga barabara za juu (flying over) katika Jiji la Dar es Salaam ambazo zimekamilika huku ikiona ulazima wa kupanua barabara ya kutoka Kimara hadi Gerezani kwa kuongezea njia moja kwa kila upande.
Mlavi amesema awamu ya tano ya mradi inayohusisha miundombinu ya BRT yenye urefu wa kilomita 25.4, kutoka Ubungo – Bandarini na Segerea – Tabata – Kigogo, uko katika hatua za mwisho za ununuzi.
Pia, ujenzi wa barabara ya Mzunguko wa Nje (Outer Ring Road) katika Jiji la Dodoma kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 112, ambao hadi kufikia Februari, 2025 umefikia asilimia 91 katika sehemu ya Kwanza ya Nala – Veyula – Mtumba – Ihumwa Bandari Kavu yenye urefu wa kilomita 52.3.
Mlavi amesema sehemu ya pili yenye urefu wa kilomita 62 inayotoka Ihumwa, Bandari Kavu-Matumbulu hadi Nala ujenzi wake ulikuwa umefikia asilimia 85.
Pia, amesema wanatekeleza mradi wa upanuzi wa barabara zinazoingia na kutoka katika Jiji la Dodoma kuelekea Chamwino katika Barabara Kuu ya Morogoro – Dodoma yenye urefu wa kilomita 32.

Foleni ya magari katika moja ya barabara jijini Mwanza.
Pia, Barabara Kuu ya Iringa hadi Dodoma kuelekea Mkonze yenye urefu wa kilomIta 4.5 pamoja na Barabara ya Arusha-Dodoma kuelekea Zamahero yenye urefu wa kilomita 8.5.
Jiji la Mwanza, wanafanya upanuzi wa Barabara Kuu ya Mwanza – Usagara – JPM Bridge kwa njia nne (kilomita 37) huku mkoani Mbeya wakiendelea na upanuzi wa Barabara Kuu ya TANZAM sehemu ya Uyole – Ifisi – Songwe Airport jijini Mbeya yenye urefu wa kilomita 36 kutoka njia mbili kuwa nne.
Mlavi amesema utekelezaji wa mradi huo wa Mbeya ulikuwa umefikia asilimia 22 hadi Februari mwaka 2025.
Kwa Jiji la Arusha na Kilimanjaro, Mlavi amesema wanaendelea na usanifu wa miradi ya upanuzi wa barabara za mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kwenye sehemu ya Barabara Kuu ya Tengeru – USA River.
Amesema ujenzi unahusisha barabara ya mchepuo ya Kwa Sadala ikijumuisha Daraja la Kikafu na sehemu ya Kibosho Shine hadi Kiboroloni.
Katika Manispaa ya Iringa, mkataba wa ujenzi wa barabara ya mchepuo umeshasainiwa na Mji wa Songea mkoani Ruvuma upo kwenye hatua ya ununuzi.
Akizungumzia ujenzi wa barabara nchini, Mlavi amesema barabara zenye urefu wa ya kilomita 15,625.55 zimekuwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji na barabara zenye urefu wa kilomita 1,365.87 zimekamilika.
Katika mkutano huo, Mlavi amesema kuna mikakati mbalimbali ya kuwajengea uwezo makandarasi wa ndani ikiwamo kutenga asilimia kumi ya bajeti ya kila mwaka ya maendeleo kwa ajili ya miradi ya mafunzo kwa vitendo.
Amesema kutenga angalau asilimia tano ya bajeti ya miradi ya maendeleo kwa ajili ya makundi maalumu.
“Kazi za matengenezo ya barabara na madaraja ziendelee kusimamiwa na makandarasi wazawa na kusimamiwa na washauri elekezi wazawa tu,” amesema Mlavi.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Wasafarishaji kwa Njia ya Barabara (Tarotwu), Mussa Nsese amesema changamoto ya msongamano barabarani ni jambo linalowafanya kulia.
Ameiomba Serikali izidi kuweka miundombinu itakayokidhi mahitaji ya ongezeko la watu na vyombo vya usafiri.
“Sasa hivi kwa Dar es Salaam wametuletea boti unazolipia Sh500 badala ya Sh200 tuliyoizoea ila zinatusaidia ukitaka kukaa muda mrefu unalipa ya Sh500 lakini ni wangapi ambao wanauwezo huo,” amehoji.
Ameshauri wananchi walioko pembezoni mwa barabara, wakubali Serikali iwape maeneo ili iweze kupanua barabara katika maeneo yao.
“Naomba Sh600 milioni ili niondoke hapa, kwa sababu wewe ni mwananchi na barabara ni kwa manufaa yetu sote tujaribu kuangalia hili,” amesema.
Mwenyekiti wa wenye Malori, Machuuki Msamba amesema wameshaiomba Serikali iwajengee njia ya kutoka maeneo yenye msongamano kwa muda mrefu sasa.
“Kwa mfano bandari imeboreshwa lakini kuboreshwa bandari sio kuboreshwa kwa barabara. Achana na barabara za katikati ya jiji, sisi tunaomba kuboreshewa barabara ya kuanzia Kibaha hadi Chalinze mkoani Pwani ambayo ni shida kubwa kwa wasafirishaji,” amesema Msamba.
Amesema wameomba kutengenezewa njia ya vumbi na kama ikiwezekana ifike hadi Morogoro na watakuja kuweka lami baadaye.
“Kutoka Kibaha hadi Chalinze unatumia kati ya saa tano hadi sita wakati ni mwendo usiozidi saa mbili hivyo ingetusaidia sana. Ukifika Mikese kuna barabara za mchepuo, zinatusaidia kidogo, shida kutoka Kibaha hadi Chalinze,” amesema Msamba.
Ameomba pia Serikali isaidie kupanua barabara ya kutoka Mbozi hadi Tunduma kwa kuwa wanakaa muda mrefu wakati mwingine hata siku tatu ili wavuke mpakani Tunduma.
“Watengeneze hata barabara za pembeni wananchi wapitie pembeni huko, unakuta hata bodaboda ikiharibika njiani lori haliwezi kupita. Kutoka Mbozi hadi Tunduma kuvuka baada ya siku tatu hata ‘service road’ hata boda ikiharibika lori haliwezi kupita,” amesema.