TCAA yaonya matumizi mabaya ya ‘drones’

Moshi. Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imesema kumekuwepo na matumizi mabaya ya ndege zisizo na rubani (drones), hali ambayo inatishia usalama wa anga.

Amesema licha ya teknolojia hiyo kuwa nzuri na muhimu, bado kumekuwepo na baadhi ya watu, ikiwemo waandishi wa habari, kuitumia vibaya kinyume cha sheria.

Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Salim Msangi, ameeleza hayo leo Jumatatu, Februari 17, 2025, wakati akikabidhi misaada mbalimbali katika Gereza Kuu la Karanga, Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Msangi ameonya watumiaji wote wa drones kuhakikisha wanafuata taratibu, ikiwemo kupata kibali cha kuiingiza, kuisajili na kupata kibali wakati wa kuitumia, na kwamba watakaokiuka watakamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

“Teknolojia ya drones ni muhimu na inatusaidia kwenye mambo mengi, lakini hivi karibuni tumekuwa na matumizi mabaya ya drones kwa baadhi ya watu, ikiwemo waandishi wa habari,” amesema Msangi.

Ameongeza kuwa, “Tuna sheria inayosimamia eneo hilo ambayo inasema unapotaka kuingiza drones lazima upate kibali, maana ile ni kama ndege inatumia anga letu. Lakini pia, inapaswa isajiliwe kama inavyosajiliwa ndege nyingine, na unapotaka kuitumia ni lazima upate kibali cha kuitumia.”

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya anga Tanzania (TCAA) Salim Msangi (Kushoto) akimkabidhi  Mkuu wa Magereza Kilimanjaro, Leonard Burushi baadhi ya misaada ya kibinadamu iliyotolewa na mamlaka hiyo

Aidha, amesisitiza kuwa katika maeneo ya magereza na majeshi yote, hairuhusiwi mtu kurusha drones, na kwa atakayekamatwa kwa kosa hilo, atachukuliwa hatua kali, ikiwemo kushtakiwa.

“Tutii sheria kuepuka kujiletea matatizo, kwani drones ni teknolojia ambayo imekuja kwa kasi na zinatumika kwenye shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

“Tulichofanya sisi kama mamlaka ni kuhakikisha tunatunga sheria ya kuzisimamia, kuweka utaratibu wa namna gani iruke ifanye shughuli zake, lakini isiathiri mwenendo wa ndege nyingine angani,” amesema.

Ameongeza kuwa, “Tusingependa kushuhudia ajali ya ndege yenye abiria 280 hadi 400 kwa sababu tu imegongana na drones. Hilo tusingependa litokee, na hata ninyi nadhani msingependa. Hivyo, tumeweka utaratibu kuhakikisha zinaingia kwa utaratibu, zinasajiliwa, na wakati wa kutumiwa tunajua zinatumika wapi.”

Aidha, kuhusu misaada ya kibinadamu waliyoitoa, Msangi amesema wamefanya hivyo ili kuwasaidia wafungwa na mahabusu wenye mahitaji mbalimbali, kwa kuwa nao wana mahitaji muhimu kama ilivyo kwa watu wengine.

“Mamlaka ya Usafiri wa Anga tumeona leo tukutane na uongozi wa Gereza Kuu Karanga ili kutoa huduma za kibinadamu kwa wenzetu waliopo hapa. Leo tumeanza na vitu hivi vidogo, lakini tutakapopata fursa nyingine tutawasaidia zaidi, maana ni watu ambao hawakupenda kuwa hapa, lakini wamelazimika kutokana na sababu mbalimbali. Tutakapowasaidia, pengine wanapotoka hapa na kurudi kwenye jamii watajirekebisha,” amesema.

Ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa taasisi mbalimbali za binafsi na za Serikali kuona umuhimu wa kuwasaidia wafungwa na mahabusu magerezani, kwa kuwa Serikali pekee haiwezi kuhudumia kila kitu.

Akizungumza, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kilimanjaro, Leonard Burushi, mbali na kuwashukuru TCAA kwa misaada waliyopeleka, ametoa wito kwa wadau wengine kujitokeza ili kutoa msaada, ili kuweza kukidhi mahitaji ya watu wanaowahudumia katika Gereza Kuu la Karanga, Moshi.

“Nashukuru tumetembelewa na TCAA na hiki walichotupatia kitatusaidia, kwa sababu kuna watu wana mahitaji makubwa ndani ya gereza. Nitoe rai kwa wenzetu wenye uwezo waweze kuguswa na kutoa mahitaji mbalimbali kwa wenzetu, kama magodoro, blanketi, viatu, sabuni na dawa. Walete na vitawafikia walengwa,” amesema.

Misaada iliyotolewa na TCAA ni pamoja na taulo za kike, sabuni, miswaki na dawa za meno.

Related Posts