Utafiti: Wajasiriamali wengi Tanzania wanakubali malipo ya kidijitali

Dar es Salaam. Utafiti mpya uliofanywa na kampuni ya kimataifa ya malipo (Visa) umeonyesha kuwa tabia ya wajasiriamali wadogo na wa kati nchini imebadilika ndani ya miaka miwili iliyopita, na asilimia kubwa wanakubali malipo ya kidijitali.

Utafiti huo unaoitwa ‘Thamani ya upokeaji: Kuelewa mazingira ya malipo ya kidijitali Tanzania,’ unaeleza kuwa asilimia 84 ya wajasiriamali hao waliohojiwa walieleza kuwa ndani ya miaka miwili iliyopita walianza utaratibu wa kupokea fedha kidijitali.

Ripoti ya utafiti huo inaeleza kuwa asilimia 64 ya wafanyabiashara hao wanaamini kupokea malipo kwa kadi ni uwekezaji wa kimkakati unaoweza kuchangia maendeleo ya baadaye ya biashara zao.

Aidha, ripoti inasisitiza kuwa zaidi ya asilimia 50 ya biashara ndogo na za kati zilizoko kwenye majukwaa ya masoko mtandaoni tayari zinatumia malipo ya kidijitali, ikidhihirisha ukuaji wa mfumo wa malipo wa kidijitali.

“Matokeo ya utafiti yanaonyesha taswira yenye matumaini kuhusu ukuaji wa malipo ya kidijitali Tanzania,” alisema Chad Pullock, ambaye ni msemaji wa Visa.

Pullock alisema faida zinazopatikana kwa wafanyabiashara, watumiaji, na uchumi kwa ujumla zinatoa fursa kubwa ya maendeleo. Visa imejizatiti kufanya kazi na wadau wote katika mfumo huu ili kufanikisha upatikanaji wa malipo ya kidijitali kwa wote nchini Tanzania.”

Kadhalika, ripoti hiyo inaangazia fursa muhimu za kuanzisha suluhisho za malipo ya kidijitali zinazotoa urahisi sawa na fedha taslimu, kama vile urahisi wa kurejesha malipo pamoja na usalama wa hali ya juu.

Hata hivyo, pamoja na maendeleo yanayotajwa katika ripoti hiyo, ni asilimia 30 tu ya biashara zinazotegemea fedha taslimu zilikosa mauzo au miamala kwa sababu wateja hawakuwa na pesa taslimu za kutosha.

Hata hivyo, utafiti umebaini changamoto kadhaa zinazoathiri kupanuka kwa matumizi ya malipo ya kidijitali Tanzania. Wengi wao wamekutana na changamoto kama kushindwa kwa malipo kutokana na matatizo ya kiufundi (yaliyotajwa na asilimia 47 ya wafanyabiashara) na gharama kubwa ya kupata mashine za POS.

Ripoti inapendekeza hatua za kushughulikia changamoto hizi ili kuongeza matumizi ya malipo ya kidijitali, moja wapo ikiwa ni kampeni za elimu ili kubadilisha tabia za walaji na kuhimiza matumizi ya njia za malipo ya kidijitali, pamoja na mipango ya uhamasishaji wa umma.

Related Posts