Wanaotoa mikopo umiza ujumbe wenu huu hapa

Geita. Serikali imezitaka kamati za ulinzi na usalama kuwachukulia hatua kali wale wanaotoa mikopo bila kuwa na leseni, pamoja na kuwanyang’anya leseni hizo wote wanaotoa mikopo bila kuzingatia masharti na kuwaumiza wananchi.

Mikopo hiyo, ambayo imepachikwa majina mengi ikiwemo kausha damu, komandoo, pasua moyo, kichefuchefu na mengine mengi, imekuwa ikitajwa kuwa chanzo cha kufilisika, kujiua, kuvunjika kwa mahusiano na kusababisha magonjwa ya akili baada ya wakopaji kushindwa kuilipa kutokana na masharti magumu.

Tatizo hilo, ambalo limesambaa katika maeneo mbalimbali nchini, limekuwa likiibua mijadala ndani na nje ya Bunge. Mathalani, Mei 2024, mbunge wa Viti Maalumu, Felista Njau, alitaka kufahamu Serikali inachukua hatua gani kwa kuwa wananchi mitaani wanaadhirika kwa kusombewa mali zao wanapochelewa kulipa.

Swali hilo lilisababisha mjadala huo kuwa mpana hadi Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, kuwaagiza mawaziri Dk Mwigulu Nchemba (Fedha) na Nape Nnauye (wakati huo akiwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) kwenda kulifanyia kazi kwa kuwa riba zake zimekuwa kubwa na zinawaumiza wananchi

Novemba 21, 2021, BoT ilitangaza kuzifungia programu tumizi (applications) zilizotoa mikopo kidijitali baada ya kubaini kuwa zinaendesha shughuli hiyo bila kuwa na leseni wala idhini.

Wakati mikopo hiyo ikiendelea kutolewa, leo Jumatatu, Februari 17, 2025, Serikali imejitokeza tena kutoa maagizo ya kupambana na tatizo hilo. Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, wakati wa ufunguzi wa jengo la ofisi ya Hazina Ndogo ya Mkoa wa Geita, akisema wimbi la mikopo umiza limeendelea kuwatesa wananchi.

Akisoma hotuba ya Dk Mwigulu, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo, amesema kumekuwa na changamoto katika sekta ya fedha, ikiwemo taasisi na watu binafsi kutumia mwanya wa uhitaji wa pesa miongoni mwa wananchi na kuwatoza riba kubwa kiasi cha kuwafilisi.

“Mikopo hii inajulikana kama mikopo umiza, kausha damu, chuma ulete, mikopo kuzimia na mengine mengi. Nitoe onyo kwa watu binafsi na taasisi zinazojihusisha na utoaji wa mikopo ya aina hii kuacha mara moja kwa kuwa jambo hili linarudisha nyuma wananchi na kuwaingiza kwenye lindi la umaskini,” amesema.

Aidha, amewataka wananchi kuwa na nidhamu ya fedha, ikiwemo kukopa kwa ajili ya uzalishaji mali badala ya matumizi ya kawaida, na kukopa kwenye taasisi zinazotambulika.

Kwa mujibu wa uchambuzi uliofanywa na na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kati ya Julai 2019 na Machi 2021, malalamiko 195 yalipokelewa kuhusu mikopo umiza.

Kati ya malalamiko hayo, asilimia 66 yalitoka kwa walimu (walio kazini na wastaafu), asilimia 12 yalitoka kwa wafanyabiashara, na asilimia 8 yalitoka kwa askari.

Aidha, asilimia 61.5 ya malalamiko yalihusu wakopeshaji binafsi, huku asilimia 38.5 yakihusu kampuni za ukopeshaji.

Baadhi ya wananchi wa mji wa Geita wameelezea namna mikopo umiza inavyowaumiza, wakisema wakopaji wengi hujikuta wakipoteza nyumba, mashamba na hata vifaa vyao vya kazi baada ya kushindwa kulipa madeni yaliyoongezeka kutokana na riba kubwa.

Ndekia Nazareth, mkazi wa Mtaa wa Mission, amesema baadhi ya familia zimesambaratika kutokana na ugumu wa kurejesha mikopo, lakini pia huchangia msongo wa mawazo kwa mkopaji.

Amesema licha ya mikopo kukopwa kwa lengo la kusaidia kuwainua wananchi kimaisha, mikopo hiyo imegeuka kuwaongezea umaskini kutokana na mzigo wa madeni.

Yohana Baraka, mkazi wa mji wa Geita, ameishauri Serikali kutoa elimu ya fedha kwa wananchi ili waelimishwe kuhusu mikopo salama, mipango ya fedha, na umuhimu wa kuwa na malengo kabla ya kukopa.

Amesema wanaotoa mikopo kinyume cha sheria wanapaswa kushitakiwa ili kulinda wananchi wasiendelee kunyonywa, na kushauri benki na taasisi halali za kifedha kutoa mikopo yenye masharti nafuu ili wananchi waepuke kukimbilia wakopeshaji wa mitaani.

Mwakilishi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Leah Komanya, ameishauri Wizara ya Fedha kuwajengea uwezo wahasibu ili kuondoa changamoto za uandaaji wa taarifa katika usimamizi wa fedha za Serikali.

“Fedha nyingi zinapelekwa halmashauri, lakini usimamizi ni mdogo. Ni vema wahasibu wajengewe uwezo ili waweze kusimamia na kuepuka ubadhirifu,” amesema.

Mshauri Mwelekezi kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Amina Lumuli, amesema jengo hilo limejengwa na mkandarasi Masasi Construction kwa gharama ya zaidi ya Sh4.3 bilioni.

Related Posts