Wanauliza, tuwapige ngapi? | Mwanaspoti

HAKUNA kulala wala kuzubaa ndivyo ilivyo katika mechi za duru la pili za Ligi Kuu Bara wakati leo tena vita itaendelea kwenye viwanja viwili tofauti, huku kazi kubwa ikiwa jijini Dar es Salaam wakati watetezi Yanga itakapovaana na Singida Black Stars, huku kila moja ikionekana kuwa moto.

Mchezo mwingine wa leo utapigwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, mjini Babati Manyara na wenyeji Fountain Gate itaikaribisha Tabora United, kila moja ikiwa imetoka kupata matokeo tofauti.

Mechi hizo zote zinapigwa saa 10:00 jioni na Yanga itakuwa KMC Complex, ambao juzi kati wametoka kuifumua KMC mabao 6-1, wakati wageni wao wakitoka kuzinduka mbele ya JKT Tanzania waliowanyoa bao 1-0 nyumbani kwao.

Mechi zote za leo zina kila dalili ya kuzalisha mabao mengi kutokana aina ya safu ya ushambuliaji walizonazo na pia udhaifu wa baadhi ya timu kuruhusu mabao hasa Fountain Gate ambayo ni mechi moja pekee ilicheza bila kuruhusu bao, huku nyingine 18 ikiruhusu.

Y 01

Yanga v Singida Black Stars

Unaweza kusema hii ni mechi ya kibingwa, Yanga yenye pointi 49 baada ya mechi 19, inapambana kuongeza pengo zaidi dhidi ya Simba yenye 47 ikishika nafasi ya pili ikicheza michezo 18.

Singida BS iliyotoka kuvunja rekodi ya JKT iliyokuwa timu pekee ambayo haikupoteza nyumbani msimu huu kabla ya kulala 1-0 lililowekwa kimiani na mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Jonathan Sowah aliyeanza Ligi Kuu na moto mkali, nayo inahitaji pointi tatu zitakazowaweka sehemu nzuri zaidi katika msimamo kwani inafahamu ikipoteza kuhatarisha kukaa nafasi ya nne kwa kasi ya Tabora Utd.

Kwa sasa Singida ina pointi 37, tano zaidi na ilizonazo Tabora yenye 32 na kama leo itaifyatua Fountain  na Singida kupoteza, itazifanya zitofautiane pointi mbili na hapo ndipo balaa litakuwapo kwa Wauza Alizeti.

Yanga inaingia katika mchezo huu ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa 1-0 ilipokutana na Singida mechi ya duru la kwanza, bao likifungwa na Pacome Zouzoua dakika ya 67.

Rekodi zinaonyesha mechi tano za mwisho Yanga imekuwa na matokeo mazuri zaidi ya wapinzani wao kwani imeshinda nne na sare moja wakati Singida imeshinda mbili na kupoteza mbili, sare moja.

Kwa mechi za nyumbani, Yanga imecheza 10 na kukusanya pointi 24 zilizotokana na kushinda 8 na kupoteza 2, imefunga mabao 30 na kuruhusu 7, hali hiyo inadhihirisha kuwa safu yao ya ushambuliaji ni hatari lakini ulinzi upo imara.

Y 02

Singida iliyotoka kucheza ugenini mechi mbili ikipoteza moja mbele ya KMC kwa mabao 2-0 kabla ya kushinda 1-0 dhidi ya JKT Tanzania, rekodi ya ugenini inaonyesha imecheza mechi 9 na kukusanya pointi 19, imeshinda 6, sare 1 na kupoteza 2, huku ikifunga mabao 12 na kufungwa 7, haina wastani mbaya wa kufunga mabao.

Ikumbukwe mchezo huu utamkutanisha Kocha Miloud Hamdi na Singida aliyokuwa akikinoa tangu Desemba 30, 2024 kabla ya kutambulishwa Yanga Februari 4, 2025 akichukua mikoba ya Sead Ramovic.

Kipindi chote ambacho ligi ilisimama kuanzia Desemba 28, 2024 kabla ya kuendelea Februari Mosi 2025, Kocha Hamdi alikuwa kambini Arusha akisuka mipango na kikosi cha Singida, hivyo ni wazi anawafahamu vizuri sana wachezaji wa timu hiyo kuliko wa Yanga aliokaa nao kwa takribani siku 12.

“Wanaonifahamu wanajua namna gani nina kuwa na uchu wa kupata ushindi, lakini hilo haliondoi ukweli kwamba tunapaswa kuwaheshimu wapinzani. Nikisema nawaheshimu wapinzani haimaanishi nina hofu, namaanisha mpira ni mchezo wa ushindani na kila mtu anatumia mbinu mbalimbali kujaribu kushinda hivyo lazima niende kwa tahadhari na umakini hata kama nahitaji kupata alama tatu.” Miloud Hamdi, huku kocha wa Singida, David Ouma alisema anajua hautakuwa mchezo mwepesi, lakini wamejiandaa kupambana kwa dakika 90 za mtanange huo.

Y 03

Fountain Gate vs Tabora United

Fountain Gate maarufu kama FOG, imekuwa haina matokeo mazuri katika mechi tano zilizopita na leo itavaana na Tabora United inayoonekana kuwa na moto mkali msimu huu mechi ikipigwa Manyara.

Fountain inayofundishwa na Mkenya Robert Matano, inarejea nyumbani baada ya kucheza mechi mbili mfululizo ugenini ilizopoteza bila ya kufunga bao lolote, ikianza kulazwa 2-0 na KenGold kisha kulala 3-0 na Kagera Sugar (3-0) baada ya awali kutoka sare ya 1-1 nyumbani na Simba.

Rekodi zinaonyesha timu hiyo ikiwa nyumbani imekusanya pointi 15 katika mechi 10 ikishinda nne, sare tatu na kupoteza tatu, ikifunga mabao 18 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 16 na leo inakutaa na Tabora United iliyotoka kushinda mechi mbili mfululizo kabla ya juzi kati kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na KenGold.

Walima asali hao kutoka Tabora wanaofundishwa na Anicet Kiazayidi, wanaenda ugenini wakifahamu rekodi kwa mechi za ugenini wamevuna pointi 13 baada ya kucheza mechi nane, wakishinda nne, sare moja na kupoteza tatu, huku wakifunga mabao 12 na kufungwa 13.

Y 04

Hapo katika kufungwa, inaonyesha timu zote hazipo imara eneo la kulinda jambo ambalo linaashiria tunaweza kushuhudia mchezo wenye mabao.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Sept 20, 2024 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora wageni Fountain Gate walishinda 3-1.

Offen Chikola mwenye mabao sita na asisti mbili, anaonekana kuwa ndiye nyota wa kutumainiwa wa Tabora sambamba na Heritier Makambo mwenye mabao matano kama aliyonayo Edger William wa Fountain ambaye atawaongoza wenyeji kutaka kuendelea ubabe na kuondoka jinamizi la vipigo.

Related Posts