Wasiwasi, usalama wa wanafunzi vyoo kuwa mbali na shule

Dar es Salaam. Wazazi wa wanafunzi wanaosoma Shule ya Msingi Tabata, wilayani Ilala, jijini Dar es Saalam wameonesha wasiwasi kuhusu usalama wa watoto wao wanaolazimika kuvuka barabara kufuata huduma ya vyoo.

Wanafunzi hulazimika kutembea umbali wa takribani mita 30 kufuata vyoo vilivyo nje ya eneo la shule, wakivuka barabara katika Mtaa wa Tabata Shule.

Barabara hiyo inatumiwa na vyombo vya moto ikiwa mbadala pale kunapokuwa na msongamano katika barabara ya kuelekea Segerea, hivyo kuwa hatari zaidi kwa wanafunzi kuvuka.

Shadya Saddick, mzazi wa mtoto shuleni hapo akizungumza na Mwananchi amesema watoto wenye umri mdogo ndio walio katika hatari zaidi.

“Napata hofu mtoto anapokuja shule, hatari kubwa ni kwa mtoto wa chekechea (darasa la awali) hata wa umri wa miaka saba au nane kutembea umbali huu hadi chooni akiwa peke yake, hivyo tunaiomba Serikali ifikirie kujenga vyoo karibu na madarasa ili kupunguza changamoto hii,” amesema Shadya.

Mbali ya hilo, anasema kwa mazingira ya choo kilivyo mtoto anaweza kudhuriwa pasipo mtu kujua. Choo hicho kina uzio wa mabati ambao haujakamilika eneo lote.

Mzazi mwingine, Jumanne Ismail, mkazi wa Mtaa wa Umoja amesema pia kuna changamoto ya usafi na usalama wa kiafya kwa watoto.

“Watoto wengine ili kuepuka safari ya kwenda chooni wanaamua kujibana jambo ambalo si salama kiafya. Tunahitaji watoto wetu walindwe kwa kuwawekea huduma karibu na salama,” amesema.

Mwalimu aliyezungumza na Mwananchi hivi karibuni kwa sharti la kutokutajwa jina amesema ni hatari kwa watoto kuvuka upande wa pili kwani wanatoka nje ya geti la shule kwenda chooni na kuna vyombo vya moto vinapita.

“Ni hatari kwao, sisi tunakuwa ndani na wao wanatoka wenyewe kwa hiyo kitakachotokea huko nje hatujui. Tumekuwa na vikao vya kufanyia kazi jambo hili,” amesema.

Amesema wazazi wameshaongea kwenye vikao kuhusu tatizo hilo akieleza uongozi wa shule umekusanya changamoto na kuzifikisha sehemu husika ili kuona namna ya kulitatua.

Bakari Omari, dereva wa pikipiki jirani na shule hiyo, amesema ameshashuhudia ajali wakati mtoto akivuka upande wa pili wa mtaa ambako kuna vyoo vya shule.

“Mara nyingi tunawaona watoto wadogo wakielekea chooni bila usimamizi jambo linalohatarisha usalama wao.  Tunashauri shule iwe na walinzi wa kuwasimamia wanapokwenda mbali,” amesema.

Amesema kuwazuia waendesha bodaboda ni ngumu kwani kila mmoja anakuwa na haraka zake licha ya kuwepo kwa tuta la kupunguza mwendo lakini halisaidii kuzuia ajali.

Akizungumza na Mwananchi Novemba 11, 2024, Diwani wa Tabata, Omary Matulanga alisema tatizo hilo wameliona na tayari wamefanyia kazi kwa kuomba msaada wa kutengenezewa vyoo ndani ya eneo la shule.

“Hii ni changamoto na tayari tulishakaa vikao na wenzangu kuzungumzia hili la vyoo kwani wanavyotumia si rasmi na si salama kwa wanafunzi,” alisema.

Alipotafutwa na Mwananchi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilala, Elihuruma Mabelya alielekeza suala hilo waulizwe watu wa kitengo cha habari na mawasiliano wa halmashauri.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Februari 17, 2025 Msemaji wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu kuzungumzia hali hiyo amesema jambo hilo lina hitaji utatuzi wa pamoja utakaoshirikisha kamati za shule, wananchi na viongozi wa eneo hilo ili kuja na majibu ya pamoja katika kutatua changamoto hiyo.

“Ukiangalia pale kuna eneo la shule na kuna barabara imepita hapo na kile choo kilijengwa kama sehemu ya shule, sasa tunafanyaje kwa pamoja kuitatua changamoto hiyo? Ni lazima kuangalia uhalali wa barabara ilipopita na huku choo kilipo ili tuone tunakuja na majibu ya pamoja,” amesema Tabu.

Amesema changamoto iliyopo kila mmoja anaiona, hivyo maandalizi ya sasa ni kuja na majibu ya pamoja ya kuondokana na tatizo hilo la wanafunzi kwenda kupata huduma upande wa pili wa shule.

Related Posts