Dar es Salaam. Said Ndomboloa na wenzake wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina mirungi zenye uzito wa kilo 145.20.
Mbali na Ndombokoa, washtakiwa wengine ni Hamisi Ndomboloa na Amor Seiph.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Jumatatu, Februari 17, 2025, na kusomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Asiat Mzamiru, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo.
Wakili Mzamiru amedai kuwa Julai 18, 2019, eneo la Gongo la Mboto, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilo 105.17, kinyume cha sheria.
Shtaka la pili, Julai 18, 2019, katika ofisi za Posta zilizopo wilaya ya Ilala, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha kilo 40.03 za mirungi, kinyume cha sheria.
Baada ya kusomewa mashtaka yao, upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na wapo katika hatua za kusajili taarifa na nyaraka muhimu Mahakama Kuu.
Baada ya kueleza hayo, hakimu Swallo ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 3, 2025 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili hayana dhamana.