Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amesema Jiji la Dar es Salaam litakapoanza kufanya biashara saa 24 mapato ya Wafanyabiashara yataongezeka sambamba na kukua kwa uchumi wa nchi kwa ujumla kutokana na kuongezeka kwa wigo wa biashara.
Ameyasema hayo leo tarehe 18.02.2025 alipomtembelea Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda ofisini kwake na kueleza kuwa uzinduzi wa Biashara saa 24 unatarajiwa kufanyika Februari 27 mwaka huu.
Mhe. Chalamila amesema wanatarajia kuongeza idadi ya Wafanyabiashara kupitia kufanya biashara saa 24 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam jambo ambalo litaongeza wigo wa ukusanyaji wa Kodi kwa upande wa TRA.
Amesema kwa utaratibu waliouweka biashara zote zitasajiliwa na kupatiwa Leseni kwa upande wa Halmashauri na namba ya utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa upande wa TRA hali itakayorahisisha ulipaji wa Kodi.
“Ili kufanikisha jambo hili la biashara saa 24 tayari tumeanza kukaa na kuzungumza na wadau mbalimbali wakiwemo wa usafirishaji ili na wao waanze pindi tutakapoanza” amesema RC Chalamila.
Amesema walifikia uamuzi wa kurasimisha biashara saa 24 kutokana na kuwepo kwa baadhi ya maeneo kuwa yanakesha lakini pia kuwepo kwa huduma za usafiri wa mabasi saa 24 hali inayosababisha kuwepo kwa mahitaji ya usafiri saa 24 ndani ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na huduma za chakula.
Ameyataja maeneo yatakayoanza kufanya biashara saa 24 kuwa ni Kariakoo, Magufuli Terminal, Tandika, Mbagala, Bunju, Manzese na Mwenge.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda akizungumza katika kikao hicho amesema TRA ipo tayari kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha biashara inafanyika saa 24.
Bw. Mwenda amesema kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam watahakikisha kuna kuwa na ustawi wa biashara pamoja na utulivu jambo ambalo litawavutia watu wengi zaidi kuingia kwenye biashara.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema miongoni mwa majukumu ya TRA ni kusimamia ustawi wa biashara hivyo mahala popote panapogusa kuweka mazingira mazuri ya biashara TRA ipo tayari kusaidia ili kuweka mazingira rafiki na mazuri kwa walipakodi kufanya biashara zao.
Mwisho.