CRDB yavuka lengo mauzo ya hatifungani ya miundombinu

Dar es Salaam. Benki ya CRDB imetangaza mafanikio makubwa ya hatifungani ya miundombinu ya ‘Samia Infrastructure Bond,’ iliyovuka lengo kwa asilimia 115, ikikusanya Sh323bilioni ambayo ni zaidi ya mara mbili ya lengo la kukusanya Sh150 bilioni.

Leo Februari 18, 2025 wakati wa maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema mafanikio yaliyopatikana yanadhihirisha ukubwa na uwezo wa uwekezaji walionao wananchi.

Pia, amesema mafanikio hayo ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na menejimenti ya Benki ya CRDB ikishirikiana na Tamisemi kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) huku akisisitiza kuwa, matunda yake yatawanufaisha Watanzania wengi.

 “Tumepata wawekezaji wengi binafsi kwa sababu walimudu kiwango cha chini cha shilingi 500,000 tu. Fedha zote tulizozikusanya kwenye mauzo ya hatifungani hii zitatumika kuwawezesha makandarasi wa wanaotekeleza na watakaoshinda zabuni zitakazotangazwa na Tarura. Tunaamini upatikanaji wa fedha hizi utasaidia kwa kiasi kikubwa kukamilisha miradi kwa wakati,” amesema Nsekela.

Amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana wawekezaji wake kwa miaka mitano ya uhai wa hatifungani hiyo kama walivyowaahidi wakati wa mauzo yaliyofanyika nchi nzima ikiwamo kulipa riba ya asilimia 12 kwa mwaka itakayotolewa kwa awamu nne.

“Malipo ya riba yatakuwa yanafanyika kila tarehe 10 Februari, 10 Mei, 10 Agosti na 10 Novemba. Kwa mwaka huu, wataanza kupokea malipo ya faida tarehe 10 Mei,” amesema Nsekela.

Katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ameipongeza Benki ya CRDB kwa mafanikio makubwa ya mauzo ya Hatifungani hiyo huku akielezea umuhimu wake.

Waziri Mchengerwa amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) katika kuboresha miundombinu ya usafiri na kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji nchini.

“Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond ni mfano halisi wa namna ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi unavyoweza kuleta manufaa kwa taifa letu. Kiasi hiki cha Sh323 bilioni kilichokusanywa kinatoa mwanga wenye matumaini kwa maendeleo ya miundombinu hasa ya barabara huko mbeleni,” amesema Waziri Mchengerwa.

Tangu Novemba 29, 2024 uzinduzi wa mauzo hayo ulipofanyika mpaka Januari 17 mwaka huu, dirisha hilo lilipofungwa, kampuni na taasisi 327 zimejitokeza kuwekeza Sh118.99 bilioni pamoja na watu binafsi 6,896 waliowekeza jumla ya Sh204.1 bilioni.

Asilimia 94 ya kiasi chote kilichopatikana kimekusanywa kupitia Programu ya SimBanking.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tarura, Victor Seff amesema ushirikiano huo ulioanzishwa kati ya Benki ya CRDB na Tarura utakuwa na manufaa makubwa katika utekelezaji wa miradi ya barabara nchini.

“Tunayo miradi mingi inayotekelezwa katika maeneo tofauti na changamoto kubwa iliyokuwepo ilikuwa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya malipo ya makandarasi. Naamini wengi sasa watapata fedha zao kwa wakati ili kukamilisha miradi kwa muda uliopangwa,” amesema Mhandisi Seff.

Mkurugenzi Mtendaji wa CMSA, CPA Nicodemus Mkama amesema kuorodheshwa kwa Samia Infrastructure Bond kumeongeza thamani ya uwekezaji katika hatifungani za kampuni na taasisi kwa asilimia 38.9 na kufikia Sh1.16 trilioni kutoka Sh837.31 bilioni.

“Samia Infrastructure Bond ni kielelezo wazi cha nguvu za masoko yetu ya mitaji na kufanya Soko la Hisa la Dar es Salaam kuwa mchezaji muhimu katika kuwezesha uwekezaji katika miradi ya miundombinu ya kitaifa ya Tanzania,” amesema Mkama.

Pia, baada ya kutangaza matokeo ya mauzo, hatifungani hiyo iliorodheshwa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ili kuwaruhusu wawekezaji waliochelewa kupata nafasi ya kushiriki kuijenga nchi yao huku wakipata faida ya asilimia 12 itakayotolewa kwa kipindi chote cha miaka mitano.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela amesema kila siku idadi ya Watanzania wanaoshiriki sokoni hapo inazidi kuongezeka jambo linalotia matumaini kwamba, litazidi kukua, hivyo kuwa na manufaa makubwa baadaye.

“Mafanikio zinazopata kampuni zililizoorodheshwa sokoni ni mafanikio ya soko zima. Sisi wasimamizi wa soko tunapata faraja kuona mambo yanaenda vizuri kila kunapokuwa na bidhaa mfano wa hatifungani hii ya Samia Infrastructure Bond ya Benki ya CRDB,” amesema Nalitolela.

Related Posts