DCEA yanasa bustani ya bangi ndani ya nyumba

Dar es Salaam. Licha ya udhibiti mkali wa kilimo cha bangi, wakulima wamebuni mbinu mpya za kukwepa mkono wa dola, ikiwemo kupanda miche kwenye makopo.

Mkoani Arusha, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imemkamata mtu anayedaiwa kuotesha miche ya bangi ndani ya nyumba yake.

Mtuhumiwa huyo, ambaye jina lake halijawekwa wazi, inaelezwa alikamatwa akiwa ameotesha zaidi ya miche 200 kwenye eneo alilotengeneza kwa ajili ya shughuli hiyo nyumbani kwake, Mtaa wa Kijenge, Kata ya Moshono.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema bila taarifa za kiintelejensia, isingekuwa rahisi kubaini mbinu hiyo ya kuotesha bangi nyumbani.

Amesema huenda ndiyo mbinu inayotumiwa na baadhi ya watu wanaoendeleza kilimo haramu cha bangi.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Februari 18, 2025, Lyimo amesema baada ya kupata taarifa kuhusu mtuhumiwa, walimfuatilia na hatimaye siku ya tukio waliingia nyumbani kwake na kukuta ameotesha bangi kwenye makopo na glasi za plastiki.

 “Kama watu wapandavyo maua, tulikuta huyu mtu amepanda miche ya bangi nyumbani kwake. Hii imetushtua kidogo kwa sababu mbinu aliyotumia hatukuwahi kuiona awali ya mtu kulima bangi nyumbani.

“Ukiingia nyumbani kwake unaona ni nyumba ya kawaida. Unapofika kwenye mlango wa kutokea nyuma ndipo unakuta kuna chumba kama bwalo chini hakujasakafiwa na juu kimeezekwa, ila kuna sehemu ya bati imeachwa wazi ili kuruhusu mwanga kuingia,” amesema, na kuongeza:

“Pale tulikuta zaidi ya miche 200 ikiwa imepandwa kwenye vikopo huku kukiwa na vikopo vingine ambavyo vimeandaliwa kwa ajili ya kupandwa miche.”

Kutokana na hilo, amesema mamlaka itaanza ukaguzi wa nyumba kwa nyumba hasa katika mikoa ambayo imeathiriwa na kilimo cha bangi.

Katika hatua nyingine, taarifa ya DCEA leo Februari 18, 2025 imesema kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, imeteketeza ekari 336 za mashamba ya bangi yaliyokuwa ndani ya hifadhi ya Ikome wilayani Kondoa, mkoani Dodoma, yakichanganywa na mazao mengine.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema kwa taarifa walizonazo, mashamba hayo yalianza kuandaliwa Desemba 2024.

Katika operesheni hiyo, wananchi wa vijiji jirani walijitokeza kufyeka bangi iliyolimwa shambani.

Hii ni operesheni kubwa ya kwanza kufanyika mkoani Dodoma, ikionyesha wazi kuwa kilimo cha bangi kimeanza kuenea katika baadhi ya maeneo ya mkoa huu.

“Tulipata taarifa za awali wakati mashamba yanaandaliwa, tulifuatilia na hatimaye tumekuta bangi ikiwa imelimwa katika hatua za awali.

“Tutaendelea kuchukua hatua kali kudhibiti uzalishaji, biashara na matumizi ya dawa za kulevya, hata kama wahusika watajaribu kutumia mbinu mpya kama walivyofanya Kondoa kwa kuchanganya bangi na mazao mengine kama mahindi na maharage,” amesema.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Haubi, Fatina Ramadhani, amekiri kuwa baadhi ya wananchi katika eneo hilo wanajihusisha na kilimo cha bangi, na amewataka kuachana nacho.

“Tunafanya mikutano ya kijamii ambayo hueleza bayana madhara ya dawa hizi. Pia tunafanya doria katika msitu huu kwa kushirikiana na polisi jamii, askari wa akiba na wahifadhi ambao ni TFS,” amesema.

Mhifadhi wa Misitu, Amon Mlimwa, amesema, “TFS itaendelea na doria kila siku kwani viongozi wa kijiji na kata ya Haubi wamekubali kushirikiana nasi kuhakikisha tunalifanikisha hili”

Mkazi wa Mafai, Kata ya Haubi, Abushekhe Kalinga, amesema baadhi ya vijana wanajihusisha na matumizi ya bangi.

“Vijana wengi walikuwa wameshaanza kuathirika, japo wengine wanadai wanalima bangi kwa ajili ya pesa, lakini ukilinganisha hasara na faida, hasara ni kubwa zaidi kuliko faida. Vita dhidi ya dawa za kulevya inahitaji juhudi za pamoja kwa Serikali, jamii na vyombo vya usalama kushirikiana,” amesema.

Kati ya Januari na Februari 2025, DCEA kupitia ofisi zake za kanda, imekamata kilo 790.528 za aina mbalimbali za dawa za kulevya katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Mbeya, Mtwara na Dar es Salaam.

Related Posts