Arusha. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Masijala imewahukumu kifungo cha maisha jela watuhumiwa wawili baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin.
Hukumu hiyo ilitolewa Februari 14, 2023 na Jaji Sedekia Kisanya na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Waliohukumiwa adhabu hiyo ni Jimmy Mlaki na Stanley Ngowi ambao walidaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) na (3) (i) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, vikisomwa kwa pamoja na aya ya 23 ya jedwali la kwanza la sheria na vifungu vya 57 (1) na 60 (2) vya Sheria ya Kudhibiti Uhalifu wa Kiuchumi na Kupangwa (EOCCA).
Watuhumiwa hao walidaiwa Januari 27, 2020 walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroin yenye uzito wa gramu 509.63 katika eneo la Ubungo Kibo, mkoani Dar es Salaam.
Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 34 ya mwaka 2023, upande wa mashtaka uliokuwa na mashahidi nane na vielelezo 14 uliwakilishwa na jopo la mawakili tisa huku utetezi wakiwa mawakili wanne.
Jaji Kisanya baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili katika kesi hiyo amesema kwenye makosa ya jinai ni kanuni iliyoimarishwa kwamba upande wa mashtaka unabeba mzigo wa kuthibitisha hatia ya mshitakiwa bila kuacha shaka yoyote.
Amesema baada ya kupitia pande zote mbili, upande wa mashtaka umethibitisha kuwa washtakiwa walikutwa wakisafirisha dawa hizo za kulevya zilizokuwa kwenye mifuko miwili ya plasitiki.
“Upande wa utetezi umeshindwa kuleta shaka ya kutosha katika kesi ya mashtaka, ushahidi unaonyesha kuwa washtakiwa walikuwa na gramu 509.63 za dawa za kulevya.
“Kutokana na hali hiyo, washitakiwa hao, Jimmy na Stanley wanakutwa na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya na kutiwa hatiani kwa kosa hilo na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha jela,” amesema Jaji Kisanya.
Sambamba na hukumu hiyo, Mahakama hiyo ilitoa amri kuwa dawa hizo za kulevya (kielelezo cha sita na saba) na vifungashio vyake vitaharibiwa au kushughulikiwa vinginevyo kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kutekeleza Dawa za Kulevya na kanuni zake.
Jaji Kisanya amesema gari lenye namba za usajili T776 DSE (kielelezo cha 12) na kadi yake (kielelezo cha 10) zitarudishwa kwa mmiliki wake halali, Amina Nuhu Mvungi, kwa kuwa hakuna dalili kuwa alikuwa na dawa hizo za kulevya.
Awali, ilidaiwa siku ya tukio shahidi wa nne wa mashtaka, Inspekta Beatus aliongoza timu ya maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) wakiwa doria eneo la Magomeni, Dar es Salaam, saa tatu usiku, alitafutwa na mtoa taarifa wa siri kuhusu biashara ya dawa za kulevya iliyotarajiwa kufanyika eneo la Ubungo.
Inspekta huyo aliwapa taarifa wenzake na kuongozana na mtoa taarifa huyo wakiwa kwenye magari mawili hadi eneo walilokuwa watuhumiwa hao.
Ilidaiwa kuwa mtoa taarifa alilitaja gari aina ya Toyota Sienta lililokuwa na namba za usajili T776 DSE lililokuwa limeegeshwa eneo la Ubungo Kibo, ambapo baada ya mtoa taarifa kuonyesha gari hilo, aliondoka na kuwaacha maofisa hao wa DCEA.
Upande wa mashtaka uliendelea kudai kuwa maofisa hao walipokaribia gari hilo lililoshukiwa, washtakiwa hao walijaribu kukimbia lakini walikamatwa mbele ya mjumbe wa uongozi wa mtaa na shahidi huru wakati wa upekuzi.
Shahidi wa nne, alidai kuwaamuru washukiwa hao kutoka nje ya gari na kuwajulisha kuhusu tuhuma zinazowakabili ambapo wakati wa upekuzi huo mshitakiwa wa kwanza alikutwa na mkoba ambao ndani yake uligundulika kuwa na mifuko miwili ya plastiki iliyokuwa na unga unaoshukiwa kuwa ni dawa za kulevya pamoja na vitu vingine 15 ikiwemo simu za mkononi.
Wakijitetea mahakamani hapo, Jimmy alidai alikuwa akiishi kwa miaka mitano eneo la Mirerani mkoani Manyara kwenye Kitalu D, kwenye kampuni ya uchimbaji madini inayomilikiwa na mjomba wake ambapo yeye alikuwa akifanya kazi kama Mwanajiolojia Msaidizi.
Alidai Januari 26, 2020 mwajiri wake alimwagiza jijini Dar es Salaam akiwa na wenzake wawili kwa ajili ya kununua vifaa vya uchimbaji madini ambapo walifanikiwa kununua vifaa hivyo kisha akawataarifu wenzake kuwa atakutana na rafiki yake, Abel Shoo na kuhudhuria maombi katika Kanisa la Mchungaji Gwajima lililopo Ubungo.
Alidai baada ya kufika eneo la Ubungo-Maji, akiwa kwenye bodaboda, alikamatwa ghafla na askari polisi na kumpiga kofi, kuingizwa kwa nguvu kwenye gari aina ya Land Rover Defender, ambako alikuta wanaume watano na mwanamke mmoja ambaye hakuna hata mmoja aliyemfahamu.
Alidai alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar ss Salaam na kuwekwa mahabusu bila maelezo yoyo ambapo alikaa kwa zaidi ya siku 30 kuanzia Januari 27 hadi Machi 3, 2020 alipofikishwa mahakamani Kisutu.
Mshitakiwa wa pili, alidai Januari 26, 2020 akiwa anaangalia mpira wa miguu katika eneo la Toto Tundu, Tabata Segerea, kulizuka zogo na kusababisha watu kukamatwa.
Alidai kuwa alipigwa na mtu ambaye awali alidhani ni raia. Alipojaribu kujitetea, askari polisi walifika na kushuhudia matendo yake, wakampiga na kumshutumu kwa kumshambulia ofisa wa polisi.
Alidai kuwa aliwekwa kwenye gari na mahabusu wengine na kupelekwa kituo cha polisi, ambapo alipigwa sana na kuachwa akiwa amepoteza fahamu, alifungiwa katika chumba cha mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi na baadaye kupelekwa Mahakama ya Kisutu ambako alisomewa shitaka la kusafirisha dawa za kulevya.
Mbali na maelezo hayo mshitakiwa huyo alikana hajawahi kuona vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo, hajawahi kusaini nyaraka zozote zinazohusina na kesi hiyo ikiwemo cheti cha kukamata na maelezo ya onyo na kusisitiza hana hatia, hivyo anaomba Mahakama imuachie huru.