Dar es Salaam. Hayo yameelezwa leo wakati shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) lilipokutana na wadau mbalimbali kujadili changamoto ya unywaji wa pombe zilizozalishwa na kuuzwa kwa njia haramu.
Warsha hiyo iliwaunganisha wadau muhimu wa sekta ya viwanda, watunga sera, na mamlaka za udhibiti kama Wizara ya Afya, Wizara ya Mambo ya Ndani, Tume ya Ushindani (FCC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), na wadau wengine muhimu katika sekta ya pombe.
Katika warsha hiyo iliyofanyika jana CTI ilisisitiza hatari kubwa za kiafya zinazotokana na pombe zisizodhibitiwa, ikiwa ni pamoja na viwango vya juu vya sumu, madhara ya muda mrefu kama ugonjwa wa ini, upofu, na hata vifo.
Aidha, CTI lilieleza kuwa pombe haramu huchangia matatizo ya kijamii kama uhalifu, unyanyasaji wa majumbani, na kushuka kwa ufanisi kazini, hali inayoongeza mzigo kwa mifumo ya afya na ustawi wa jamii.
Katika warsha hiyo aliyekuwa mwenyekiti wa Mwenyekiti wa zamani wa CTI, Paul Makanza, alisema, mapambano dhidi ya pombe haramu si tu suala la udhibiti ni juhudi za kulinda maisha ya Watanzania, kulinda mapato ya serikali, na kuendeleza mazingira ya biashara yenye ushindani wa haki.
“Pombe haramu inahatarisha afya ya umma, inachochea matatizo ya kijamii, na inadhoofisha sekta rasmi ambayo inatoa maelfu ya ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi. Tunahitaji kuimarisha utekelezaji wa sheria na sera huku tukiendelea kuongeza uelewa ili kuhakikisha sekta ya pombe inayowajibika na endelevu ambayo inachangia maendeleo ya Tanzania kwa njia chanya,” anasema.
Ili kulinda afya ya umma na uthabiti wa uchumi, Makanza ilitoa wito wa udhibiti mkali wa sekta ya pombe, ikisisitiza umuhimu wa kuimarisha imani ya wawekezaji, kuhamasisha unywaji wa pombe kwa uwajibikaji, na kuwalinda wananchi dhidi ya bidhaa hatari.
Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi, anasema “Sisi, tunaamini kuwa mafanikio ya kweli katika sekta hii hayapimwi tu kwa utendaji wa kifedha, bali pia kwa uwezo wetu wa kuchangia maendeleo endelevu ya jamii yetu. Matumizi mabaya ya pombe ni hatari kwa kila mtu na jamii na kushughulikia changamoto hii kunahitaji ushirikiano.”
Aidha mbali na athari za kiafya, utafiti uliofanywa na kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya Ernest & Young mnamo Novemba 2018 ulibaini kuwa serikali ya Tanzania inapoteza takriban Sh1.2 trilioni kila mwaka kutokana na biashara ya pombe haramu.
Mauzo yasiyodhibitiwa yanadhoofisha biashara halali na kusababisha hasara kubwa ya mapato ya kodi, hali inayopunguza uwezo wa serikali kufadhili huduma muhimu kama afya na elimu. Zaidi ya hayo, sekta rasmi ya pombe ambayo inatoa maelfu ya ajira inakabiliwa na ushindani usio wa haki kutoka kwa waendeshaji wasiosajiliwa ambao wanakwepa kanuni za usalama na viwango vya ubora.