NYOTA wawili wa Pamba Jiji FC, Mkenya Mathew Momanyi Tegisi na Abdoulaye Yonta Camara raia wa Guinea, wameongeza mzuka ndani ya kikosi hicho kutokana na mchango wao wanaouonyesha kikosini, tangu wajiunge dirisha dogo la Januari mwaka huu.
Momanyi ametokea Shabana FC ya kwao Kenya, huku kwa upande wa Camara akijiunga na kikosi hicho kwa mkopo kutoka Singida Black Stars, alichojiunga nacho Agosti 14, mwaka jana, ila alishindwa kushindania nafasi na Mkenya Elvis Rupia kikosini.
Tangu nyota hao wawili wajiunge na kikosi hicho kilichopanda Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kushuka daraja mwaka 2001, wamekuwa muhimili mzuri eneo la ushambuliaji na kusababisha kushinda michezo yote mitatu mfululizo kwa mara ya kwanza.
Katika michezo hiyo mitatu mfululizo iliyoshinda Pamba, ilianza kwa kuzifunga Dodoma Jiji na Azam FC bao 1-0, kila mmoja wao, huku mechi ya mwisho iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ikaifunga pia Coastal Union mabao 2-0.
Katika ushindi huo, nyota wote wawili wamechangia kwa asilimia 100 na Momanyi amefunga bao moja na kusaidia mengine mawili kwa maana ya ‘Asisti’, huku kwa upande wa Camara akitupia kambani moja na kuasisti moja vile vile.
Momanyi alifunga bao moja hilo katika ushindi wa timu hiyo wa 1-0, dhidi ya Dodoma Jiji Februari 6 na kuasisti mbili wakati kikosi hicho kiliposhinda kwa mabao 2-0, mbele ya Coastal Union CCM Kirumba Mwanza Februari 15.
Nyota huyo ni kama ameendeleza pale alipoishia wakati akiwa na Shabana FC, kwani kabla ya kujiunga na Pamba Jiji alikuwa amefunga mabao matano kwao Kenya, nyuma ya nyota mwingine wa kikosi hicho, Brian Michira aliyekuwa anaongoza na saba.
Kwa upande wa Camara amefunga moja katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-0, dhidi ya Coastal Union Februari 15, huku akiasisti wakati Pamba ilipoifunga Azam FC bao 1-0, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza Februari 9.
Camara alijiunga na Singida Agosti 14, 2024, ingawa kitendo cha kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara mbele ya Mkenya Elvis Rupia mwenye mabao manane hadi sasa, kikamfanya kutolewa kwa mkopo kwenda Pamba Jiji dirisha dogo la Januari mwaka huu.
Camara alitua nchini akitokea Milo FC ambapo msimu uliopita aliibuka mfungaji bora baada ya kufunga mabao 21 na kuwavutia mabosi wa Singida, huku akiwahi kuzichezea pia, AS Ashanti Golden Boys na Wakriya AC zote za kwao Guinea.