Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imesema kuwa jeshi la Rwanda na washirika wake wameingia katika mji wa Bukavu, mashariki mwa nchi hiyo, katika jimbo la Kivu Kusini, na kuwataka wananchi kuwa macho.
Wizara ya Mawasiliano ya DRC imesema kupitia mtandao wa X kwamba: “Serikali inafuatilia hali inayoendelea Bukavu, kufuatia kuingia huko kwa jeshi la Rwanda na washirika wake.”
Waasi wa M23 walidai siku ya Ijumaa kuwa wameuteka uwanja wa ndege wa Kavumu, ulioko kilomita 25 (maili 15) kutoka mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, Bukavu.
Aidha, waasi hao wameingia Bukavu baada ya kuteka mji wa Kavumu. Serikali ya DRC imelaani kupuuzwa kwa suluhisho la amani na imeitaka jamii ya kimataifa kusaidia kusimamisha mapigano.
Taarifa ya Wizara ya Mawasiliano ya DRC imesema: “Rwanda inasisitiza mpango wake wa kukalia kwa mabavu ardhi, kupora mali na kufanya uhalifu pamoja na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika ardhi yetu.”
Hata hivyo, Rwanda imekana mara kwa mara madai hayo kwamba inawaunga mkono waasi.