Katibu Bavicha Mwanza adaiwa kutoweka, Polisi waanza uchunguzi

Mwanza. Katibu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Mkoa wa Mwanza, Amani Manengelo anadaiwa kuchukuliwa na watu waliojitambulisha kuwa ni maofisa wa polisi mkoani humo.

Kwa mujibu wa Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zacharia Obad, katibu huyo (Manengelo), alichukuliwa na watu hao na kuondoka naye Februari 14, 2025 saa 12:30 jioni, eneo la Misungwi mkoani humo.

Hata hivyo, leo Jumanne Februari 18, 2025, Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limethibitisha kupokea taarifa ya kutoweka kwa kiongozi huyo wa Bavicha mkoani humo, huku likidai kuwa bado waliomchukua hawajafahamika.

Taarifa iliyotolewa kwa umma na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Audax Majaliwa imesema jeshi lilipokea taarifa ya kupotea kwa Manengelo jana Jumatatu kutoka kwa Katibu wa Chadema wilayani humo, Peter Daniel akidai Manengelo ametoweka na hajulikani alipo huku akidokeza kuwa ufuatiliaji wa tukio hilo umeshaanza.

“Kituo cha Polisi Misungwi Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kutoka kwa Peter Daniel na viongozi wengine wa Chadema kuwa Amani Manengelo haoenekani nyumbani kwake wala kwa ndugu na jamaa tangu tarehe 14, Februari, mwaka huu na kwamba, alichukuliwa na watu ambao hata hivyo hawakuweza kufahamika, hadi sasa hajulikani yuko wapi na yuko katika hali gani,” amasema Majaliwa.

Amesema ili kuweza kufanikisha uchunguzi wa haraka wa tukio hilo, Jeshi la Polisi linaomba ushirikiano kwa wananchi, ndugu, jamaa na marafiki na jamii kwa ujumla.

Alivyochukuliwa kisa Sh5 milioni

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Februari 18, 2025 jijini Mwanza, Katibu wa Chadema Wilaya ya Misungwi, Peter Manengelo, amedai kuwa katibu huyo ambaye anaishi Misungwi alipigiwa simu na rafiki yake wa kike ambaye ni msusi, akimtaka rafiki yake huyo (Katibu wa Bavicha) afike kwenye saluni yake.

“Tulimhoji huyo msusi, anasema watu hao ambao walijitambulisha kuwa ni polisi, walimpigia simu wakisema wanashida ya kusukwa aina fulani ya msuko wa nywele. Walikwenda hadi pale saluni wakawa wanasubiria kwenye foleni ya kusukwa,” amedai Obad.

Anadai baada ya kusubiri kwa muda mrefu, ilipofika saa 12 jioni, wanawake hao wawili walimgeuka yule dada msusi na kumweleza kuwa nia yao haikuwa kusukwa nywele, bali walikuwa wakimsaka Manengelo.

Anasema dada huyo amedai baada ya kumweka chini ya ulinzi wakimshurutisha ampigie simu Manengelo kwa lengo la kumshawishi afike ilipo saluni hiyo, ndipo aliridhia kisha kumpigia akimwomba afike saluni.

“Ametuambia alimpigia Manengelo na kwa sababu aliona anapigiwa na mtu anayemfahamu kuwa ni rafiki yake wa kike akaenda hapo saluni akawakuta wale watu, wakajitambulisha na kumweleza kuwa wanamtafuta kwa sababu kuna fedha fulani ilitumwa kwa rafiki yake (rafiki wa Manengelo) na huyo rafiki yake wanamtafuta kwenye simu yake lakini hapatikani,” amedai Obad.

Kwa mujibu wa Obad, watu hao walimkamata Manengelo kwa lengo la kuweka mtego wa kumkamata rafiki yake (jina linahifadhiwa) kwa madai kuwa maofisa hao walimtumia fedha Sh5 milioni kimakosa, hata hivyo, walivyomtafuta azirejeshe hakupatikana kwenye simu.

“Akiwa bado yuko pale saluni walifika wanaume wawili wakiwa na pingu wakamfunga pingu na kuondoka naye. kwa hiyo. Tangu Februari 14, 2025, Mengelo hajaonekana mpaka leo, ndugu na wana Chadema wameenda mpaka kituo cha Polisi wakaambiwa ataachiwa lakini baadaye simu zake nazo zikawa hazipatikani tena,” amedai Obad.

Kuhusu mawasiliano ya wanaodaiwa kuwa maofisa wa polisi, Obad anasema baada ya kumtia pingu Manengelo walichukua simu ya rafiki yake (msusi), wakafuta namba zao ili wasitambulike kisha kuondoka na katibu huyo.

“Ametuambia walisema wanakwenda naye kituo cha polisi atawasaidia kwa uchunguzi, lakini mpaka leo hajulikani alipo. Chadema tunataka huyo kijana apatikane, Jeshi la Polisi lina wajibu wa kulinda raia na mali zao, lina vyombo vya kuchunguza, huyo aliyempigia simu kwa kutumia namba ya yule dada waanze naye,” anasema Obad.

Alipopigiwa simu na Mwananchi, Babu wa Katibu huyo, amesema mjukuu wake ametoweka siku kadhaa zilizopita hadi leo alipopatiwa taarifa na mmoja wa viongozi

wa Chadema wilayani humo aliyemtaja kwa jina la Kimburu Mabina.

“Hadi sasa hatujamuona ila nimepewa taarifa na Kimburu Mabina ambaye ameniambia kuwa Manengelo alichukuliwa na watu hao. Bado tunafuatilia ila nilikuwa naishi naye huku Misasi wilayani Misungwi,” amesema Mohammed.

Kauli ya Mkuu wa Mkoa Mtanda

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amelitaka Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama mkoani humo kuchua hatua za haraka kufuatia kutoweka kwa Katibu wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) mkoani humo, Amani Manengelo Ijumaa wiki iliyopita.

Mtanda ameyasema hayo leo Jumanne Februari 18, 2025 jijini Mwanza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia.

Amesema kuwa amepata taarifa kuwa vijana wa Chadema wamepanga kukusanyika kesho ofisini kwake kushinikiza kuelezwa alipo kiongozi wao huyo aliyetoweka.

“Ninawakaribisheni, hii ni serikali yenu, mwananchi yeyote anapokuwa na kero yake anakaribishwa ndani ya serikali. Tahadhari yangu mje vizuri ili muondoke vizuri, kwangu unavyokuja ndivyo utakavyopokelewa, utakavyokuja ndivyo utakavyohudumiwa.

“Sasa niwatake jeshi la polisi na vyombo vya usalama Mwanza vichukue hatua ya haraka kwa huyo anayesadikika kutoweka, na nyie vijana wa chadema na nyie njooni niwakabidhi kwa polisi ili msaidiane katika kumtafuta,”amesema Mtanda.

Related Posts