Maseke aingia anga za wazee wa kujiweka

KIPA Wilbol Maseke ameingia katika orodha ya wachezaji waliojifunga Ligi Kuu Bara hadi sasa baada ya jioni ya leo kujikwamisha wavuni wakati akitaka kuokoa mpira wa kichwa uliopigwa na kiungo Hassan Nassor Maulid ‘Machezo’ wakati wakilala mabao 2-0 mbele ya JKT Tanzania.

Katika pambano hilo lililopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam, KMC ikiwa wenyeji, kipa huyo alijifunga dakika ya 68 na kuiwazawadia maafande w JKT bao la pili baada ya awali, Machezo kufunga la kwanza kwa kichwa akimalizia mpira wa frikikii uliopigwa na Najim Magulu dakika ya 10 tu ya mchezo huo uliokuwa mkali.

Maseke anakuwa mchezaji wa 10 hadi sasa kujiweka wenyewe, lakini akiwa ni kipa wa tatu msimu huu kujifunga baada ya Daniel Mgore wa Dodoma Jiji aliyefungua pazia wakati wakiumana na Mashujaa na kulala bao 1-0, kisha Mohamed Mustafa wa Azam akajifunga walipocharazwa mabao 2-1 na Tabora United katika mechi kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.

Kujifunga kwa bao hilo kwa Maseke, kumeifanya KMC kuwa miongoni mwa timu nne zilizojifunga mabao mengi hadi sasa, akiwa ni mawili kama ilivyo kwa Dodoma Jiji, Simba na Azam FC. Mbali na Maseke mchezaji mwingine wa KMC aliyejifunga alikuwa ni Fred Tangalo aliyekuwa wa pili msimu huu kujifunga baada ya Mgore wakati Wanakinondoni wakifa 4-1 mbele ya Azam FC.

Jambo usilolijua ni kwamba huu ni msimu wa pili mfululizo kwa Maseke kujifunga bao, kwani msimu uliopita alikuwa mchezaji wa tatu kati ya 12 waliojifunga akifanya hivyo katika mchezo kati ya KMC Tanzania Prisons.

Msimu huo alikuwa kipa wa pili kujifunga baada ya Mohamed Makaka wa Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja baadae kujiweka dhidi ya Geita Gold ambayo nayo ilishuka daraja.

Kwa msimu huu, beki wa Simba, Kelvin Kijili ndiye aliyekuwa mchezaji wa tatu kujifunga wakati Simba ikilala 1-0 mbele ya Yanga katika Dabi ya Kariakoo ya Kwanza iliyopigwa Oktoba 19 mwaka jana, huku mchezaji wa pili wa timu hiyo kujifunga akiwa ni Ladack Chasambi alipojiweka katika sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Fountain Gate, mjini Babati Manyara.

Chasambi alikuwa ni mchezaji wa nane kwa msimu huu kujifunga hata hivyo.

Beki wa zamani wa Azam, Yannick Bangala ndiye alikuwa mchezaji wa nne kujiweka katika mechi dhidi ya Dodoma Jiji, lakini akiwa ni wa pili kwa timu kujifunga msimu huu, wakati Dickson Mhilu aliyekuwa mchezaji wa tano kujifunga msimu huu katika pambano kati ya Dodoma Jiji na Azam, ndiye nyota wa pili wa Dodoma kujiweka msimu huu.

Wachezaji wengine wawili waliojifunga ni mabeki, Jackson Shiga wa Fountain Gate wakati timu hiyo ilipofumuliwa mabao 5-0 na Yanga, huku akiwa mchezaji wa saba msimu huu kujiweka na Lameck Lawi wa Coastal Union alikuwa ni wa tisa kujifunga wakati wa mechi dhidi yao na JKT Tanzania.

Kwa ujumla katika mechi 153 zilizochezwa hadi sasa yamefungwa jumla ya mabao 337, yakiwamo 10 ya kujifunga na mengine yaliyosaliwa yakifungwa na wachezaji wazawa na wale wa kigeni wakati ligi hiyo ikiwa raundi ya 20 na usiku huu kuna mchezo wa kufungia siku Dodoma Jiji na TZ Prisons.

1- Daniel Mgore (Dodoma Jiji) v Mashujaa

2- Fredy Tangalo (KMC) v Azam FC

3- Kelvin Kijili (Simba) v Yanga

4- Yannick Bangala (Azam) v Dodoma Jiji

5- Dickson Mhilu (Dodoma Jiji) v Azam

6- Mohammed Mustafa (Azam) v Tabora Utd

7- Jackson Shiga (Fountain Gate) v Yanga

8- Ladack Chasambi (Simba) v Fountain Gate

9- Lameck Lawi (Coastal Union) v JKT Tanzania

10-Wilbol Maseke (KMC) v JKT Tanzania

Related Posts